• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Uhuru na Kagame watoa rai kwa M23

Uhuru na Kagame watoa rai kwa M23

NA MASHIRIKA

NAIROBI, Kenya

RAIS mtaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta na Rais wa Rwanda Paul Kagame wamekubaliana kuhusu haja waasi wa M23 kukomesha vita na kuondoka maeneo walioteka mashariki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kulingana na taarifa kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Kenyatta na Kagame walikubalia, kwa njia simu, kwamba hatua hiyo ndio utatoa nafasi kwa kupatikana amani ya kudumu DRC.

“Wawili hao walikubaliana kwamba ili amani ipatikane DRC sharti pande zote mbili zisitishe vita kwanza. Awamu ya pili ya mazungumzo ya amani itafanyika jijini Luanda, Angola wiki ijayo,” EAC ikasema kwenye taarifa iliyotolewa Ijumaa jioni.

“Watu watakuwa wakisubiri ikiwa kweli M23 na wanajeshi wa serikali ya DRC wanasimamisha vita,” mwandishi wa habari wa shirika la Al Jazeera, Malcom Webbe, akasema akiripoti kutoka mji wa Goma, mashariki mwa nchi hiyo.

Aliongeza kuwa wizara ya mashauri ya kigeni ya Kenya imethibitisha kuwa Rais wa Rwanda alizungumza kwa njia ya simu na Bw Kenyatta, ambaye anaongoza mazungumzo ya amani kati ya DRC na makundi ya waasi.

“Wamekuwa wakipigana ndani ya muda wa saa 12 hivi. Kuna ripoti kwamba milio ya risasi na mabomu ingali inasikika. Haijulikani ikiwa waasi wataondoka kutoka maeneo hayo kuelekea mazungumzo hayo yaliyoratibiwa kuanza Jumatatu asubuhi,” Webbe akasema.

Katika siku za hivi karibuni, wapiganaji wa M23 wamekuwa wakikaribia Goma huku mapigano kati yao na wanajeshi wa serikali yakishika kasi.

Kundi hilo lililobuniwa mnamo 2012, liliteka eneo kubwa la DRC na kushambulia Goma kwa muda mfupi kabla ya kufurushwa na wanajeshi wa serikali wakisaidiwa na vikosi vya Umoja wa Mataifa (UN).

Waasi hao waliripotiwa kuingia Uganda na Rwanda.

Mkataba

Kundi la M23 lilitia saini mkataba wa amani na serikali ya DRC mnamo 2013 kwa ahadi kwamba wapiganaji wake wangeshirikishwa katika jeshi la kitaifa nchini humo.

Hata hivyo, kundi hilo lilianza vita tena mwishoni mwa 2021 kwa sababu ya kile walidai ni hatua ya serikali ya DRC kudinda kutimiza ahadi ya 2013.

Wapiganaji wa kundi hilo wametekeleza mashambulio matatu makubwa mashariki mwa DRC tangu Machi 2022.

Katika shambulio la hivi punde walitekeleza mwanzoni mwa Oktoba ambapo waliwaua mamia ya watu huku wengine zaidi ya 200,000 wakitoroka makwao.

  • Tags

You can share this post!

Rais aonya wauzao mihadarati, aahidi minofu Pwani

WANTO WARUI: Wanafunzi wa Gredi ya Saba ni wa shule za...

T L