• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri kilimo cha plamu nchini

Mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri kilimo cha plamu nchini

Na SAMMY WAWERU

NDUGU wawili, Wairimu Mungai na Simon Mungai, wana jumla ya ekari 15 katika kijiji cha Miiri, Milangine, Kaunti ya Nyandarua.

Unapozuru shamba lao utakaribishwa na mpangilio wa dari ya miti. Wana aina tofauti y miti kuanzia Cypress, Blue gum na pia miplamu au plums kama inavyofahamika zaidi na mipea.

Wawili hao walitwaa shughuli za kilimo kutoka kwa wazazi wao miaka ya themanini.

Kulingana nao, kiwango cha mazao ya plamu miaka hiyo kilikuwa cha kuridhisha.

“Tuliporithi, kila mti ulikuwa ukizalisha wastani wa kilo 70,” Simon asema, akifichua walichukua hatamu mwaka wa 1985.

Wazazi wao walikuwa wametenga ekari moja iliyositiri miti 100 ya plamu .

Plamu ni matunda ya msimu mmoja kwa mwaka hulimwa kwa wingi maeneo ya Nyandarua, Limuru – Kiambu na pia Nyeri.

“Yanastawi sehemu zenye baridi,” Wairimu adokeza, akiongeza kuwa huwa yanahitaji maji mengi kunawiri.

Matunda haya matamu hufanya vyema katika udongo usiotuamisha maji na wenye asidi na alkali (pH) kati ya 5.5 – 6.5.

Aidha, anaeleza kwamba miaka ya themani, kilo moja ilikuwa ikinunuliwa kwa Sh3. “Mazao yalikuwa kwa wingi kwa sababu ya hali bora ya anga,” asema.

Kwa mwaka, wakulima hao wenye tajiriba ya muda mrefu kukuza plamu, wanasema walikuwa wakishuhudia kiangazi mwezi wa Februari na Machi pekee.

“Miezi mingine yote mvua ilikuwa tele na kuchangia mazao kuwa tele,” Simon aelezea.

Hata hivyo, hali si hali tena, kwa kile wanazaraa hao wanataja kama mabadiliko ya tabianchi kuathiri kwa kiasi kikubwa kilimo cha plamu.

Mambo yalianza kuenda kombo mwaka wa 1997, baada ya Kenya kushuhudia mvua kubwa ya mafuriko.

Kutoka uzalishaji wa kilo 70 katika kila mti, Wairimu asema sasa mti hauzidishi kilo 35 kwa mwaka.

Hii ina maana kuwa mazao yamepungua kwa asilimia 50. “Si ajabu mti kuzaa jumla ya kilo 5,” Simon asema, akilalamikia athari za mabadiliko ya tabianchi.

Anasema eneo la Milangine hupokea mvua kati ya Juni na Oktoba, miezi muhimu katika kunawirisha plamu.

Aghalabu, mavuno huwa mwezi wa Desemba na Januari.

Ni athari ambazo zimechochea wakulima hao kupunguza kiwango cha shamba linalokuzwa matunda hayo.

“Kwa sasa tunalima kwenye nusu ekari miti 40 ya plamu kutoka ekari moja,” akasema Wairimu wakati wa mahojiano.

Hali hiyo pia imewafanya kupunguza idadi ya wafanyakazi.

“Awali, hasa msimu wa kupogoa matawi na mavuno tulikuwa tunaajiri kati ya vibarua 7 – 10, kwa sasa ni mmoja,” akafafanua mkulima huyo.

Simon anaeleza kuwa kilimo cha plamu si kigumu kwani kwa mwaka matunzo ya mti mmoja hugharimu Sh500.

“Kilo moja ya plamu bei ya shambani ni Sh50,” Simon asema akilalamikia hasara wanayokadiria.

 

Mkulima Wairimu Mungai akichuma plamu shambani mwake eneo la Milangine, Kaunti ya Nyandarua. PICHA | SAMMY WAWERU

Wateja wao ni wale wa rejareja, kinyume na miaka ya zamani ambapo walitegemea wa jumla.

“Soko ni changamoto kuu, mbali na athari za mabadiliko ya tabianchi,” aelezea.

Waomba serikali isaidie katika uongezeaji thamani

Si kisa kimoja viwili au vitatu, mazao ya wakulima hao mandugu yameozea shambani kwa sababu ya kukosa wanunuzi.

“Tunaiomba serikali izindue kiwanda cha kuongeza plamu thamani, kama vile cha kuunda jemu ili mahangaiko ya soko yaishe tupate motisha kama wakulima wa macadamia,” Wairimu ahimiza.

Plamu haijapata mianya ya soko la nje ya nchi.

Kando na ratiba ya hali ya anga kubadilika, mabadiliko ya tabianchi yamechangia mkurupuko wa wadudu waharibifu na pia magonjwa ambayo Simon anasema yanasababisha matunda ya plamu kuwa na madoadoa meusi.

Ili kukabiliana na upungufu wa maji, Simon na Wairimu wana visima na bwawa, vyanzo vya maji vinavyowasaidia kufanikisha shughuli za kilimo.

Mabadiliko ya tabianchi yamegeuka kuwa kero Bara Afrika, baadhi ya kaunti nchini zikilemewa na baa la ukame na njaa.

  • Tags

You can share this post!

Simanzi yagubika Lamu waliouawa na wahalifu wakizikwa

TUJIFUNZE UKULIMA: Wakulima wahamasishwe jinsi ya kukabili...

T L