• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
Asasi ambazo zinachangia makuzi ya lugha

Asasi ambazo zinachangia makuzi ya lugha

NA BITUGI MATUNDURA

PENDEKEZO la kutangaza Julai 7 (leo) ya kila mwaka kuwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani na UNESCO, lilitokana na utambuzi kwamba Kiswahili ni mojawapo ya lugha zinazotumiwa sana katika Jumuiya ya Afrika.

Aidha, ni kati ya lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi zaidi duniani, ikiwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 250.

Hata hivyo, mumo kwa mumo, Kiswahili kina ‘maadui’ na ‘marafiki’. Maadui wa Kiswahili wamekuwepo tangu enzi za ukoloni. Nchini Kenya, Waingereza kwa mfano walikuwa na sera zisizokuwa na mwelekeo. Walizidunisha lugha za kiasili ikiwemo Kiswahili. Hali hii iliatika kasumba miongoni mwa baadhi ya Wakenya kwamba lugha zetu za kiasili hazikuwa na umuhimu wowote.

Marafiki

Marafiki wakubwa wa Kiswahili ndani na nje ya Afrika ya Mashariki ni vyombo vya habari.

Nchini Kenya, Taifa Leo – ambalo ndilo gazeti la pekee linalochapishwa kwa Kiswahili, linafanya kazi nzuri katika kukuza Kiswahili kimakusudi.

Taifa Leo limechangia katika kubuni, kusawazisha na kusambaza istilahi mpya za Kiswahili. Mradi wake wa Newspapers In Education (NiE) una wafuasi wengi katika mfumo wa elimu nchini Kenya.

Vituo vya runinga kama vile NTV, Citizen TV, Radio Maisha, Kenya Broadcasting Corporation (KBC) n.k. vinatoa mchango muhimu katika kuathiri sera ya lugha na kutetea matumizi ya Kiswahili fasaha.

Vituo vya Redio katika mataifa ya nje kama vile Voice Of America (VOA), Redio Japan, Deutsche Welle (DW), British Broadcasting Corporation (BBC) ya Uingereza, Radio China, Radio Moscow (Urusi), Radio Rwanda (Kigali), Radio South Africa (R.S.A), Radio Tanzania na Zanzibar n.k pia hutumia Kiswahili kwa njia ya kuvutia na kuridhisha sana.

Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani hivi leo yanapaswa kuibua kani mpya miongoni mwa wadau mbalimbali wa Kiswahili.

Kunahitajika kubuniwa mikakati ya kuleta ubia si tu katika vyombo na taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na Kiswahili – bali pia kusukuma kwa pamoja ajenda za kutetea sera murua za makuzi ya Kiswahili Afrika ya Mashariki na ulimwenguni kote. Ikumbukwe kwamba, umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.

  • Tags

You can share this post!

Taasisi zinazofundisha Kiswahili ulimwenguni

Sababu za UNESCO kuteua siku ya Kiswahili duniani

T L