• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:50 AM
Urusi yashtaki majeshi ya Ukraine kwa ‘uhalifu’

Urusi yashtaki majeshi ya Ukraine kwa ‘uhalifu’

NA MASHIRIKA

MOSCOW, URUSI

URUSI imewafungulia mashtaka wanajeshi 92 wa Ukraine kwa tuhuma za uhalifu wa kivita.

Msimamizi mkuu wa kamati ya uchunguzi ya Urusi (RIC), Alexander Bastrykin, aliiambia tovuti ya habari ya Rossiiskaya Gazeta kwamba tayari, wameanza kuchunguza visa zaidi ya 1,300 vya uhalifu wa kivita na kibinadamu, vinavyodaiwa kutekelezwa na wanajeshi hao.

Vile vile, alipendekeza kubuniwa kwa jopokazi la kimataifa kuchunguza na kuendesha mashtaka dhidi ya wanajeshi hao.

Urusi inasema kuwa jopo hilo litaungwa mkono na washirika wa Urusi kama Iran, Syria na Bolivia.

Kando na wanajeshi hao 92, mkuu huyo alisema Urusi inawasaka watu 96, miongoni mwao waliwemo makamanda 51 wa kijeshi waliojihami vikali.

“Wanajeshi hao walihusika kwenye vitendo vya uhalifu wa kivita,” akasema Bastrykin, kwenye mahojiano na shirika hilo.

Kufikia Jumatatu, Ukraine haikuwa imetoa taarifa yoyote kuhusiana na tukio hilo.

Mwezi huu wa Julai pia, Ukraine ilisema inachunguza zaidi ya visa 21,000 vya uhalifu wa kivita inavyodai vilitekelezwa na majeshi ya Urusi katika himaya yake tangu taifa hilo lilipoanza uvamizi dhidi yake Februari 24, 2022.

Mnamo Mei, Ukraine ilifanya kikao cha mashtaka dhidi ya wanajeshi hao, ambapo kamanda mmoja wa kijeshi wa Urusi alifungwa gerezani kwa kupatikana na hatia ya kumuua mtu mmoja raia wa Ukraine.

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) pia imewatuma maafisa wake kadhaa kuchunguza visa vya uhalifu wa kivita nchini humo.

ICC imeitaja hali ilivyo Ukraine kama “eneo la uhalifu wa kivita.”

Hata hivyo, Urusi imekuwa ikikanusha madai ya vikosi vyake kuwalenga raia kwenye operesheni zao Ukraine.

Badala yake, Urusi imekuwa ikivilaumu vikosi vya Ukraine kwa madai ya kuwaua raia wake na kuharibu miundomsingi yake, ambapo baadaye huwa inailaumu Urusi kwa kutekeleza visa hivyo.

Madai hayo hata hivyo yamekuwa yakipuuzwa vikali na viongozi wa mataifa kadhaa, ambayo ni washirika wa Ukraine.

Alipoulizwa kuhusu ikiwa wataruhusu uwepo wa jopo maalum lililobuniwa na Umoja wa Mataifa (UN) kuendesha kesi hizo, Bastrykin aliyalaumu mataifa ya Magharibi kwa “kuipendelea na kuifadhili Ukraine.”

Alisema kuwa Urusi ina tashwishi kubwa kuhusu uwepo wa jopo kama hilo.

Urusi imekuwa ikidai kuwa mataifa ya Magharibi ndiyo yanaendesha vita vya Ukraine, kwa kisingizio cha kuisaidia kutetea himaya yake inayoshikiliwa na Urusi.

Mkuu huyo alipendekeza kubuniwa kwa jopokazi huru katika mataifa ambayo hayajaonyesha kuegemea upande wowote kwenye mzozo huo.

Alipendekeza jopo kubuniwa nchini Syria, Iran ama Bolivia.

Mnamo Machi, Syria na Iran zilipiga kura kupinga hoja ya UN kuilaumu Urusi kwa kuivamia Ukraine.

Bolivia ilisusia kupigia kura hoja hiyo.

Mkuu huyo alisema pia Urusi inaendesha uchunguzi kuhusu tuhuma za Ukraine kutengeneza silaha za maangamizi ya halaiki.

  • Tags

You can share this post!

Wavenezuela: Chebukati abaki kimya

Omar adai ODM imekosa ajenda

T L