• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
Jinsi watalii wawili walivyopoteza mali ya thamani wakiogelea

Jinsi watalii wawili walivyopoteza mali ya thamani wakiogelea

NA FARHIYA HUSSEIN

WATALII wawili waliokuwa wamezuru Kaunti ya Mombasa wamekwama baada ya kuibiwa bidhaa zao ndani ya hoteli eneo la Shanzu.

Kulingana na wawili hao waliokuwa wakilala katika hoteli ya kifahari ya Royal Shaza, walikuwa wametoka chumbani mwao jioni ya Septemba 13, 2023, na waliporudi walipata mali yao ikiwa imeibwa.

“Kando na sababu za utalii, tulikuwa Mombasa kwa mkutano au mafunzo ambayo yalikuwa yakifanyika kati ya Septemba 11 na Septemba 16. Tulifika hotelini wiki moja kabla ya mafunzo kuanza ili kujitayarisha mapema,” alieleza mmoja wao.

Wawili hao ambao walikataa kutajwa majina yao kwa sababu za kiusalama na kutokana na uchunguzi unaoendelea, wametaja asili zao. Mmoja ni raia wa Uingereza anayefanya kazi nchini Ufilipino naye mwingine ni raia wa Canada anayefanya kazi nchini Thailand.

“Siku hiyo tulikuwa tumehudhuria kikao cha mafunzo. Nakumbuka ilikuwa siku yetu ya tatu ya masomo na ilipofika jioni, tuliamua kuenda kuogelea katika kidimbwi kilichoko hapo hotelini kwa dakika chache. Ilikuwa saa kumi na moja jioni. Tuliporudi chumbani tulipata mlango ukiwa umevunjwa na sanduku la kuhifadhi vitu muhimu lilikuwa limetoweka,” mmoja wa watalii hao alieleza.

Wageni hao walisema ndani ya chumba hicho kulikuwa na simu mbili za mkononi, tarakilishi mbili na kamera, na ndani ya sanduku la kuhifadhi vitu muhimu kulikuwa na dola 900,000 sawa na Sh132 milioni na hati zao za kusafiria.

“Tuliripoti suala hilo mara moja kwa wasimamizi wa hoteli ambao walitoa taarifa kwa polisi na tukaripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Bamburi ambapo kilinakiliwa kwa nambari C/ORG/1/9/VOL11/016/2023,” akaeleza mmoja huyo.

Walibainisha kuwa safari hiyo ilikuwa ya nne kwao nchini Kenya na hawajawahi kukumbana na hali kama hiyo katika ziara zao tatu za awali.

“Sitaki kuelekeza kidole cha lawama kwa hoteli lakini kuna baadhi ya mambo hatuyaelewi. Kwa mfano, dakika 30 baada ya tukio hilo kutokea tuliambiwa kuwa kuna mwanamke aliyekuwa kwenye pikipiki akiwa amevaa baibui ambaye inadaiwa alirudisha hati zetu za kusafiria pale langoni na kumkabidhi mlinzi. Naelewa utovu wa usalama hutokea kila mahali lakini siku zijazo, naomba waimarishe ulinzi hotelini ili kuepusha matukio ya aina hiyo kutokea,” alisema mmoja wa watalii hao.

Wasimamizi wa hoteli walikiri kuwa waliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Bamburi na wanashirikiana na wapelelezi ili kubaini ukweli.

Mkuu wa polisi Kisauni Bw Joseph Mutungi alithibitisha kisa hicho kuripotiwa eneo la Bamburi na wameanzisha uchunguzi.

Afisa wa uchunguzi alidokeza ya kuwa wameanza kufuatilia washukiwa na hivi karibuni watawakamata.

“Tunachunguza suala hilo, tukishapata maelezo kamili nitawasiliana nawe. Tumebaini ya kuwa wale washukiwa walijisajili usiku kwenye hoteli hiyo na kushinda pale mchana wa siku iliyofuata kabla ya kuwaibia wageni jioni. Walitumia vitambulisho bandia kujisajili,” alieleza afisa huyo ambaye jina lake limebanwa kwa sababu haruhusiwi kuzungumza na wanahabari

Wageni hao walisema wanashuku kuna mtu alikuwa akiangalia kila hatua yao kwani ni chumba chao pekee ndicho kilichovunjwa.

  • Tags

You can share this post!

Wasioamini Mungu wataka kila familia iwe na mtoto mmoja

Anavyopunguza gharama kufuga kuku kwa kutumia Azolla

T L