• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Ulimwengu kuadhimisha Siku ya Kiswahili kesho Alhamisi

Ulimwengu kuadhimisha Siku ya Kiswahili kesho Alhamisi

NA MASHIRIKA

DAR ES SALAAM, TANZANIA

ULIMWENGU kesho Alhamisi utaadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani huku kukiwa na wito wa kutaka lugha hiyo itawazwe kuwa moja ya lugha rasmi za Umoja wa Mataifa (UN).

Maadhimisho hayo yanafanyika huku Uganda ikitangaza kuwa ufundishaji wa Kiswahili utakuwa wa lazima katika shule za msingi na sekondari.

Baraza la Mawaziri nchini humo lilisema kuwa lilichukua hatua hiyo kufuatia uamuzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kufanya Kiswahili kuwa lugha rasmi.

Kesho Alhamisi itakuwa mara ya kwanza kuadhimishwa kwa siku hiyo tangu Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) kuteua Julai 7 kuwa Siku ya Kiswahili Duniani.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan jana Jumanne aliambia Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kuwa maadhimisho hayo ni heshima kubwa kwa ukanda wa Afrika Mashariki, ambako Kiswahili huzungumzwa na idadi kubwa ya watu.

“Maadhimisho haya yana maana kubwa kwetu kwamba sisi wenye chimbuko la lugha ya Kiswahili tumetambuliwa kimataifa.

“Ni heshima kubwa kwa taifa letu, Afrika Mashariki na hadhi ya maeneo yote ambapo Kiswahili kinazungumzwa. Hata Ulaya na Amerika watu wanasoma sana Kiswahili. Sasa kuwekwa siku hii maalumu ya kimataifa ya Kiswahili, itafanya watu wakisome sana Kiswahili,” akasema Rais Suluhu.

Kiswahili tayari kimetawazwa kuwa lugha rasmi ya Umoja wa Afrika (AU).

Kulingana na Unesco, Kiswahili ndiyo lugha inayozungumzwa na idadi kubwa ya watu barani Afrika.Pia ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa na idadi kubwa zaidi ya watu duniani.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 200 kote duniani.Rais Suluhu ameapa kutumia Kiswahili iwapo atapata fursa ya kuhutubia kongamano la UN katika siku za usoni.

“Kiswahili tayari kimeidhinishwa kuwa lugha rasmi ya EAC, Jumuiya ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC) na AU. Sasa tumeanza juhudi za kuhakikisha kuwa kinagonga hodi pia kwenye Umoja wa Mataifa,” akasema Rais Suluhu.

Maudhui ya maadhimisho ya mwaka huu ni: ‘Kiswahili kwa Amani na Ustawi’.

Lengo hasa la maadhimisho haya ya mwaka ni kusongesha matumizi ya lugha ya Kiswahili kama nguzo ya amani, na ustawi na wakati huo kuimarisha tamaduni mbalimbali.

Uganda imekuwa inaendelea na utafiti kote nchini kupitia Idara ya Lugha ya Chuo Kikuu cha Makerere kwa lengo kubaini kwa nini lugha ya Kiswahili haikui kama inavyotarajiwa katika nchi hiyo mwanachama mkongwe wa EAC.

Ulimwengu unaadhimisha siku ya Kiswahili huku kukiwa na mjadala mkali nchini Tanzania ikiwa lugha hiyo isitumike kufundishia katika shule za msingi au la.

“Hili limeshajadiliwa sana Tanzania, wananchi wamelijadili, bungeni wamelijadili. Wizara ya elimu sasa iko kwenye hatua za kuhoji wananchi kuhusu mabadiliko ya mitaala,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Gor yasaka kocha mpya baada ya kumtema Spier

Uhuru kuacha raia katika kona mbaya

T L