• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Wakenya 2 kati ya 19 waliokufa ajalini TZ

Wakenya 2 kati ya 19 waliokufa ajalini TZ

BUKOBA, TANZANIA

WAKENYA wawili ni miongoni mwa watu 19 waliofariki kwenye ajali ya ndege ya shirika la Precision Air kutoka Tanzania, iliyoanguka katika Ziwa Victoria mnamo Jumapili asubuhi.

Wawili hao ni Bw Peter Odhiambo, aliyekuwa mhudumu wa ndege hiyo na Bi Eunice Ndirangu.

Taifa hilo jana Jumatatu lilifanya ibada maalum kwa ajili ya 19 hao walioaga dunia.

Mazishi hayo yalifuata taratibu za dini za Kikristo na Kiislamu, kwani walioaga ni washirika wa dini hizo mbili.

Ibada kabla ya mazishi ilifanyika katika Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba, ambapo iliongozwa na viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu.

Miongoni mwa waliohudhuria ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwenye hotuba yake, Majaliwa aliziagiza idara husika kuchunguza kiini halisi cha ajali hiyo.

Vile vile, aliagiza maafisa husika kutoa idadi kamili ya watu waliokuwepo katika ndege hiyo, kwani taarifa za awali zilisema ilikuwa imewabeba abiria 43, ijapokuwa idadi hiyo ilibainika baadaye kuwa 45.

Wakati huo huo, Kamishna wa eneo la Kagera, Albert Chalamila, jana Jumatatu alitoa majina kamili ya watu waliopoteza maisha yao katika ajali hiyo.

Wafu hao wanajumuisha mtawa wa Kanisa Katoliki ambaye jina lake halikubainika mara moja.

Ndege hiyo aina ya PW 494-5H-PWF ilikuwa ikisafiri kutoka Dar es Salaam ikielekea Mwanza kupitia Bukoba, ilipopata ajali hiyo.

Ndege hiyo ilikuwa ikijitayarisha kutua katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba, ilipoanguka.

Kwingineko, shirika moja lisilo la kiserikali lilipata pigo kubwa, baada ya wafanyakazi wake watano kufariki katika ajali hiyo.

Wafanyakazi watano wa shirika la Management and Development for Health (MDH) walikuwa miongoni mwa watu 19 waliofariki.

Hata hivyo, wafanyakazi wake watatu walikuwa miongoni mwa watu 24 waliookolewa na kupelekwa hospitalini.

Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika hilo, David Sando, alisema kuwa wafanyakazi hao wanane walikuwa wakielekea mjini Tabora kupitia Mwanza kwa shughuli za kikazi. Wafanyakazi hao wanajumuisha wanawake watatu na wanaume watano.

“Tulikuwa na wafanyakazi wanane katika ndege hiyo. Baadhi yao bado wako hospitalini,” akasema.

Waliofariki walitambuliwa kama Boniphace Jullu, Alice Simwinga, Sauli Epimack John, Neema Faraja na Zacharia Mlacha. Waliookolewa walitambuliwa kama Josephine Mwakisambwe, Felix Otieno na Nixon Jackson.

Hapo jana Jumatatu, ripoti zilianza kuibuka kuhusu yale yaliyofanyika kabla ajali hiyo kufanyika.

Akirejelea matukio hayo, Richard Komba, aliyekuwa miongoni mwa wale walionusurika, alisema hali ya hewa ilibadilika ghafla walipokuwa wakikaribia kutua mjini Bukoba.

“Hali ya hewa iliendelea kudorora tulipoendelea kukaribia Bukoba,” akasema kutoka hopitalini alikolazwa.

Ndege hiyo ilipokaribia Uwanja wa Ndege wa Bukoba, ilibainika ilikuwa vigumu kutua. Rubani aliwaambia abiria kuwa mvua ilikuwa ikinyesha sana na hakuwa akiona vizuri.

“Alisema ikiwa hali hiyo ingeendelea, angelazimika kurejea katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza. Ilitangazwa angefaulu kutua licha ya hali mbaya ya hewa,” akaongeza.Hata hivyo, ndege ilianguka ghafla katika Ziwa Victoria na kuzama.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Mawaziri wakome kutoa kauli kiholela

TUSIJE TUKASAHAU: Kwa kuvipuuza vyuo vikuu Kenya Kwanza...

T L