• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:39 AM
Viongozi wa Ulimwengu wamwomboleza Malkia Elizabeth II

Viongozi wa Ulimwengu wamwomboleza Malkia Elizabeth II

NA MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

VIONGOZI kote ulimwenguni wameungana kuomboleza kifo cha Malkia Elizabeth wa Uingereza ambaye alifariki dunia kwa utulivu Alhamisi jioni katika kasri la Balmoral.

Kiongozi huyo aliyetawala kwa miaka 70 alipendwa zaidi ulimwenguni kwani alipende kuzuru mataifa mbalimbali yakiwemo yale ya bara la Afrika.

Mfalme mpya Charles III alisema, “Tunaomboleza kifo cha kiongozi mpendwa na Mama wetu. Najua kuondoka kwake kumeathiri raia wengi kote nchini, mataifa ya Jumuia ya Madola na watu wengin kote ulimwenguni.”

Waziri Mkuu mpya wa Uingereza Liz Truss alisema: “Tumevunjwa moyo na habari ambazo tumesikia kutoka Blamoral.

“Kifo cha Mstahiki Malkia kimeshtua taifa na ulimwengu kwa ujumla.”

Alikamilisha taarifa yake kwa kutamkia maneno: “Mungu saidia Mfalme.”

Rais wa Amerika Joe Biden alisema: Malkia Elizabeth II nyakati zote aliongoza kwa upendo na alionyesha kujitolea kwake katika kutekelezaji majukumu yake. Alivumilia hatari na changamoto za Vita vya Ulinwengu pamoja na watu wa Uingereza na aliwaongoza Waingereza wakati wa janga la Covid-19 huku akiwapa matumaini ya siku nzuri zijazo.”

Akaongeza: “Tunatuma rambirambi zetu kwa Familia ya Kifalme, ambayo inaomboleza sio tu Malkia wao bali mama na nyanya. Kumbukumbu zake zitadumu katika kusara za historia ya Uingereza na stori ya ulimwenguni wetu.”

Rais Biden ameamuru kwamba bender azote nchini Amerika zipeperushwe nusu mlingoti.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pia alikuwa mojawapo wa viongozi wa kwanza ulimwenguni waliotoa rambirambi zao kufuatia kifo cha Malkia Elizabeth.

Akasema: “Mstahiki Malkia Elizabeth II alipalilia umoja wa Uingereza kwa zaidi ya miaka 70.

“Nakumbuka kama rafiki mkubwa wa Ufaransa, Malkia mkarimu ambayo ameacha kumbukumbu ya kudumu nchini mwake katika katiba karne hii.”

Kiongozi wa Ireland Micheal Martin pia alituma rambirambi zake kufuatia kifo cha Malkia.

Martin akasema: “ Uongozi wa Malkia ulikuwa wa kihistoria, yenye manufaa na uliopendwa na kuenziwa kote ulimwenguni.

“Alidhihirisha kujitolea kwake kutekeleza wajibu wake kwa hekima na ujuzi wa kipekee.

“Kwa hakika kifo cha Malkia ni mwisho wa kipindi muhimu katika historia ya ulimwengu.

“Ziara yake rasmi nchini Ireland mnamo 2011 ilikuwa mwanzo wa kurejeshwa kwa uhusiano kati yetu na jirani wetu karibu-Uingereza.

Martin alisema ziara hiyo ilifaulu kwa kikubwa kutokana na hotuba nzuri ambazo Malkia huyo alitoa wakati wa ziara yake nchini Ireland.

Aliyekuwa Rais wa Amerika Barack Obama alisema: “Michelle na mimi tulikuwa na bahati ya kumjua Malkia na alikuwa kielelezo kubwa zaidi kwetu. Kila mara alionyesha upendo kwa walimwengu na alifahamu jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha.”

Naye Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau alituma ujumbe kupitia twitter akisema : “Tunasikitika zaidi kujulishwa kuhusu kifo cha Mstahiki Malkia Elizabeth II.

“Uwepo wake ulidhihirika maishani mwetu na huduma alizotoa kwa watu wa Canada daima zitasalia kuwa sehemu kubwa ya historia yetu kama taifa,” Trudeau akasema.

Wengine waliotuma rambirambi zao ni, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, Rais wa Ureno Marcelo Rebelo de Sousa, na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

  • Tags

You can share this post!

Chelsea waajiri kocha Graham Potter kujaza pengo la Thomas...

Tafrija wanajeshi wakimuaga Uhuru

T L