• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
AKILIMALI: Asihi wakulima kukumbatia kilimo kidijitali

AKILIMALI: Asihi wakulima kukumbatia kilimo kidijitali

Na RICHARD MAOSI

KUMEKUWA na ongezeko la hitaji la zao la ngano, nje ya nchi, ingawa ni wakulima wachache hususan kutoka maeneo kame, ambao wanakuza mmea wenyewe.

Hata hivyo changamoto kubwa ni ile ya upungufu wa vipande vya ardhi mijini jambo linalofanya wakulima wengi kutoweza kukidhi mahitaji ya soko.

Kwa upande mmoja maendeleo ya teknolojia yanaonekana kushika kasi huku wakulima wengi wakihimizwa kukumbatia mifumo ya kisasa kuendesha kilimo sahihi.

Akilimali ilizungumza na Dickens Kiprop kutoka eneo la Chinese katika Kaunti ya Uasin-Gishu ambaye alisema amekuwa akiendesha kilimo cha ngano kwa miaka 25 sasa.

Anasema ngano ni mojawapo ya mazao ambayo soko lake ni nzuri humu nchini, ikizingatiwa kuwa ni kiungo muhimu katika lishe za kila siku.

Katika ardhi ya ekari tano anaweza kuvuna magunia 150, hii ikimaanisha kuwa anapata maguna 30 kutoka kila ekari, lakini faida yake nyingi huendea vibarua wakati wa kuvuna, kupakia na kupakua shehena ya mazao.

“Ikilinganishwa na mahindi ngano humpatia mkulima baina ya Sh150-200 kwa kilo moja kinyume na unga wa mahindi ambao ni Sh60 ,” akasema.

Anasikitika licha ya ngano kuwa na soko kubwa humu nchini na kimataifa, tija yake ni ndogo kwa wakulima ikizingatiwa kuwa gharama ya kukuza mmea huu ni kubwa.

Anasema kukuza ngano sio rahisi ikizingatiwa kuwa wadudu sugu hushambulia mazao yakiwa shambani, hivyo basi kudhibiti hali hii kunahitaji uangalifu ili mkulima asije akaharibu virutubishi na maliasilia kwenye udongo.

Ukosefu wa mitindo mwafaka huwafanya wakulima kulima katika sehemu kubwa isipokuwa mazao wanayopata ni kidogo.

“Aidha hufanya viwanda kununua mazao ya ngano kwa bei ya chini, hali ambayo huathiri wakulima wakashindwa kuongeza kiwango cha uzalishaji,” akasema.

Vilevile takwimu zinaonyesha kuwa bei ya ngano imekuwa ikipanda kila kukicha, isipokuwa wakulima wachache humu nchini ndio wametwikwa jukumu la kuzalisha mmea huu.

Lakini Kiprop anaona kuwa ili kufanikisha kilimo cha ngano, ubunifu wa teknolojia unafaa kupatiwa kipaumbele ili kuwapunguzia gharama

Mashine za kisasa ambazo zinaweza kuharakisha upanzi, kupalilia na kuvuna zitakuwa za manufaa ikizingatiwa kuwa mmea huu haufai ukae sana shambani, kwani unaweza kuathiriwa na mvua au joto jingi kupita kiasi.

Mmea wa ngano huchukua miezi miwili hivi kabla ya kukomaa, huku nafaka zikichukua hadi miezi minne ili ziwe tayari kuvunwa,”akasema

Alieleza kuwa ni lazima kuwa mvumilivu kwani mara nyingi wakulima hupanda mara moja kwa mwaka.

Lakini mnamo 2018 Kiprop alitembelea maonyesho ya kilimo ya Eldoret ASK ambapo alipata mafunzo ya kutumia combine harvestor.

Awali Kiprop alikuwa mgumu kukumbatia mfumo huu akiamini kuwa gharama yake ni ghali, hatimaye alitumia akiba yake na kuomba mkopo katika benki akanza kuendesha kilimo kidijittali.

Kilimo kidijitali

Vincent Sufunya ambaye ni mwanauchumi na mtaalam wa mashine za ukulima anasema kuwa teknolojia inaweza kutoa suluhu kwa ukulima.

Vincent anaongezea kuwa idadi ya watu ulimwenguni inaendelea kuongezeka ila mashamba yanaendelea kupungua.

“Ina maana kuwa wakati mmoja raia watahitaji kiwango kikubwa cha chakula endapo mifumo ya kisasa itapatiwa kipaumbele,” akasema.

Anasema kwa sababu ya kile kinachofahamika kama minimal wastage mitambo kama combine harvestor inaweza kumpatia mkulima baina ya magunia 40-50 kwa ekari moja.

Mbinu za kienyeji kama kupalilia kupitia majembe, kupalilia na kuvuna hazitatosha kulisha ongezo la watu ulimwenguni hali ambayo itawalazimu wakulima kukimbilia teknolojia ya mitambo kama hii.

You can share this post!

Rais Kenyatta azindua kiwanda cha kutengeneza silaha za...

KILIMO NA ELIMU: Digrii haikuwa kiunzi kwake kuzamia kilimo...