• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
ZARAA: Siri ni kukuza pilipili mboga za rangi tofauti kuvutia wateja

ZARAA: Siri ni kukuza pilipili mboga za rangi tofauti kuvutia wateja

Na SAMMY WAWERU

JUNI 2021, Peter Kang’acha alizuru makao makuu ya maduka ya Zucchini na ambayo ni tajika katika uuzaji wa mboga aina mbalimbali, viungo vya mapishi na matunda, kutafiti.

Shabaha yake, ilikuwa kubaini mboga, pilipili mboga na nyanya zinavyonunuliwa.

Yakiwa eneo la Ngong Road, kiungani mwa jiji la Nairobi, Kang’acha anasema aliridhishwa zaidi na soko la pilipili mboga za rangi tofauti.

Isitoshe, zao hilo lilivyonunuliwa mithili ya mahamri moto sokoni lilimtia motisha kuwa miongoni mwa wazalishaji.

“Bei ilikuwa bora, ile ya kuacha mkulima akitasabamu,” Kang’acha asema.

Anaelezea kwamba mpangilio wa duka hilo, ulikuwa hoho tatu za rangi nyekundu, manjano na kijani Sh200.

“Nikikadiria, zilikuwa na uzito wa kati ya gramu 400 – 500, na baada ya kukokotoa hesabu nikagundua kilo moja si ajabu ikiingiza Sh400,” anafafanua.

Hatimaye, alirejea kwake akiwa na jawabu: “Sina tashwishi kilimo cha pilipili mboga ndicho chaguo langu la kwanza.”

Chini ya kipindi cha mwezi mmoja, aligeuza robo ya shamba lake lenye ukubwa wa ekari moja na robo tatu, Miti-Ini, Kennol, Kaunti ya Murang’a, kuwa uga wa kilimo.

Alitengeneza kivungulio chenye kipimo cha mita 16 kwa 30, kilichokumbatia mfumo wa kisasa kunyunyizia mimea na mashamba maji kwa kutumia mifereji.

Anafichua, kilimgharimu Sh500,000 alizokuwa ameweka kama akiba.

“Kwanza nilitangulia na vipimo vya udongo, kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Mimea na Uimarishaji Mifugo (Kalro),” afafanua, akisema alitozwa Sh200 pekee kukagua sampuli ya udongo wa shamba lake.

Kabla kuingilia shughuli za kilimo, wakulima wanahimizwa kufanya vipimo vya udongo ili kujua kiwango cha pH (asidi na alkali).

“Vipimo vya pH humuwezesha mkulima kujua kiwango cha virutubisho vilivyopo na vinavyohitajika kuongezwa,” aelezea Edwin Njiru mtaalamu wa masuala ya kilimo.

Kufikia mwishoni mwa mwezi Julai, Kang’acha alikuwa amefanya upanzi wa pilipili mboga za rangi nyekundu na manjano, na nyanya.

Mkulima huyu anasema ilikuwa jaribio, jaribio ambalo limemtia tabasamu na kuapa kamwe hataasi kilimo cha hoho.

Rekodi ya mauzo inaashiria zina mapato ya kuridhisha. Huku akiwa alianza kuvuna pilipili mboga Oktoba, anasema kila baada ya siku mbili hufanya mavuno ya kreti tatu, kila moja ikiwa na uzani wa kilo 15.

“Wateja wangu ni wakazi wa Kennol, kilo moja ni Sh100,” adokeza, akisema nyanya alianza kuvuna mwezi Septemba.

“Gharama ya mbegu, fatalaiza na dawa dhidi ya wadudu niliyotumia tayari imerejea.”

Kang’acha, 42, anaiambia Akilimali ni kutokana na mapato ya kuridhisha kupitia zao la hoho za rangi nyekundu na manjano, anajipa muda wa miaka mitatu pekee awe amevalia sare kamilifu za kilimo.

Kwa sasa anaendeleza zaraa kama shughuli ya ziada na kwa sasa ameajiriwa na kampuni moja jijini.

“Pilipili mboga ni zao la thamani, ambalo nimegundua wateja hupenda zile za rangi kufanya chakula kuwa maridadi,” asema mkulima huyu mwenye Shahada ya Uzamili katika Masuala ya Uchumi.

Anasema changamoto kuu, ni ugonjwa wa barafu (powdery mildew) na mdudu aina ya leaf miner na Tuta absoluta.

Hata hivyo, anakiri kwa kukumbatia kilimo cha mvungulio, kero ya wadudu na magonjwa hudhibitiwa kwa kiwango kikubwa.

Kang’acha pia hulima mboga aina ya sukumawiki na spinachi.

Peter Kang’acha vilevile hukuza sukumawiki na spinachi. PICHA | SAMMY WAWERU

Yeye pia ni mfugaji wa kuku wa kienyeji ambapo kwa sasa ana kuku 67 na vifaranga 120 na ng’ombe wa maziwa, ufugaji unaomsaidia kupata mbolea kuboresha mazao.

Chanzo cha maji kwake si hoja, kwani ana kisima chenye kina cha urefu wa futi 40, anachosifia hakiishi maji.

You can share this post!

‘Omicron’ imefika lakini hatufungi nchi –...

NJENJE: Matumizi ya pesa kwa njia ya simu yaongezeka

T L