• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 9:50 AM
Wakuu wa shule waadhibiwa kwa kuruhusu watoto kucheza wimbo wa Zuchu ‘Honey’

Wakuu wa shule waadhibiwa kwa kuruhusu watoto kucheza wimbo wa Zuchu ‘Honey’

Dar es Salaam, Tanzania

NA MWANANCHI COMMUNICATIONS LIMITED

Baada ya kusambaa kwa kipande cha video kinachowaonyesha wanafunzi wa shule za msingi wakicheza wimbo wa msanii Zuchu ‘Honey’ wilayani Tunduma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda ameagiza walimu wakuu wa shule hizo wavuliwe vyeo.

Amesema hayo Novemba 2, 2023 nje ya Bunge jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu video hiyo ambapo pia amepiga marufuku wanafunzi kucheza nyimbo zisizo na maadili na kuwataka walimu kuwa wasimamizi wa maadili pindi wanafunzi wanapokuwa shuleni.

Video hiyo ambayo imejipatia zaidi ya ‘views’ milioni 16 kwenye YouTube, inamuonyesha mwanamuziki huyo ambaye jina lake kamili ni Zuhura Othman akiwa kwenye mazingira ya chumbani huku staili yake ya kudensi ikiwa ya michezo ya chumbani.

“Tumeshatambua shule yenyewe iko Tunduma, kulikuwa na kikundi kimeenda kutoa msaada shuleni pale, baada ya kutoa msaada ule kikaweka na muziki halafu wanafunzi wakacheza, na maudhui ya muziki wenyewe kila mtu ameuisikia sina haja ya kuurudia.

“Tumeongea na wadhibiti ubora wapeleke taarifa kule, mkurugenzi awaondoe walimu wakuu wa shule mbili; moja shule ya Tunduma na nyingine ambazo ni kama shule pacha, waondolewe madaraka ya ukuu wa shule, watafutwe wakuu wengine wa shule. Tunafanya hivi kutuma ujumbe, walimu wakuu tusaidieni msiruhusu vitu kama hivi viingie shuleni,” akasema Profesa Mkenda.

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt Dorothy Gwajima, amempongeza Profesa Mkenda kwa kukemea kitendo hicho na kutoa wito kwa watoa huduma wote na wanaohudumia watoto kusimamia malezi na makuzi ya watoto.

  • Tags

You can share this post!

Sauti Sol kupiga densi ya mwisho leo na kuachana rasmi

Huyu Defoe hapoi, anaye Alisha lakini bado anachovya mzinga...

T L