• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:39 AM
UN kuchunguza mauaji ya watoto katika nchi 3

UN kuchunguza mauaji ya watoto katika nchi 3

NA MASHIRIKA

GENEVA, USWISI

UMOJA wa Mataifa (UN) utaanzisha uchunguzi kuhusiana na mauaji ya watoto nchini Ukraine, Ethiopia na Msumbiji.

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres, alisema hayo katika ripoti iliyoonyesha kuwa watoto 8,070 waliuawa au kujeruhiwa vibaya katika mapigano mwaka 2021 kote duniani.

Watoto 6,310 walisajiliwa katika makundi ya uhalifu kote duniani mnamo 2021.

Nchi zilizo kwenye orodha ya Amerika kwa kuongoza kusajili watoto katika makundi ya kupigana ni Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Libya, Nigeria Myanmar, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Syria na Yemen.

Ripoti hiyo inasema kuwa jumla ya watoto 23,982, wengi wao wakiwa wavulana, waliathiriwa na vita katika nchi 21.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa visa vya watoto kudhulumiwa kingono, kutekwa nyara, kuvamiwa shuleni na hospitalini viliongezeka mwaka jana ikilinganishwa na 2020.

Ripoti hiyo inasema kuwa visa vingi vya dhuluma dhidi ya watoto mwaka jana viliripotiwa Yemen, Syria, Afghanistan, DRC, Somalia, Israeli na Palestina.

Guterres alisema kuwa UN itachunguza mauaji ya watoto katika nchi ambazo sasa zinakumbwa na mapigano kama vile Ukraine, Ethiopia na Msumbiji.

Balozi wa UN kuhusu watoto, Virginia Gamba, alisema kuwa kuwa wanajeshi wa Urusi nchini Ukraine wamekuwa wakishambulia shule na hospitali hivyo kuhatarisha maisha ya watoto.

Umoja wa Mataifa wiki iliyopita, ulisema kuwa zaidi ya watoto 300 wameuawa katika machafuko Ukraine tangu Urusi ilipovamia nchi hiyo Februari mwaka huu.

Kulingana na ripoti, wanajeshi wa Israeli waliua watoto 78 wa Palestina, kujeruhi vibaya wengine 982 na kuweka kizuizini 637 mwaka 2021, kwa mujibu wa ripoti.

Wanajeshi wanaoongozwa na vikosi vya Saudi Arabia waliua watoto 100 nchini Yemen ndani ya kipindi hicho.

“Hali ikiendelea hivyo mwaka huu, Israeli itaingizwa kwenye orodha ya nchi hatari zaidi kwa watoto,” alionya Guterres.

Mnamo Aprili, UN ilipiga kura kuondoa Urusi kutoka katika Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Kibinadamu. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kubainika kuwa wanajeshi wa Urusi waliua watoto katika eneo la Bucha nchini Ukraine.

Miili ya watu waliouawa kinyama iligunduliwa baada ya wanajeshi wa Urusi kuondoka eneo la Bucha.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa watoto 70 waliuawa nchini Iraq na wengine maelfu wanazuiliwa seli au magerezani kwa madai ya kutishia usalama wa nchi.

Ripoti hiyo ilitolewa siku moja baada watoto saba kuangamia nchini Togo katika mlipuko wa bomu uliotokea kijijini Tone Prefecture, kaskazini mwa nchi hiyo, Jumapili.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Vyama vya UDA na ODM vilikosea kutunuku...

Wavuvi walia nyavu mbovu zikipunguza samaki ziwani

T L