• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:10 PM
AKILIMALI: Biashara ya vyungu vya udongo inampa mwanga

AKILIMALI: Biashara ya vyungu vya udongo inampa mwanga

Na SAMMY WAWERU

WINNIE Ndung’u ni mama mwenye furaha na tabasamu kutokana na kazi ya ubunifu anayofanya.

Ni mfinyanzi, na hutengeneza vifaa vya matumizi ya nyumbani, hususan vya jikoni, kwa kutumia udongo.

Chini ya kampuni yake, The Clay Republic, anayoshirikiana na mfanyabiashara mwenza, Peter Shardie Musire, hujaribu kuvumbua vyombo vya kisasa, kuviimarisha, kuanzia vifaa vya kuhifadhia maji na vyungu vya mapishi.

Vilevile, katika ya wawili hawa iliyoko eneo la Kangemi, kiungani mwa jiji la Nairobi, huunda vikaangio, vyungu vya kuchoma au kukaanga samaki wakiwa wazima, bila kuwakata kuwa vipande na pia kuchemsha mahindi.

“Isitoshe, huwa tunatengeneza vikombe, sahani, vyungu vya maua na majiko ambayo hudhibiti na kupunguza matumizi ya moto,” Winnie asema.

Mjasirimali huyu, anasema lengo la The Clay Republic ni kuibuka na vifaa ambavyo vina manufaa kiafya.

“Badala ya kutumia friji unaweza kuhifadhi maji kwa kutumia chungu. Maumbile ya udongo yana Iron, Calcium na Magnesium, madini muhimu sana kwenye mwili wa binadamu,” anasema.

Winnie anasema vyungu wanavyofinyanga huhifadhi unyevuunvyevu wa maji na joto kwenye chakula, na ambavyo vinaweza kutumika kwa njia tofauti. Kupika na kusafu.

“Vyungu vya maji huviboresha. Kando na kuviunda kuhifadhi maji, huviweka tapu na standi ya kusimamisha,” adokeza.

Mama huyu amejaribu biashara tofauti, kuanzia ya uuzaji wa nguo, viatu na nafaka, ila hii ya kufinyanga vyungu anakiri imemkubali.

Anasema alianza utafiti wa biashara ya vyungu vya udongo 2019, na kufikia Aprili 2020, alikuwa ameiingilia.

Licha ya kuwa yeye pamoja na mfanyabiashara mwenza, inawasaidia kujiendeleza kimaisha, Winnie anasema ni mradi wa kuinua na kupiga jeki kina mama na vijana kule mashinani.

Aidha, ana makundi manne, Kendu Bay – Kaunti ya Homa Bay, Kakamega na eneo la Ukambani, ambayo hushirikiana nao katika kutengeneza bidhaa.

Idadi kubwa ya kina mama wana umri kati ya miaka 60 – 80, ambao Winnie anataja wamekuwa katika ufinyanzi wa vyungu kwa muda mrefu.

Huku asilimia 90 ya udongo bora ukitoka Kakamega na Homa Bay, Winnie anasema kina mama hao hufunza vijana jinsi ya kufinyanga vyungu.

Anasema kampuni ndiyo hujiri na ubunifu, asilimia 70 ikitoka kwa wateja. “Baada ya kuchora, huwapa kazi ya kutengeneza chini ya uangalizi wetu,” asema.

Anasema kwa mwezi kundi la watu 20 huunda karibu vyungu 100.

Kabla kuingia sokoni, vyungu huchukua kati ya siku 21 – 28 kukauka na kuboreshwa.

Gharama kutengeneza inategemea maelezo ya mteja na muundo anaotaka.

“Huwa tunafanya vipimo vya udongo kabla ya kufinyanga, tunasimamia shughuli za kutengeneza na kuthibitisha ubora wa bidhaa,” anasema Peter Shardie Musire, mkurugenzi mwenza wa Winnie na ambaye pia anajukumika kukagua ubora.

Bei ya bidhaa zao ni kati ya Sh800 – 7, 500, mitandao ya Facebook, Twitter, Instagram, WhatsApp na tovuti ya kampuni na ambayo imesajiliwa, ikiwa majukwaa kusaka wanunuzi.

Huku mradi huo ukiwa wa kuimarisha maisha ya kina mama na vijana na kuhamasisha haja ya kurejelea vifaa asilia katika mapishi, kuhifadhi vyakula na maji, mbali na wateja wa humu nchini, wafanyabiashara hao wameweza kupenya soko la nje.

Aidha, wana wateja kutoka Dubai, Sudan Kusini na Uganda.

Winnie anaiambia Taifa Leo kwamba wamepata wanunuzi kadha kutoka Amerika wanaoagiza kwa wingi, na kwa sasa wanatafuta laini kunogesha soko la bidhaa zao Australia na Uturuki.

Kupenya soko la nje ya nchi, hata hivyo, Winnie anasema si rahisi, kutokana na gharama ya juu kupaki vyungu na pia kuvisafirisha.

Changamoto nyingine ni wakati wa mvua, vyungu huchukua muda mrefu kukauka.

“Kwa sasa tunatafiti jinsi ya kutengeneza chupa za maji kwa kutumia udongo na pia dispensa. Tunataka kuangazia matatizo ya afya yanayosababishwa na vifaa tunavyotumia kula, kunywa na kuhifadhia vyakula na maji. Haja ipo turejelee mila na tamaduni kama Waafrika, katika mdahalo mzima wa vyakula na vinywaji,” Winnie anasisitiza, akielezea mipango waliyonayo.

You can share this post!

Patrick Vieira akubali kuwa kocha wa Crystal Palace

Masharti magumu zaidi yanukia kwa timu za kigeni Japan...