• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Wanajeshi wawaachilia wafungwa wa kisiasa Guinea

Wanajeshi wawaachilia wafungwa wa kisiasa Guinea

Na MASHIRIKA

CONAKRY, Guinea

VIONGOZI wa kijeshi waliotwaa uongozi nchini Guinea baada ya kumpindua Rais Alpha Conde, wamewaachilia huru wafungwa wote wa kisiasa waliompinga kiongozi huyo.

Viongozi hao walitangaza kuwaachilia jumla ya wafungwa 80, wakitaja hatua hiyo kama “mwanzo mpya.”

“Tunataka kuwa na ukurasa mpya katika nchi hii. Tunawaahidi raia kwamba tutarejesha uzingatiaji wa haki za binadamu,” akasema Luteni Kanali Mamady Doumbouya, ambaye ndiye aliongoza mapinduzi hayo.

Watu hao walikuwa wamefungwa gerezani kwa kuukosoa utawala wa Rais Conde.

Jumatano, viongozi wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) walitarajiwa kufanya kikao maalum kujadili mapinduzi hayo na utaratibu wa mpito nchini Mali.

Rais Conde alipinduliwa na makomando wa kijeshi mnamo Jumapili.

Doumbouya alimlaumu vikali Rais Conde, 83, kwa tuhuma za ufisadi, ukiukaji wa haki za binadamu na kudorora kwa hali ya uchumi.

Ismael Conde, ambaye alikuwa miongoni mwa wafungwa hao, alisema alipitia hali ngumu sana.

Hata hivyo, alisema ana matumaini mapya kwa mustakabali wa taifa hilo.

Mfungwa huyo ni mwanachama wa chama cha upinzani cha UFDG.

“Ni hali ya kipekee sana. Tulipitia hali ngumu sana gerezani kwa miezi 12 ambayo tulikuwa tumezuiliwa. Ni vigumu kueleza jinsi tunavyohisi,” akasema.

Naye mwanaharakati alikuwa miongoni mwa walioachiliwa.

“Tumeteseka sana tukiwa gerezani. Sitaki turudie makosa waliyofanya watangulizi wetu. Ni matumaini yangu kuwa utawala mpya wa kijeshi utachukua hatua za haraka ili kuleta hali ya maridhiano kuliwezesha taifa hili kusonga mbele,” akasema Mamady Onivogui, ambaye ni mwanaharakati wa haki za binadamu na masuala ya demokrasia.

Taifa hilo ni miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani.

Hata hivyo, ndilo taifa la pili duniani kwa kuzalisha madini aina ya alumini kwa wingi.

Bei za madini hayo zimepanda maradufu tangu mapinduzi hayo kutokea. Wakati huo huo, utawala huo uliongeza udhibiti wake katika taifa hilo baada ya kuwateua maafisa wa kijeshi kuwa wakuu wa majimbo manane.

Hata hivyo, shirika la ECOWAS limetishia kuuwekea vikwazo utawala huo ikiwa hautafuata taratibu zitakazopitishwa ili kurejesha uongozi kwa raia.

Kabla ya mapinduzi hayo, Rais Conde alikuwa akilaumiwa pakubwa kutokana na hali mbaya ya uchumi iliyoandamana na athari za janga la virusi vya corona.

Mwaka 2020, Conde alibadilisha katiba, ambapo ilimruhusu kuwania urais kwa muhula wa tatu mwezi Oktoba.

Hatua hiyo ilizua maandamano makubwa, huku mamia ya waandamanaji wakiuawa.

Conde alitangazwa kuwa mshindi kwenye uchaguzi huo ijapokuwa upinzani ulishikilia haukuwa huru wenye uwazi.

Licha ya ahadi mpya za uongozi huo, wadadisi wanasema kwamba una kibarua kikubwa kujenga imani yake miongoni mwa raia.

You can share this post!

Wito viongozi wa kisiasa wasitishe kampeni za mapema

Serikali yatangaza ukame kuwa janga