• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 4:34 PM
Utaoshwa! Hisia mseto, wasiwasi kufuatia kuzinduliwa kwa apu inayobatilisha jumbe za Mpesa

Utaoshwa! Hisia mseto, wasiwasi kufuatia kuzinduliwa kwa apu inayobatilisha jumbe za Mpesa

NA MARY WANGARI

UTAHITAJIKA kuwa makini zaidi iwapo wewe ni mfanyabiashara anayetumia mbinu za kielektroniki kupokea malipo kutoka kwa wateja.

Hii ni kufuatia kuzuka kwa Apu mpya inayofahamika kama Fake Text (Ujumbe Ghushi) ambayo huenda ikawasababishia hasara tele wauzaji bidhaa na watoaji huduma mbalimbali.

Apu hiyo inayoweza kuopolewa kirahisi bila malipo yoyote kupitia mtandao wa Apps on Google Play inamwezesha mtumiaji kubadilisha ujumbe wote na kuugeuza jinsi apendavyo.

Isitoshe, kando na kumwezesha mtumiaji kuongeza vigezo vya ziada kwenye ujumbe husika, apu ya Fake Text inaruhusu kubadilisha jina la aliyetuma na pia wakati ujumbe huo ulipotumwa.

Tovuti ya shirika la wataalamu wa teknolojia almaarufu kama Softonic linafafanua apu ya Fake Text Message kama “jinsi jina linavyoashiria ni apu inayohusu mtindo wa maisha inayotolewa bila malipo na inayokuwezesha kujitumia na kupokea ujumbe ghushi.”

“Ni mbinu kabambe ya kukusaidia kujitoa kwenye hali tatanishi maadamu unaweza ukabadilisha ujumbe na kuandika kitu kinachoonekana kana kwamba kinahitaji kushughulikiwa kwa dharura.”

“Unaweza pia kubadilisha jina la aliyetuma ili kuufanya ujumbe kuwa wa kuaminika zaidi. Fake Text Messages pia inahifadhi jumbe zote ghushi ulizotuma au kutumiwa kwenye kitengo chake cha Historia ya Jumbe. Utaona majina ya wote waliotuma na jumbe zote uliowatumia.”

Apu hiyo tatanishi imeonekana kuwachangamsha baadhi ya Wakenya kwenye mitandao ya kijamii huku wafanyabiashara na watoaji huduma wanaotumia mfumo wa malipo kidijitali wakitahadharishwa kuwa makini la sivyo wakumbane na hasara kubwa.

Kupitia video iliyosambazwa mno mitandaoni, kundi la vijana lilijirekodi kwenye mtandao wa Tiktok wakishangilia baada ya kufanikiwa kubadilisha ujumbe wa malipo kupitia Mpesa.

Vijana hao walimtapeli mfanyabishara mamilioni, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Shirika linalojihusisha na Masuala ya Data Afrika Mashariki, George Njoroge.

“Katika sakata mpya, vijana wenye ujuzi kiteknolojia wanaunda nambari feki za malipo ili kuwahadaa wauzaji rejareja. Tapeli huyu mjanja amesababisha wizi wa bidhaa zenye thamani ya mamilioni,” alionya Bw Njoroge kupitia mtandao wa kijamii wa X.

“Kuna ujanja wa kubadilisha jumbe za Mpesa unaogharimu biashara nyingi. Kwa kutumia apu wanaunda ujumbe ghushi wa Mpesa unaojitokeza kwenye simu ya mhusika. Kwa biashara, sisitiza kuwasilisha bidhaa baada ya kuona jumbe upande wako ama utaoshwa!” anaeleza Mhariri Mkuu na Mwasisi wa Kenya Insights, Kenya West.

Apu hii ni pigo kuu kwa wafanyabiashara hasa wakati huu gharama ya maisha inazidi kupanda na kusababisha biashara kuyumba huku nyingi zikiishia kufungwa.

“Nimeona video ya utapeli wa Mpesa na nimeshtushwa na jumbe. Tunawezaje kusherehekea uhalifu kama huo? Biashara tayari zinakabiliwa na nyakati ngumu na sasa tunawaongezea masaibu kwa kugeukia wizi?” Anahoji mfanyabiashara kwa jina Farhiya Abass.

  • Tags

You can share this post!

Ufisadi katika kaunti unapitiliza maelezo, ripoti ya EACC...

Jinsi makateli wanavyofufua biashara ya mifuko za plastiki...

T L