• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Watafiti waibua hofu ya silaha za nyuklia kuzidi

Watafiti waibua hofu ya silaha za nyuklia kuzidi

NA AFP

STOCKHOLM, USWIDI

IDADI ya silaha za nyuklia duniani inatarajiwa kuongezeka katika mwongo mmoja ujao, taharuki na mapigano kati ya nchi tofauti zikiendelea, walisema watafiti mnamo Jumatatu.

Hili linajiri huku mapigano kati ya Urusi na Ukraine yakiendelea kuchacha.

Tangu miaka ya themanini, idadi ya silaha hizo duniani imekuwa ikipungua.

Kulingana na Kituo cha Kimataifa cha Amani na Utafiti cha Stockholm (SIPRI), mataifa tisa duniani yanayoongoza kwa umiliki wa silaha hizo yalikuwa na jumla ya silaha 12,705 kufikia mwanzoni mwa mwaka huu.

Hilo ni ikilinganishwa na mwishoni mwa 2021, ambapo mataifa hayo yalikuwa na jumla ya silaha 13,080.

Nchi hizo ni Uingereza, China, Ufaransa, India, Israeli, Korea Kaskazini, Pakistan, Amerika na Urusi.

Idadi ya silaha hizo imepungua kutoka karibu 70,000 mnamo 1986, kutokana na hatua ya baadhi ya nchi kama Amerika na Urusi kupunguza akiba yao ya silaha hizo. Mataifa hayo mawili yaliongeza akiba ya silaha hizo wakati wa Vita Baridi vya Dunia, vilivyodumu kati ya 1947 na 1990.

Hata hivyo, watafiti wanasema mataifa mengi yameanza kuongeza akiba zao, hasa baada ya janga la virusi vya corona.

“Katika siku za hivi karibuni, tutafikia mahali ambapo kwa mara ya kwanza baada ya Vita Baridi vya Dunia, idadi ya silaha za nyuklia duniani itaanza kuongezeka,” akasema Matt Korda, ambaye ni mmoja wa walioandika ripoti hiyo, kwenye mahojiano na wanahabari.

“Huu ni mwelekeo hatari kwa mustakabali wa kiusalama duniani,” akaeleza.

“Baada ya idadi ya silaha hizo kupungua kwa kiwango kidogo mwaka uliopita, akiba ya silaha hizo inatarajiwa kuongezeka sana mwongo mmoja ujao,” ikasema SIPRI.

SILAHA HATARI

Kwenye vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine, Rais Vladimir Putin wa Urusi amekuwa akirejelea uwezekano wa taifa hilo kutumia silaha za nuklia.

Ripoti ilieleza kuna uwezekano mataifa kama China na Uingereza yanaongeza au kuboresha akiba zao za silaha hizo.

“Itakuwa vigumu sana kupata mafanikio kuzirai nchi nyingi kupunguza utengenezaji wa silaha hizo katika miaka ijayo kutokana na vita hivi na na kauli anazotoa Putin kuhusu matumizi yake,” akasema Korda.

“Kauli hizo zinayafanya mataifa mengine kubuni na kutathmini njia za kuongeza akiba ya silaha zake,” akaongeza.

Kulingana na kituo hicho, mataifa mengi yamekuwa yakitengeneza silaha hizo licha ya kupitishwa kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu udhibiti wa utengeneaji wake mwaka uliopita. Mkataba huo ulipiga marufuku nchi kuhusu utengenezaji wa silaha za nuklia.

Wataalamu wanasema kuwa kando na vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine, mpango wa Iran kuhusu utengenezaji wa silaha hizo pia umeibua wasiwasi duniani.

Walisema kuwa sababu kuu ya kupungua kwa silaha hizo kwa sasa ni hatua ya Amerika na Urusi “kuharibu silaha zake za zamani.”

Kwa sasa, Urusi na Amerika zinamiliki asilimia 90 ya silaha hizo duniani.

Hata hivyo, Urusi ndiyo inaongoza kwa kuwa na jumla ya silaha 5,977 kufikia mwaka huu 2022.

  • Tags

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Inatia moyo kuona wanawake wakiwa katika...

SHINA LA UHAI: Glakoma yapofusha Wakenya kimya kimya

T L