• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
AKILIMALI: Kuku wa kienyeji wanampa donge nono

AKILIMALI: Kuku wa kienyeji wanampa donge nono

Na SAMMY WAWERU

MBALI na kuwa mfugaji wa mbuzi wa maziwa, Esther Muthoni Maina ni hodari katika kufuga kuku. 

Ni mfugaji wa kuku halisi wa kienyeji, wanaoachiliwa kujitafutia lishe hasa katika maeneo ya mashambani.

Safari ya kufikia alipo katika ufugaji wa ndege hao, ilianza kwa kuku mmoja pekee.

“Mama rafiki yangu wa karibu alinipa koo mmoja, akanieleza hataniuzia aje aliwe na mwewe,” Muthoni akaambia Taifa Leo kwenye mradi wake ulioko eneo la Muruguru, Kaunti ya Nyeri.

Ni tuzo ambayo kati ya 2012 – 2015, ilikuwa imempa zaidi ya kuku wengine 50.

Huku takwimu za Idara ya Ufugaji Nchini, zikionyesha idadi ya wafugaji wa kuku Kenya iliongezeka 2020, hususan baada ya taifa kukumbwa na janga la Covid-19, Muthoni anasema ni shughuli ya ufugaji-biashara asiyojutia kuhusishwa nayo.

Idara husika, inasema wengi wa walioathirika kufuatia virusi vya corona kwa kupoteza ajira, waliingilia ufugaji wa kuku.

Muthoni kwa sasa ana jumla ya kuku 21 wa kienyeji, 16 wakiwa koo wa kutaga mayai na jogoo ni watano.

“Yai halipungui Sh15. Nikifanya hesabu, ikizingatiwa kuwa huwapa chakula cha madukani mara moja pekee kwa siku, mapato yake ni faida,” aelezea.

Malisho mengine ni punje za mahindi na mboga, huku wakijituma kujitafutia nyasi na wadudu vipenzi wa kuku.

Esther Muthoni Maina akilisha kuku wake halisi wa kienyeji katika mradi wake ulioko eneo la Muruguru, Kaunti ya Nyeri. Picha/ Sammy Waweru

Kwa mujibu wa maelezo yake, mfugaji huyu huingiza Sh450 kwa kila kreti ya mayai.

Wanunuzi wa mayai ni majirani na wenye maduka rejareja eneo la Muruguru, Nyeri.

Cha kuridhisha katika ufugaji wa kuku halisi wa kienyeji, ni vigumu kuugua, hivyo basi kero ya magonjwa si hoja kwa mfugaji.

Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya ufugaji wanasema changamoto inayojiri kwa kuku wa kuachiliwa kujitafutia lishe endapo kutaibuka na mkurupuko wa maradhi, wote wanaotangamana nao watakuwa katika hatari ya kuugua na hata kufariki.

“Ndio maana huskia kijiji kizima kuku wamefariki kutokana na ugonjwa, kwa sababu ya msambao wanapotangamana, endapo utalipuka. Ni muhimu wafugaji wahakikishe kuku wanapata chanjo ya maradhi ibuka,” Morris Irungu daktari wa mifugo Kiambu anashauri.

Kando na mauzo ya mayai, Muthoni anasema msimu wa Krismasi, bei ya kuku hunoga.

“Koo hapungui Sh700 na jimbi Sh1,000,” asema.

You can share this post!

Ruto akataa talaka ya Uhuru

Wito viongozi wa Mlima Kenya wajipange wawe pamoja kisauti