• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 3:57 PM
Anavyopunguza gharama kufuga kuku kwa kutumia Azolla

Anavyopunguza gharama kufuga kuku kwa kutumia Azolla

NA SAMMY WAWERU 

MZEE Ken Macharia, amekuwa akiendeleza ufugaji wa kuku tangu 1990. 

Aliuingilia kama mojawapo ya njia kujipa pato la ziada, ikizingatiwa kuwa yeye ni mfanyabiashara. 

Ni mfugaji katika Mtaa wa Golf View, Gatanga, Kaunti ya Murang’a na anasema endapo kuna wakati ambapo biashara ya kuku imekumbwa na ugumu ni baada ya Kenya kuwa mwenyeji wa janga la Covid-19. 

Malighafi kutengeneza malisho ya mifugo nchini na katika masoko ya kimataifa, bei imeongezeka mara dufu baadhi ya viwanda vikifunga milango yake. 

Ni changamoto ambazo zimelemea wafugaji wengi, wengine wakilazimika kufuga kuku kukidhi mahitaji ya nyumbani pekee; mayai na nyama, badala ya biashara. 

Ken Macharia, mfugaji wa kuku Murang’a akielezea kuhusu matumizi ya Azolla kupunguza gharama ya malisho. PICHA|SAMMY WAWERU

Macharia anasema, alikuwa akifuga hadi kuku wapatao 3, 600 wa mayai, wa kienyeji walioimarishwa ila kwa sababu ya mfumko wa bei ya chakula sasa anachezea wastani wa 500.

Kero hiyo ikiwa nusra izime jitihada zake, mfugaji huyu amegundua matumizi ya mmea maalum aina ya Azolla kama njia bora kupunguza gharama. 

Zao hilo ni chanzo cha Protini ya mimea. 

Ken Macharia, mfugaji wa kuku Murang’a kwenye dimbwi la kukuza Azolla. PICHA|SAMMY WAWERU

Aidha, ni mbadala wa soya na omena, kwani malighafi yake ni ghali sana. 

Macharia ana mabwawa sita kwa ajili ya kuzalisha Azolla.

Mmea huo unakadiriwa kuwa na kati ya asilimia 25-35 ya Protini, 10-15 ya madini, na 7-10 inayojumuisha mchanganyiko wa asidi za Amino, Bio-aktivi, na Biopolima.

Macharia anasema mmea huo ni rahisi kukuza, na unachukua siku 14 tu kukomaa baada ya mbegu kupandwa kwenye mabwawa.

Mimea iliyobaki baada ya mavuno hutumika kuendeleza uzalishaji zaidi. 

Mfanyakazi wa Ken Macharia, mfugaji wa kuku Murang’a akivuna Azolla. PICHA|SAMMY WAWERU

Mbali na maji, mabwawa yanawekwa mbolea ya mifugo au fatalaiza.

“Kilo moja ya soya inauzwa Sh140, na chini ya siku 14 tunavuna hadi kilo 20 za Azolla. Kwa wastani, kilo moja inahitaji Sh20 kuzalisha,” Mzee Macharia aelezea. 

Anafichua kwamba Azolla imemsaidia kupunguza gharama ya Protini kwa zaidi ya asilimia 75. 


Mfanyakazi wa Ken Macharia akilisha kuku Azolla.
Kuku wakishabikia Azolla. PICHA|SAMMY WAWERU

“Ninahimiza wafugaji kukumbatia matumizi ya mmea huu hasa kwa kuku,” ashauri.

Hukausha Azolla, kisha kulisha kuku na pia inaweza kutumika ikiwa mbichi. 

Isitoshe, mmea huo pia hupewa ng’ombe na samaki.

“Gharama ya malighafi yenye virutubisho vya Protini kuunda malisho ya mifugo, kote duniani ni ghali. Mkulima yeyote anayetaka kufanikiwa katika uzalishaji wa mayai na nyama, lazima apate chanzo cha Protini cha bei rahisi,” anasema Francis Faluma, mtaalamu kutoka Serikali ya Kaunti ya Kakamega. 


Kuku wa Ken Macharia wakishabikia Azolla. PICHA|SAMMY WAWERU

Mbinu nyingine kupunguza gharama ya ufugaji wa kuku ni wadudu maalum aina ya Black Soldier Fly (BSF), Faluma adokeza. 

“Azolla ikitumiwa pamoja na BSF, zinasaidiana katika kuwepo na kiwango cha juu cha Protini,” aelezea. 

Ni mbinu za kupunguza gharama ya ufugaji, anbazo wakulima wakizikumbatia itasaidia kushusha bei ya mayai na kuku ambayo kwa sasa haikamatiki. 

  • Tags

You can share this post!

Jinsi watalii wawili walivyopoteza mali ya thamani...

Chiloba asema tuhuma dhidi yake ni ‘madai tu’

T L