• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Watu 632 wafariki kwenye tetemeko kubwa la ardhi nchini Morocco

Watu 632 wafariki kwenye tetemeko kubwa la ardhi nchini Morocco

NA MASHIRIKA

RABAT, MOROCCO

IDADI ya walioangamia nchini Morocco kufuatia tetemeko la ardhi imefika watu 632, mkuu wa ufuatiliaji wa zilizala nchini humo Hani Lahsan akisema matetemeko mengine madogo yanaendelea kushuhudiwa.

Ameiambia Al Jazeera akiwa jijini Rabat kwamba matetemeko mengine yataendelea kushuhudiwa baada ya lile la kwanza.

“Matetemeko hayo hata hivyo yatakuwa ya kiwango cha chini kuliko lile kubwa ambalo limeshuhudiwa na kadri muda unavyosonga ndivyo hali itatulia na kuwa ya kawaida,” amesema Lahsan.

Ripoti ya Jiolojia kutoka Amerika imesema tetemeko la kipimo cha 6.8 kwenye vipimo vya Ritcher lilitokea katika eneo la milima lililo umbali wa 72 kilomita kusini mwa mji wa Marrakesh, ambao ni kivutio cha watalii, saa tano na dakika 11 Ijumaa usiku.

Nyumba kadha ziliharibiwa katika mji huo wa tatu kwa ukubwa nchini Morocco huku wakazi wakitorokea barabarani katika harakati za kujinusuru.

Runinga ya kitaifa ya nchini humo imeripoti kwamba miongoni mwa waliojeruhiwa, 51 kati yao walipata majeraha mabaya zaidi.

Aidha, runinga hiyo imepeperusha picha ya Msikiti ulioporomoka huku vifusi vya jengo hilo vikifunika magari yaliyoharibiwa.

Wakazi wa mji huo wa Marrakesh, wamesema baadhi ya majengo yaliporomoka katika mji huo wa kale uliotangazwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kuwa kituo cha turathi duniani.

Matetemeko mengine yametokea katika miji ya mwambao wa pwani ya Rabat, Casablanca na Essaouira.

Viongozi wa mataifa mbalimbali wanatuma risala zao baada ya kutokea kwa janga hilo.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amefariji Morocco kwa janga hilo.

“Hizi ni habari za kuhuzunisha kutoka Morocco. Kwa wakati huu, tunafariji wote walioathirika na tetemeko hilo,” akaandika Scholz kwenye mtandao wa kijamii wa X, ambao awali ulifahamika kama Twitter.

Akichapisha hayo, idadi ya walioangamia ilikuwa 296 lakini baadaye ikapanda mara moja. Scholz yuko njini India kwa Kongamano Kuu la mataifa makubwa duniani yanayofahamika kama G20.

Wengine waliotuma risala zao ni Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez aliyesema nchi yake iko tayari kuisaidia Morocco na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliyesema nchi yake itatoa huduma ya kwanza wakati wa janga hilo.

  • Tags

You can share this post!

Wanaume 3 wanaswa Bungoma kwa kuitisha hongo kwa vijana...

Uchaguzi wa viongozi wa UDA kufanyika Desemba 2023 –...

T L