• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
TAHARIRI: Serikali iepuke kuwasaliti raia kila inapowahamisha

TAHARIRI: Serikali iepuke kuwasaliti raia kila inapowahamisha

NA MHARIRI

IMEIBUKA kuwa maelfu ya watu waliotolewa kwa nguvu na serikali katika Msitu wa Mau, Kaunti ya Narok, sasa wanaishi katika hali za kusikitisha kwenye kambi wa wakimbizi wa ndani kwa ndani (IDPs).

Wengi wanaishi katika kambi za Tendwet na Ol-Mekenyu, eneo la Narok Kusini, wakisema wamelazimika kufanya vibarua ili kujikimu kimaisha, hasa kununua chakula.

Wakati serikali ilikuwa ikiwatoa watu hao kwenye msitu huo, walipewa kila ahadi kwamba wangetafutiwa makao mbadala baaadaye, ikiwa ingebainika kuwa ardhi walizokuwa nazo katika Msitu wa Mau walikuwa wamezipata kwa njia halali.

Hata hivyo, wengi wanasema hakuna ahadi hata moja iliyotimizwa kati ya zile ambazo walipewa na maafisa wa serikali walioendesha operesheni ya kuwafurusha kutoka msitu huo.

Kimsingi, serikali inafaa kuhakikisha kuwa ina makao mbadala kila wakati inapowahamisha raia kutoka eneo moja hadi nyingine.

Ni sikitiko wakati wananchi wanatolewa katika eneo moja kwa kisingizio cha serikali kuanzisha miradi, na baadaye kuachwa bila usaidizi wowote.

Ni sawa na serikali kuwasaliti raia wake.

Kando na suala la Mau, si mara ya kwanza wananchi kutolewa kwenye makazi yao na kuahidiwa kupewa makao mbadala, ikiwa wataipa nafasi serikali kuendesha miradi muhimu kama vile ujenzi wa barabara.

Mara nyingi, idara zinazohusika huwa zimetengewa fedha za kutosha ili kuwalipa waathiriwa kama fidia.

Usaliti huo pia ulijitokeza kwenye mikakati ya serikali ya marehemu Mwai Kibaki kuwasaidia watu walioathiriwa na vita vya baada ya uchaguzi wa 2007 kuwatafutia makao mbadala.

Baada ya vita hivyo, Wizara ya Fedha ilisema ilitoa zaidi ya Sh4 bilioni kwa Wizara ya Ardhi ili kuwanunulia mashamba watu waliofurushwa kutoka makazi yao, hasa katika eneo la Bonde la Ufa.

Hata hivyo, ilibainika baadaye kuwa ni watu wachache tu waliolipwa fidia au kupata mashamba, kati ya watu zaidi ya 600,000 walioathiriwa na vita hivyo.

Mzozo huo ulisababisha mchipuko wa makundi tofauti ya waathiriwa, wakidai kuwa serikali iliwahadaa kwamba ingewalipa fidia au kuwanunulia mashamba.

Mivutano hiyo kati ya wizara hizo mbili iliendelea hadi pale Rais Kibaki aling’atuka uongozini mnamo 2013.

Hadi sasa, idadi kubwa ya watu waliofurushwa makwao kwenye vita hivyo bado wako kwenye kambi katika sehemu tofauti nchini.

Kinaya ni kuwa, baadhi ya wanasiasa waliokuwa wakisimamia wizara hizo bado wako huru, huku wengine wakishikilia nyadhifa muhimu sana serikalini.

Wito mkuu kwa serikali ni kuhakikisha kuwa kuna mipango kabambe kila wakati inapanga kuwahamisha raia kutoka eneo moja hadi nyingine ili kuendesha miradi.

Ni makosa kuwaacha raia kuteseka kutokana na ukosefu wa mpangilio mzuri kwenye uendeshaji wa miradi yake.

  • Tags

You can share this post!

Urusi sasa yasema iko tayari ‘kuokoa’ Afrika

VALENTINE OBARA: Wapwani waunge juhudi zote za kuhifadhi...

T L