• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Zelensky awafuta kazi maafisa akidai usaliti

Zelensky awafuta kazi maafisa akidai usaliti

NA MASHIRIKA

KYIV, UKRAINE

RAIS Volodymyr Zelensky wa Ukraine amesimamisha kazi mkuu wa Idara Kuu ya Ujasusi (SBU) na Kiongozi Mkuu wa Mashtaka wa Serikali kwa tuhuma za kushirikiana kisiri na Urusi.

Kiongozi huyo alisema zaidi ya watu 60 wanaohudumu katika idara hizo mbili wanashirikiana na Urusi kwenye uvamizi wake dhidi ya Ukraine.

Alisema wafanyikazi hao wanavisaidia vikosi vya Urusi kutambua maeneo vitakayoshambulia.

Aliongeza kuwa kufikia sasa, jumla ya kesi 651 za usaliti na uhaini zimefunguliwa dhidi ya maafisa wa serikali na vikosi vya usalama vya Ukraine.

Hata hivyo, maafisa hao wawili, Ivan Bakanov na Iryna Venediktova, hawajatoa taarifa yoyote.

“Makosa kama hayo yanakiuka misingi na mwongozo wa utendakazi wa idara zetu za usalama wa kitaifa. Ni makosa yanayoibua pakubwa uwajibikaji wa maafisa hao wawili na taasisi walizokuwa wakiziongoza,” akasema Zelensky

Lakini baadaye, Andry Smirnov, aliye mojawapo ya washauri wakuu wa Zelensky, alieleza kuwa maafisa hao wawili hawakuwa wamefutwa kazi, kama ilivyokuwa imeelezwa awali.

Alisema waliondolewa kwenye nafasi zao kwa muda ili kufanyiwa uchunguzi.

Kuondolewa kwa akanov kama mkuu wa SBU kunafuatia kukamatwa kwa afisa mwingine wa zamani wa ngazi ya juu katika idara hiyo, Oleh Kulinych.

Kulinych alihudumu kama mkuu wa SBU katika eneo la Crimea mnamo 2014. Bakanov ni rafikiye wa utotoni wa Rais Zelensky.

“Kila mmoja aliyeshirikiana naye kutoa siri zetu kwa Urusi atakamatwa. Ni makosa kutoa siri kwa maadui wetu kwani ndizo zinazotumiwa kutushambulia,” akasema Zelensky.

Maafisa wa ngazi za juu wa ujasusi wanaohudumu katika eneo la Kherson pia wamefunguliwa mashtaka. Zelensky alisema maafisa zaidi wa idara hiyo watachukuliwa hatua.

Tangu uvamizi huo kuanza mnamo Februari, kumekuwa na hofu Urusi imekuwa ikipata siri kuhusu mipango na mikakati ya kiusalama ya vikosi vya Ukraine.

Hata hivyo, wadadisi wanasema kuwa si ajabu kwa Urusi kupata maelezo ya siri ya shughuli za vikosi vya Ukraine.

Idara ya Ujasusi ya Urusi (FSB) ina historia ya kuingilia idara za kijasusi za mataifa tofauti.

Wanaeleza kuwa kile kinashangaza ni jinsi Urusi ilivyofanikiwa kuingilia idara za ujasusi za Ukraine na kufaulu bila kugunduliwa.

Inaelezwa kuwa moja ya sababu zilizofanya vikosi vya Urusi kuuteka mji muhimu wa Kherson kwa urahisi ni maelezo ya kijasusi vilivyopata kutoka kwa baadhi ya maafisa wa Ukraine.

Wadadisi wa masuala ya usalama wameeleza kushangazwa kwao na idadi kubwa ya maafisa wa usalama ambao wamekuwa wakitoa maelezo ya kijasusi kwa Urusi.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Wafadhili wa kampeni za Ruto na Raila...

SHINA LA UHAI: Tiba ya ‘ketnyo’ yanusuru wengi Pokot...

T L