• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:50 AM
AKILIMALI: Sungura ‘mjanja’ ila thamani yake kubwa ukizamia ufugaji wake

AKILIMALI: Sungura ‘mjanja’ ila thamani yake kubwa ukizamia ufugaji wake

Na PETER CHANGTOEK

HUKU akivalia bwelasuti yenye rangi ya kijani, Emanuel Adundo, awakagua sungura wake waliomo ndani ya vibanda anavyovitumia kuwafuga, katika eneo la Syokimau.

Yeye ni mkulima anayeshughulika na ufugaji wa sungura aina ainati, na kuuza nyama ya wanyama hao, mbolea na mkojo wa sungura.

Mkulima huyo ni mmiliki wa Genrab Farm, aliloliasisi miaka miwili iliyopita.

“Nilianza kuwafuga sungura kama uraibu tu. Nilikuwa nikiwapenda sana sungura, na kwa kuwa nina sehemu ya kutumia, nikaamua kuwafuga,” anaeleza mkulima huyo, mwenye umri wa miaka 34.

Adundo, aliyesomea shahada ya Bioteknolojia ya Kilimo, katika Chuo Kikuu cha Moi, anafichua kuwa, sungura huzaana haraka sana, na kwa sasa, ana sungura takribani 400.

Alianza kwa kuutumia mtaji wa Sh10,000, pesa taslimu alizozitumia kuwanunua sungura wanne; watatu wa kike na mmoja wa kiume. Aliwanunua kwa Sh2,000 kila mmoja. Akazitumia hela zilizosalia kwa shughuli ya kuvijenga vibanda anavyovitumia kuwafuga.

Kabla mkulima huyo hajaanza kuwafuga sungura hao, alifanya utafiti wa kutosha, kwa kulizuru shamba moja, lililokuwa likimilikiwa na mfugaji wa sungura. Akajifunza mengi kuko huko. Aidha, akatumia mitandao kufanya utafiti zaidi kuhusu ufugaji faafu wa sungura.

Adundo, ambaye huwalisha sungura wake kwa kuzitumia lishe za madukani, majani ya mimea fulani na nyasi, huwalisha mara mbili kwa siku. Pia, huhakikisha kuwa wao hupewa maji safi ya kunywa.

Mkulima huyo, anayefuga sungura kama vile: Californian White, Chinchilla, Dutch, Havana, na Flemish Giant, anadokeza kuwa, ni watu wachache ambao hushughulika na ufugaji wa sungura katika eneo hilo.

Hapo awali, alikuwa akijishughulisha na ukuzaji wa mimea ya spinachi na sukumawiki, lakini aliacha shughuli hiyo.

Ili kuzuia uzalishanaji kati ya sungura wa uzao mmoja, mkulima huyo huwachukua sungura wa kiume kutoka sehemu tofauti, ili kuwatumia kuwatungisha mimba wale wa kike.

Mojawapo ya changamoto ambazo amewahi kuzipitia ni kufa ghafla kwa baadhi ya sungura wake.

“Baadhi ya sungura hawaonyeshi dalili za kuugua, utawapata tu wakiwa wamekufa,” asema Adundo.

Baadhi ya sungura wanaofugwa na Emanuel Adundo. Picha/ Peter Changtoek

Yeye hushirikiana na mkewe katika shughuli hiyo, japo ana mfanyikazi mmoja, ambaye huwasaidia katika utunzaji wa wanyama hao.

Anasema kuwa, sungura wana magonjwa kadha wa kadha, japo mengi huweza kuzuia kwa urahisi, kwa kujenga vibanda vilivyo bora.

“Ugonjwa unaowaathiri sungura mara kwa mara ni ule unaowafanya kuhara,” asema, akiongeza kuwa, yeye huuzuia ugonjwa huo kwa kuwapa lishe zisizokuwa na unyevu.

Huuza nyama ya sungura kwa Sh700.

“Nina mikakati kadhaa ninayoitumia ili kuuza. Kwanza, hutumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook. Pili, ni kwa kuwaelezea wateja kuhusu nyama ya sungura. Wakati fulani, mimi huwapa nyama ya sungura waonje, na baada ya kuonja, hununua,” asema.

Adundo anawashauri wale wanaonuia kujitosa katika ufugaji wa sungura, kuyazuru mashamba yanayoshughulika na ufugaji wa sungura kwanza, kabla hawajaanza kufanya shughuli hiyo. Isitoshe, anawashauri wafanye utafiti wa kina kwanza.

Pia, anaongeza kuwa wanafaa wawe na subira kwa muda wa angaa miezi sita, kabla hawajaanza kuwauza sungura wao.

Mbali na kuwauza sungura wakiwa hai na baadhi yao wakiwa wamechinjwa, mkulima huyo pia huuza mbolea na mkojo wa sungura, ambao hutumiwa katika ukuzaji wa mimea mbalimbali. Mbolea ya sungura ina kiwango cha juu cha naitrojeni.

Mkulima huyo, humwuza sungura mwenye umri wa miezi miwili kwa Sh800, mwenye umri wa miezi mitatu kwa Sh1,000 na mwenye umri wa miezi minne kwa Sh1,500. Pia, humwuza sungura mwenye umri wa miezi mitano kwa Sh2,000 na wa kiume kwa Sh2,500.

Aidha, huuza mbolea ya sungura kwa Sh300 kwa kila gunia la kilo 50, na mkojo wa sungura kwa Sh50 kwa lita moja.

Anafichua kuwa, katika siku za usoni, anaazimia kuongeza idadi ya sungura anaowafuga kuwa zaidi ya 1,500.

Aidha, anapania kuongeza thamani kwa kutengeneza soseji na sambusa kutokana na nyama ya sungura.

Kwa mujibu wa Dkt Wyckliff Ng’etich, kutoka katika Idara ya Mifugo, Chuo Kikuu cha Egerton, ni kuwa, vifo vya ghafla kwa sungura, vyaweza kusababishwa na kula lishe zenye sumu, kubadilika kwa mazingira, msongo wa mawazo, miongoni mwa vyanzo vingi vinginevyo.

“Lishe zinazotolewa shambani zinaweza kuwa na mimea yenye sumu. Lishe za madukani ni salama, iwapo zitahifadhiwa vyema na kanuni faafu kuzingatiwa.”

You can share this post!

AKILIMALI: Anajichumia kwa kuunda unga wa mabuyu na mafuta...

AKILIMALI: Anaelewa kuhangaikia nafsi yake kwa njia halali