• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
AKILIMALI: Usitegee tunda la papai pekee, uza pia mbegu zake

AKILIMALI: Usitegee tunda la papai pekee, uza pia mbegu zake

Na PETER CHANGTOEK

ANA tajriba pana katika shughuli ya ukuzaji wa mipapai.

Alex Kamwinzi, alijitosa katika ukuzaji wa mipapai mwaka 2009, na kwa sasa yeye ni mkulima anayefahamika mno kwa shughuli hiyo. Aidha, ameanzisha kampuni inayozalisha mbegu za mipapai.

Alijitosa katika kilimo hicho alipokuwa na umri wa miaka 19, na kwa kuutumia mtaji wa Sh150,000.

Hata hivyo, hakuwa ameigeuza zaraa hiyo kuwa biashara, hadi mwaka 2015.

“Nilitiwa hamasa na mkulima mmoja kijijini, ambaye alikuwa akiyachuma matunda mengi kwa mimea yake ya mipapai,” asema.

Kamwinzi, ambaye alisomea Shahada ya Bayokemia na Bayolojia ya Molekyuli katika Chuo Kikuu cha Egerton, na kuhitimu mwaka 2014, hutumia shamba la ekari moja kuikuza mipapai, katika kitongoji cha Mandoi, eneo la Wote, Kaunti ya Makueni.

Kabla hajaipanda miche ya mipapai, yeye hulitayarisha shamba ipasavyo. Pia, huyaondoa magugu yaliyoko shambani.

“Jambo lililo kubwa ni kuyachimba mashimo ya futi 2 (kina) kwa futi 2 (upana) kwa futi 2 (urefu), na kuacha nafasi ya mita 2 kwa mita 2 (kutoka kwa mmea mmoja hadi mwingine),” asema, akiongeza kuwa, huchanganya mchanga na mbolea kwa urari wa 3:1.

Kwa wakati huu, anasema kuwa ana mimea 500 iliyokomaa.

“Nina mfanyakazi mmoja na vibarua sita ninaowaajiri kwa kutegemea wingi wa kazi,” adokeza Kamwinzi.

Baada ya kuipanda miche ya mipapai, mkulima huyo huhakikisha kwamba mimea inapaliliwa ili kuyaondoa maotea yanayoota shambani.

Aidha, huhakikisha kuwa mimea inapata maji ya kutosha.

Mbali na hayo, mkulima huyo anasema huhakikisha kuwa wadudu waharibifu na magonjwa yanazuiwa yasiharibu mimea shambani.

Pia, hupogoa ili kuiwezesha mimea kunawiri vyema na kuzaa matunda yenye ubora wa hali ya juu.

Kinyume cha matarajio ya wengi, mkulima huyo anadokeza kuwa, biashara yake haijaathiriwa na maradhi ya Covid-19.

“Hatujawahi kupata mauzo kiasi hiki; Mungu ni mwema.”

Yeye huikuza mipapai aina ya Calina papaya, Malkia F1 na aina iliyoboreshwa inayojulikana kwa jina Solo Sunrise.

“Mche unafaa kupandwa katikati ya shimo na kunyunyiziwa maji iwapo hakuna mvua,” asema, akiongeza kuwa, mipapai iliyoboreshwa hutoa maua baada ya siku 55 baada ya kupandikizwa.

Anaongeza kuwa, matunda huanza kuchumwa baada ya miezi minane tu.

Kwa mujibu wa Kamwinzi ni kuwa, aina hizo za mipapai huzaa matunda 100 hadi 150 kwa mwaka mmoja.

Hata hivyo, anasema kwamba amewahi kuzipitia changamoto kadhaa katika shughuli hiyo.

Mimea yake imewahi kuathiriwa na baadhi ya magonjwa kama vile anthracnose na kuvamiwa na wadudu kadha wa kadha, mathalan vidung’ata (mealybugs).

“Tunauza kwa bei ya Sh70 kwa kilo moja. Tunda moja huwa na uzito wa kilo moja na nusu kwa wastani. Sisi huuza kupitia kwa mitandao na kwa wateja wengine wanaotutumia oda,” afichua Kamwinzi.

Mkulima huyo anasema kuwa ukuzaji wa mipapai una faida, iwapo kanuni zote za kilimo, na agronomia zitazingatiwa.

Kwa wakati huu, mkulima huyo pia ana kampuni inayozalisha mbegu bora za mipapai, na inajulikana kama Stawi Seeds Limited.

Kampuni hiyo imekubaliwa kuendesha shughuli hiyo na asasi husika.

“Kwa sababu kuna uhitaji mkubwa wa mapapai, tunatazamia kuwapa wakulima kandarasi ya kuyazalisha matunda hayo. Pia, tunapanga kuanza kuongeza thamani kwa mapapai, kwa kutengeneza jamu,” afichua mkulima huyo.

You can share this post!

Chelsea wapepeta Villarreal na kutwaa taji la Uefa Super Cup

Makala ya Dimba – Beach Bay FC