• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Viongozi Afrika wahimizwa waangazie suala la usawa wa kijinsia katika sekta ya afya

Viongozi Afrika wahimizwa waangazie suala la usawa wa kijinsia katika sekta ya afya

NA PAULINE ONGAJI

VIONGOZI wa Afrika wameombwa kuingilia kati kuhakikisha kwamba wanaangazia suala la usawa wa kijinsia katika sekta ya afya barani.

Kwenye kikao kilichoandaliwa katika makala ya pili ya Kongamano la Kimataifa kuhusu Afya ya Umma barani (CPHIA 2021) lililong’oa nanga Jumanne jijini Kigali, Rwanda, wanawake wanaowakilisha vikundi kutoka sekta tofauti za afya barani, walisisitiza umuhimu wa wanawake kupewa kipaumbele katika huduma za afya.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Taasisi ya Huduma ya Afya na Ustawi Duniani (Institute of Global Health and Development) Dkt Magda Robalo, amesema kwamba licha ya kuwa wanawake huwa mstari wa mbele katika kutoa huduma za afya, inapowadia wakati wa kutoa maamuzi na kuchangia sera katika fani hii, bado wanasalia nyuma.

Huku akizungumza kupitia mtandaoni, Bi Winnie Byanyima, Mkurugenzi Mtendaji wa  UNAIDS, amesema kwamba umaskini, taasubi ya kiume na dhuluma dhidi ya wanawake vimezuia uwezo wa wanawake kufikia huduma za afya, vile vile kuhudumu katika sekta hii.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani WHO, wanawake barani Afrika wanawakilisha zaidi ya nusu ya vifo vya wanawake ulimwenguni vinavyosababishwa na maradhi ya kuambukizwa na matatizo wakati wa kujifungua.

Masaibu haya kwa kiwango fulani, alisema, yamechangiwa na uhaba wa wanawake katika nafasi za juu katika sekta ya afya, licha ya kuwakilisha asilimia kubwa ya wahudumu.

“Kwa mfano barani Afrika, asilimia 65 ya wahudumu wanaofanya kazi katika sekta ya afya ni wanawake, lakini wale ambao ni madaktari hawazidi asilimia 30. Hii inamaanisha Kwamba hata katika uundaji sera, mpango na kuunda bajeti ya huduma ya afya hawako,” aliongeza.

“Hii ilidhihirika wakati wa gonjwa la COVID 19 ambapo wahudumu wa kiafya wa kike walikuwa mstari wa mbele kuhudumia wagonjwa, ilhali hawakuhusishwa katika majopo ya kitaifa ya maamuzi,” alisema Bi Faith Nfii, mratibu wa mipango kwenye jopokazi la umma katika kituo cha Afrika cha kudhibiti na kuzuia maradhi barani Afrika, (Africa CDC).

Kulingana na Dkt Stellah Bosire, Mkurugenzi Mtendaji katika shirika la Africa Center for Health Systems and Gender, mojawpao ya mambo yanayochangia matatizo haya ni kwamba hakuna miunganisho rasmi ya wanawake katika sekta ya afya.

“Hatufuatilii na hakuna vipimo vya kuangazia usawa wa kijinsia kazini katika sekta hii,” aliongeza.

Kulingana na Dkt Mary Muchekeza, kutoka Wizara ya Afya na huduma kwa watoto nchini Zimbabwe, mambo ni mabaya hata zaidi kwa wanawake ambao mbali na kuwa wanahudumu katika sekta hii, pia wanaishi na ulemavu.

Bi Byanyima alisistiza umuhimu wa wanawake kuhusishwa katika nafasi za juu za sekta ya afya na serikalini.

“Ili Afrika itimize ndoto ya kutoa afya kwa wote, kuna haja ya kuwa na mtazamo mpya na kuona wanawake kama ala za kuchangia suluhu za afya,” alisema Dkt Muchekeza.

Kulingana na Dkt Norah Obudho, mkurugenzi wa mipango eneo la Afrika Mashariki katika shirika la WomenLift Health (for the motion), ingawa pengo linagalipo, mengi yameafikiwa.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Magenge ya wahalifu yaacha wakazi na makovu tele Nakuru

SHINA LA UHAI: Fahamu chakula unachofaa kula baada ya...

T L