• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
WHO yazuiwa kuingia China kuchunguza kiini cha Covid-19

WHO yazuiwa kuingia China kuchunguza kiini cha Covid-19

Na MASHIRIKA

BEIJING, CHINA

CHINA imewanyima kibali wataalamu 10 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuchunguza chanzo cha virusi vya corona nchini humo.

Hii ni licha ya majadiliano ya miezi kadhaa kati ya shirika hilo na serikali ya China ambapo pande zote zilikubaliana kuhusu ziara hiyo.

Wataalamu hao walifaa kuwasili China wiki hii ili kubaini jinsi ambavyo virusi hivyo hatari vilitoka kwa wanyama na kuambukiza binadamu kabla ya kuenea kote ulimwenguni.

Tayari wataalamu hao walikuwa wameanza safari yao ila China ikawanyima viza, hatua iliyomgadhabisha mno Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Hatua hiyo inadhihirisha kwamba China ina nia ya kuzuia utafiti wowote nchini humo kuhusu asili ya virusi vya corona. Virusi hivyo tayari vimesababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 1.8 kote duniani.

Kisa cha kwanza cha virusi vya corona kiliripotiwa jijini Wuhan mwisho wa 2019 na inashukiwa kuwa China ilihusika na kuunda virusi hivyo hatari hasa wakati huu mataifa makubwa yenye uchumi mkubwa yana ubabe kuhusu ushawishi wao ulimwenguni.

Mbali na kukataa kuruhusu uchunguzi wa ndani kuhusu virusi hivyo, China imekuwa ikitilia shaka iwapo kwa kweli virusi vya corona vilianzia nchini humo.

Msemaji wa Wizara ya Masuala ya Nje Hua Chunying alithibitisha kuwa wataalamu kutoka WHO walizuiwa, akikiri kuwa haikuwa inahusiana na suala la visa.

Hua alisema wataendelea kushauriana na WHO ili wataalamu hao waruhusiwe waingie nchini humo siku nyingine.

“Suala la kusaka chimbuko la virusi vya corona ni tata sana,” akawaeleza wanahabari.

“Kuhakikisha kwamba kazi ya wataalamu wa kimataifa nchini China inaendelea vizuri, lazima tukumbatie baadhi ya mikakati na maandalizi mazuri. Mazungumzo yanaendelea kuhusu tarehe mpya na maandalizi mengine kabla ya ziara ya wataalamu wa WHO,” akasema Chunying. Ziara ya wataalamu wa WHO ilikuwa imetazamwa kama itakayotoa mwanga zaidi kuhusu jinsi ambavyo virusi hivyo vilichipuka.

“Sote tulikuwa na matumaini kwamba wataalamu wetu wangeanza kazi mara moja,” akasema Michael Ryan ambaye ni Mkuu wa kitengo cha Majanga WHO.

Wanasayansi wanaamini kwamba virusi hivyo vilifikia wanadamu na huenda vilianzia jijini Wuhan kwenye soko moja ambalo huuza nyama. Hata hivyo, wataalamu wanashikilia wazo kwamba huenda corona haikuanzia sokoni bali ililipukia huko baada ya kuchipukia eneo jingine.

Wakati wa mlipuko wa virusi vya corona, China ilikuwa kwenye mzozo mkubwa na Rais wa Marekani Donald Trump ambaye alitumia suala hilo kujitenga kisiasa.

You can share this post!

Waboni walilia serikali watoto wapate elimu

Ruto ataka Raila abebe ‘dhambi’ kadhaa za...