• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 1:02 PM
Ananyoa kwa shoka na wateja wamejaa kibao

Ananyoa kwa shoka na wateja wamejaa kibao

Na WANGU KANURI

Julius Mwangi, 24, ni kinyozi ambaye amevuma kwa kutumia shoka kuwanyoa wateja wake. Kinyozi huyu aliamua kuanza kutumia shoka miezi mitatu iliyopita baada ya kutambua kuwa ipo haja ya kuwa na njia ya kipekee ya kuwanyoa watu.

Baada ya kipato kudidimia kutokana na kupungua kwa wateja, Julius alionelea ni heri aibuke na wazo la kipekee kuvutia wateja. “Nimebobea katika kutumia mashine lakini nilitaka njia mbadala na ya kipekee ya kuwanyoa watu,” akaambia Akilimali ilipozuru kinyozi alikoajiriwa mtaa wa Thindgua, Kaunti ya Kiambu.

Upekee wa shoka katika unyoaji ni kuwa hakuna unywele wowote unaobaki kichwani. Shoka hili ambalo Julius hutumia kuwanyoa wateja wake ni lile ambalo zamani lilitumiwa na wenye bucha kukata mifupa.

Julius ambaye kwa sasa amebandikwa jina ‘the shoka guy,’ anajionea fahari kwa kuweza kuvuma kwa unyoaji huu. “Hisia mbalimbali za watu zimenifaa. Watu wanafika hapa kuhakikisha kama ni kweli ninanyoa kwa kutumia shoka na wanapojionea, wanakubali niwanyoe,” akasema.

Hata ingawa mitindo ya unyoaji wa shoka haujakuwa maarufu, Julius ananuia kuimarisha unyoaji huu kwa kuhakikisha kuwa shoka linaweza kunyoa mitindo mbalimbali.Kwa sasa, mtindo wa kunyoa nywele zote ambao kwa Kizungu unaitwa ‘Jordan’, mtindo wa kunyoa nywele nusu ambao unafahamika kama ‘Semi-jordan’ na unyoaji wa ndevu haswa kwa kuweka mitindo ambayo mteja atataka, ndiyo mitindo ambayo shoka linaweza kufanikisha.

Unyoaji huu wa shoka unamhitaji kinyozi kuwa makini na mwangalifu sana anapomnyoa mteja. “Hata ingawa siwezi nikamkata mtu, ule uzito wa shoka wenyewe unanilazimu niangalie kwa kina ninachofanya nikimhudumia mteja wangu,” akaeleza.

Hali kadhalika, unyoaji huu una matakwa yake mahususi kama anavyoeleza Julius. Kinyozi anapaswa kuwa na maji karibu na kila baada ya dakika chache alipanguse shoka lile. Pia, kinyozi anapaswa kuhakikisha kuwa mteja wake hadondokwi na jasho kiasi cha kuifanya ngozi yake iwe nyororo.

Sababu ya muda ambao unatumiwa ili kuhakikisha kuwa mteja amenyolewa vizuri, bei ya kunyolewa kwa shoka inatofautiana sana na ile ya mashine. Aghalabu, Julius hutumia dakika 25-30 anapomnyoa mteja wake akitumia shoka ikilinganishwa na dakika 15 anapotumia mashine.

Ili kuhakikisha kuwa amewakinga wateja wake akitumia kifaa kile, Julius anathibitisha kuwa kuna mikakati ambayo amechukua. Yeye huhakikisha kuwa shoka lake limetiwa makali sana kisha kuliosha vizuri na kuliweka kwenye mashine inayowezesha kuua viini.

Hata hivyo, unyoaji huu unaotumia shoka ni ufundi ambao unapaswa kukubaliwa na watu kama anavyoeleza Dennis Mwangi, mteja ambaye alifika pale ili kunyolewa na lile shoka.“Mashine inapowanyoa watu wengi, huwa na joto lakini hii si hali ukinyolewa kwa shoka,” akaeleza baada ya kunyolewa.

Wateja wanaofika hapa kunyolewa kwa shoka huwa na uoga, jambo ambalo Dennis anathibitisha. “Kuna uoga unaomjia mtu kwa sababu hili si jambo la kawaida. Hata hivyo, itamlazimu mtu kuzoea kwani hata wakati wa kwanza kutumia mashine watu walikuwa na uoga lakini kwa sasa hawauhisi huo uoga,” akasema Bw Dennis.

Umashuhuri wa shoka katika kazi hii ya kuwanyoa watu si jambo ambalo limewahi fanywa na mtu yeyote lakini kwake Julius shoka ni kifaa kilicho na manufaa sana. “Wateja hawakosi kunyolewa wakati ambapo stima zimepotea kwani shoka haihitaji stima.

Isitoshe, kwa wateja ambao hawapendi kuonekana na nywele hata ile kidogo, shoka inawafaa.”Awali Julius alipokuwa akitumia mashine, kama anavyosimulia, meno ya mashine ile ilikuwa ikiharibika sababu ya kushinda akihakikisha kuwa ni safi na haina viini vyovyote vile.

Hata hivyo, kwa sasa hicho si kikwazo.Julius anatabiri kuwa kwa kuendelea kutumia shoka yake kuwanyoa wateja wake, kifaa hiki kitaweza kukubaliwa na kutumiwa na vinyozi wengine.

You can share this post!

Kilimo champa ajira na kumlipia karo ya chuoni

TAHARIRI: Ipo shida wauguzi kutofahamu lugha

T L