• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Wakulima wahimizwa kukumbatia mifumo bora kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi

Wakulima wahimizwa kukumbatia mifumo bora kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi

Na SAMMY WAWERU

WAKULIMA wametakiwa kukumbatia mifumo ya teknolojia ya kisasa katika shughuli za kilimo ili kupunguza na kukwepa athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Ni mabadiliko ya hali ya anga ambayo yamechangia misimu ya upanzi kuathirika, kufuatia ratiba ya mvua kusambaratika, kero ya ukame, wadudu na magonjwa.

Zaidi ya kaunti 24 nchini zimekodolewa macho na hatari ya baa la ukame, wakazi wakikadiria hasara ya mimea kukauka na mifugo kufariki kwa sababu ya ukosefu wa mvua.

Kutokana na athari hizo, InsuResilience Solutions Fund (ISF) imehimiza wakulima kukumbatia mifumo ya kisasa kama vile Bayoteknolojia kuendeleza zaraa.

Bayoteknolojia inajumumuisha bunifu za Kisayansi, ikiwemo kuongeza jeni, kuboresha mimea na mifugo ili kupata spishi zilizoimarika (GMO) kusaidia kupambana na kero ya wadudu, vimelea na magonjwa.

Mfumo huo pia unasaidia kuafikia usalama wa mazao kwa kupunguza matumizi ya kemikali.

Kando na manufaa hayo, vilevile unapunguza gharama katika uzalishaji wa mazao na chakula.

“Wakulima wageukie mifumo ya kisasa kukuza na kuzalisha chakula, ili kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi,” akashauri Bw Jonathan Nkoola, afisa kutoka ISF akizungumza jijini Nairobi.

ISF inashirikiana na Shirika la Kilimo na Kuangazia Mabadiliko ya Tabianchi Afrika (ACRE), ambalo hutoa huduma za bima kwa wakulima Barani Afrika, Kenya ikiwemo.

Aidha, hutoa ufadhili kifedha.

“Tumeweza kufikia zaidi ya mataifa 20 ulimwenguni, kutoa ufadhili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” Nkoola akadokeza.

“Zaidi ya nchi 200 zimetuma maombi kunufaika kupitia ufadhili tunaotoa,” akaongeza afisa huyo.

Afrika, Kenya, Uganda, Rwanda na Togo, zinaendelea kuridhia kupitia mpango wa ISF.

Alilalamikia mkurupuko wa janga la Covid-19 kuathiri mipango ya shirika hilo, katika kupiga jeki jitihada za wakulima duniani.

“Furaha yetu ni kuona wakulima wameinuka, na changamoto zinazowakumba zimepungua na hata kuisha,” akaelezea.

Alisisitiza kwamba shabaha ya ISF ni kuona maisha ya wakulima, hasa wale wa mashamba madogo yameboreka.

“Mazao yakiongezeka na yawe salama, maisha yao yataimarika.”

Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kuwa kero nchini.

Ni hali inayotajwa kuchangiwa na ukataji wa miti na uharibifu wa misitu, hivyo basi kuathiri vyanzo vya maji na mvua.

Mapema 2018, Kenya ilipiga marufuku ukataji wa miti katika misitu ya umma.

Wizara ya Mazingira na idara za misitu, inaendeleza kampeni ya upanzi wa miti nchini.

Machi 2019, Rais Uhuru Kenyatta aliahidi kwamba serikali inafanya kila iwezalo kuafikia kigezo cha asilimia 10 ya misitu Kenya kufikia mwaka huu, 2022.

Kongamano la Kimataifa Kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) lilifanyika Glasgow, Scotland, Novemba 2021 ambapo viongozi wa mataifa mbalimbali ulimwenguni, Kenya ikiwemo, waliahidi kupiga jeki mikakati ya kukabili athari hizo.

  • Tags

You can share this post!

Penalti ya Sadio Mane yasaidia Senegal kuzamisha Zimbabwe...

Jinsi ya kuandaa burger

T L