• Nairobi
  • Last Updated May 30th, 2023 1:21 PM
Twitter kuwazima milele wanaopotosha kuhusu chanjo ya corona

Twitter kuwazima milele wanaopotosha kuhusu chanjo ya corona

MASHIRIKA na MARY WANGARI

SAN FRANCISCO, Amerika

KAMPUNI inayomiliki mtandao wa kijamii wa Twitter Jumanne imesema itaanza kutia alama jumbe za kupotosha kuhusu chanjo ya corona.

Ilionya vilevile kwamba itawapiga marufuku watumiaji wanaozidi kusambaza habari hizo.

Tasnia hiyo ya utandawazi mnamo Jumatatu, Machi 1, ilianzisha “mfumo wa ilani” ambao hatimaye utageuka marufuku ya kudumu baada ya ujumbe wa tano wa kukera.

“Tunaamini mfumo huo utasaidia kuelimisha umma kuhusu sera zetu na kupunguza hata zaidi usambazaji wa habari hasi zinazoweza kupotosha kwenye mtandao wa Twitter,”

“Hususan kuhusu ukiukaji wa wastan na uliokithiri wa sheria zetu,” ilisema kampuni hiyo yenye makao yake San Francisco, kupitia ujumbe mtandaoni.

Watumiaji wa Twitter wataarifiwa wakati ujumbe utakapotiwa ilani au utakapohitaji kuondolewa kwa kuvunja sheria za mtandao huo, na kujishindia ilani, kulingana na kampuni hiyo.

Ilani ya pili na ya tatu matokeo yake yatakuwa kufungwa kwa akaunti inayokiuka sheria kwa muda wa saa 12.

Ukiukaji kwa mara ya nne, akaunti itazuiliwa kwa siku saba huku ilani ya tano ikisababisha akaunti kufungwa kabisa, kwa mujibu wa Twitter.

Shirika hilo la mtandao wa kijamii, mwishoni mwa mwaka jana, lilianza kuwahimiza watumiaji wake kuondoa madai hatari na ya kupotosha kuhusu COVID-19, ikiwemo mapendekezo kuwa chanjo zinatumiwa kuwadhuru au kuwadhibiti watu.

Huduma hiyo pia ililenga madai yasiyo na msingi kuhusu madhara sugu ya chanjo hizo au kuhoji uhalisia wa janga hilo.

Tangu wakati huo, Twitter imeondoa zaidi ya jumbe 8,400 na kuarifu akaunti 11.5 milioni kote duniani kuhusu ukiukaji wake wa sheria za COVID-19.

Mfumo wa ilani ni sawa na ule unaotumiwa na Twitter dhidi ya habari za kupotosha kuhusu chaguzi, uliofanya aliyekuwa rais wa Amerika Donald Trump kupigwa marufuku ya kudumu kwa ukiukaji mara kadhaa, ikiwemo lugha ambayo tasnia hiyo ilisema ingeweza kuchochea ghasia na kuhoji uadilifu katika mchakato wa upigaji kura.

Kampeni za chanjo dhidi ya COVID zinafanyika katika mataifa mengi katika juhudi za kudumisha afya za wananchi na kuwarejesha katika maisha yao kabla ya janga hilo.

You can share this post!

Everton yapepeta Southampton na kuweka hai matumaini ya...

Magavana wataka watengewe fedha za kufadhili afya, kilimo...