• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Watu wenye bunduki waua binti, dereva wa Jenerali Katumba Wamala

Watu wenye bunduki waua binti, dereva wa Jenerali Katumba Wamala

Na MASHIRIKA

KAMPALA, Uganda

WATU wenye bunduki Jumanne wameshambulia kwa risasi gari la serikali ya Uganda lililokuwa limembeba waziri mmoja katika kile kilichosemekana kuwa jaribio la kutaka kumuua.

Jenerali Katumba Wamala ambaye ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi alijeruhiwa katika shambulio hilo lakini bintiye na dereva wake wakauawa, kulingana na msemaji wa jeshi na ripoti za vyombo vya habari.

Washambuliaji hao ambao walikuwa wakisafiri kwa pikipiki walishambulia gari hili katika mtaa wa Kiasasi, viungani kwa jiji la Kampala, kulingana na shirika la televisheni la NBS.

Picha zilizokuwa zikisambaa katika mitandao ya kijamii zilionyesha akiwa amepanua mdomo wake ishara ya maumivu na mshtuko, akiwa kando ya gari hilo na long’i yake ikiwa imeloa damu. Gari hilo pia lilionekana na mashimo ya risasi ubavuni na kwenye vioo vya madirisha.

“Alihusika katika ufyatulianaji wa risasi. Amejeruhiwa na anapelekwa hospitalini. Dereva wake aliuawa katika tukio hilo,” msemaji wa jeshi Brigedia Flavia Byekwaso akawaambia wanahabari.

Nayo runinga ya NBS ikaripoti.

“Wamala alipata majeraha mengine mabegani lakini binti yake ambaye walikuwa naye ndani ya gari hilo ameuawa,” kulingana na ripoti ya runinga ya NBS.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumetokea visa kadha vya watu mashuhuri kuuawa kiajabu nchini Uganda. Hata hivyo, malengo ya wanaotekeleza mauaji hayo hayajabainika.

Miongoni mwa waliouwa kwa njia tata jinsi hiyo ni mbunge, afisa wa polisi wa cheo cha juu, mwendeshaji mashtaka mkuu nchini Uganda, viongozi wakuu wa dini ya Kiislamu na wengine.

Karibu mauaji hayo yote yalitekelezwa na wahalifu waliokuwa wakisafiri kwa pikipiki.

Eneo ambako jaribio la kumuua Wamala lilitekelezwa ndiko afisa mmoja wa polisi wa cheo cha juu aliuawa mnamo 2017 na watu wenye bunduki na waliokuwa wakisafiri kwa pikipiki.

Felix Kaweesa aliuawa pamoja na mlinzi wake na dereva.

Waziri Wamala, ambaye zamani alikuwa kamanda jeshini, anatoka kabila kubwa nchini Uganda, Baganda.

Muda mfupi kabla ya kushambuliwa kwake, Wamala waliwaambia marafiki zake katika twitter kwamba: “Nawatakia mwezi wa Amani, Furaha, Mafanikio, Afya Bora, na Mali.”

Tafsiri: CHARLES WASONGA

You can share this post!

Nyong’o aeleza jinsi huduma za afya zilivyoimarika...

Covid-19: Raila atoa wito serikali izindue miradi mingi...