• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Urusi sasa yasema iko tayari ‘kuokoa’ Afrika

Urusi sasa yasema iko tayari ‘kuokoa’ Afrika

NA MASHIRIKA

KAMPALA, UGANDA

URUSI imesema kuwa iko tayari kuiuzia Afrika mafuta na ngano yake bila vikwazo vyovyote.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, akishikilia kuwa Afrika ni mojawapo ya washirika wa karibu wa taifa hilo.

Lavrov alitoa kauli hiyo huku ubalozi wa Amerika nchini Uganda ukitoa hisia kali dhidi ya Urusi.

Jumatatu, Lavrov alikutana na Rais Yoweri Museveni wa Uganda jijini Entebbe, walikojadili kuhusu suala la kupanda kwa bei za mafuta na chakula, kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari.

“Huwa tunauza mafuta kwa mataifa yanayotaka. Ikiwa kuna nchi inayotaka kununua mafuta yetu, iwe India ama nchi ya Afrika, hakuna vikwazo vyovyote kwa hili,” akasema waziri huyo.

Akaongeza: “Hatuuzi mafuta pekee, bali huwa tunatoa usaidizi kama kuyasaidia mataifa hayo kujenga miundomsingi muhimu kama vile viwanda vya kusafisha mafuta. Kwa hayo, tumejitolea kuendesha mazungumzo na wenzetu Uganda.”

Lavrov yuko kwenye ziara ya mataifa manne barani Afrika. Alianza ziara yake nchini Misri, akaelekea DRC Congo na baadaye Uganda.

Baada ya Uganda, amepangiwa kuelekea nchini Ethiopia. Alisema Afrika ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa sana kutokana na vikwazo vya kiuchumi ambavyo vimewekewa nchi yake.

Lakini mara tu baada ya kuwasili nchini Uganda, ubalozi wa Amerika nchini humo ulionekana kukosoa ziara yake kwenye jumbe kadhaa ulioandika kwenye mtandao wa Twitter.

AMERIKA

Ubalozi huo uliikosoa vikali serikali ya Rais Museveni kwa kukosa kudhibiti bei za mafuta na chakula nchini humo.

“Tunalishukuru Shirika la Chakula Duniani (WHO) kwa juhudi zake kuendelea kuwasaidia watu walioathiriwa na bei ya juu ya vyakula kutokana na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, hata bila kuchokozwa kwa namna yoyote ile,” ukaeleza Ubalozi huo kwenye taarifa.

Ukraine na Urusi ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uzalishaji mkubwa wa ngano duniani.

Hata hivyo, uzalishaji wake umeathiriwa pakubwa na vita vinavyoendelea kati ya nchi hizo mbili.

Bei za nafaka zimepanda pakubwa katika sehemu tofauti duniani kutokana na uhaba wake.

Kutokana na vita hivyo, mataifa kadhaa ya Ulaya yaliiwekea Urusi vikwazo vikali vya kiuchumi, hali iliyoizuia kuendelea kuuza mafuta na gesi yake huko.

Ijapokuwa vikwazo hivyo havijaathiri uuzaji vyakula moja kwa moja, vimezizuia benki za Urusi dhidi ya kutumia mfumo wa malipo wa kimataifa, ambao ungerahisisha uuzaji na ulipaji wa nafaka inazouzia nchi tofauti.

Ukraine pia haiwezi kuuza ngano yake kwa sasa, kwani bandari zake muhimu zinashikiliwa na Urusi, hivyo kuzuia safari zozote za meli.

Wiki iliyopita, mataifa hayo mawili yalikubali kufungua bandari zake kufuatia mazungumzo yaliyoendeshwa na Uturuki.

Licha ya mazungumzo hayo, wadasisi wanasema kuwa itachukua wiki kadhaa kabla ya bandari zote kufunguliwa.

  • Tags

You can share this post!

Aston Villa wampa kiungo John McGinn utepe wa unahodha

TAHARIRI: Serikali iepuke kuwasaliti raia kila...

T L