• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
CHARLES WASONGA: Wafadhili wa kampeni za Ruto na Raila chanzo cha ufisadi

CHARLES WASONGA: Wafadhili wa kampeni za Ruto na Raila chanzo cha ufisadi

NA CHARLES WASONGA

INAVUNJA moyo kwamba wagombea urais William Ruto na Raila Odinga hawataweza kupambana na jinamizi la ufisadi endapo mmoja wao atashinda urais katika uchaguzi mkuu ujao ilhali uovu huu ni adui mkubwa wa maendeleo nchini.

Ni jambo la kusikitisha kuwa Wakenya wataelekea debeni Agosti 9, kuchagua rais ambaye atakuwa mateka wa ‘magenge’ ya wafisadi kwa miaka mitano na hivyo kufeli kutimiza ahadi nzuri ambazo alitoa wakati wa kampeni

Hii ni kwa sababu wawili hawa, ambao ndio wanaoongoza kwa umaarufu, kulingana na matokeo ya kura kadhaa za maoni, wamezingirwa na wanasiasa ambao maadili yao ni ya kutiliwa shaka.

Kwa kiwango kikubwa, kampeni za Dkt Ruto na Bw Odinga zinafadhiliwa na wafanyabiashara ambao ni wakwepaji wakuu wa ushuru na laghai ambao lengo lao ni kupewa zabuni serikalini kwa njia ya mkato isiyozingatia sheria.

Jambo hilo lilidhihirika mwishoni mwa wiki jana pale Dkt Ruto alipopokezwa gari la kifahari alitumie katika kampeni zake za kusaka kura za urais.

Gari hilo, ambalo limerembeshwa kwa rangi ya manjano na picha za Dkt Ruto na mwaniaji-mwenza wake Rigathi Gachagua, lilizinduliwa katika hafla fupi iliyofanyika katika makazi rasmi ya Naibu Rais mtaani Karen, Nairobi.

Dkt Ruto alimshukuru mfadhili, ambaye jina lake lilibanwa, kwa kumtunuku gari hilo ambalo linakadiriwa kugharimu karibu Sh80 milioni.

Hii ni mbali na misaada mingine mingi ambayo Naibu Rais amekuwa akipokea kutoka kwa wahisani na wafadhili.

Bw Odinga naye alipigwa jeki na mabwanyenye mbalimbali, chini ya mwavuli wa Wakfu wa Mlima Kenya (MKF), waliomchangia mamilioni ya pesa kugharimia kampeni zake huku zikizalia siku chache kabla ya Wakenya kupiga kura.

Mchango huo uliendeshwa kwa njia ya hafla ya chajio (dinner party) ambapo sahani moja ya chakula iligharimu angaa shilingi milioni moja (Sh1 milioni).

Kuna baadhi ya watu waliolipa Sh10 milioni kwa kiasi hicho cha chakula katika dhifa hiyo iliyoandaliwa katika mkahawa wa kifahari wa Safari Park, Nairobi.

Miongoni mwa wanachama wa wakfu wa MKF waliohudhuria shughuli hiyo ni mwenyekiti wake Peter Munga na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ushuru (KRA) John Njiraini.

Wakuu wa kampuni na mashirika mbalimbali ya kibinafsi, na umma, pia walihudhuria hafla hiyo inayotoa kumbukumbuku ya ile iliyofanyika 2017 kupiga jeki kampeni za Rais Uhuru Kenyatta akipania kuhifadhi kiti chake.

Kinaya ni kwamba waliohutubu katika hafla hiyo walimhimiza Bw Odinga na mwaniaji-mwenza wake Bi Martha Karua, wapambane na ufisadi bila woga endapo watashinda urais na kuunda serikali.

Sidhani Bw Odinga ataweza kufanya hivyo kwa sababu mabwanyenye wawa hawa ndio watakaomweka mateka wakipania kurejesha fedha ambazo walitumia kufadhili kampeni za urais za Azimio la Umoja- One Kenya.

Ni jambo la kawaida nchini wafanyabiashara wanaomiliki kampuni na mashirika makubwa huwapiga jeki kifedha wagombea wakuu wa urais kwa matumaini ya kufaidi serikali inapobuniwa.

Uchunguzi umeonyesha kuwa njia mojawapo ambayo wao huvuna ni kupitia zabuni za serikali za kima cha mabalioni ya fedha. Bila shaka wao hutunikiwa zabuni hizi kwa njia ambazo hazizingatii sheria zinapasa kuzingatiwa wakati wa utoaji zabuni za umma.

Hivi ndivyo, ufisadi hunawiri ambapo mabilioni ya pesa za umma huporwa. Kwa hivyo, Dkt Ruto na Bw Odinga wakome kuwahadaa Wakenya kwamba watapambana na zimwi la ufisadi.

  • Tags

You can share this post!

Makarios yazidi kufanya kweli Daraja la Pili

Zelensky awafuta kazi maafisa akidai usaliti

T L