• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Sababu za UNESCO kuteua siku ya Kiswahili duniani

Sababu za UNESCO kuteua siku ya Kiswahili duniani

NA CHRIS ADUNGO

KUTEULIWA kwa Julai 7 kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani ni uamuzi uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamadumi (UNESCO) katika Mkutano Mkuu wa 41 mnamo Novemba 23, 2021 jijini Paris, Ufaransa.

Azimio hilo namba 41C/61 lilipitishwa na nchi zote wanachama wa UNESCO bila kupingwa na kufanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza Afrika iliyo na siku maalumu ya kuadhimishwa inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN).

Uamuzi huo ni zao la maamuzi ya kikao cha 212 cha Bodi Tendaji ya UNESCO iliyojikita katika misingi mikuu 10, ikiwemo hadhi ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha rasmi za Muungano wa Afrika.

Kiswahili pia ni lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Bunge la Afrika na ni mojawapo ya lugha za utendakazi katika UN. Isitoshe, inazungumzwa na zaidi ya watu milioni 250 ulimwenguni na ni lugha ya nne rasmi ya mawasiliano katika shughuli za Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Mkutano wa 39 wa viongozi wa SADC waliokutana jijini Dar es Salaam, Tanzania mnamo Agosti 2019, uliridhia Kiswahili kuwa lugha rasmi ya kazi katika chombo hicho, kwa kutambua mchango wake katika kujenga amani na ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika na Afrika kwa jumla.

Kwa mantiki hii, ni chombo muhimu cha kufanikisha Ajenda 2030 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), kujenga amani na kukuza ushirikiano wa kikanda hususan katika kutekeleza Mkataba wa Eneo la Soko Barani Afrika (ACFTA).

“Maadhimisho haya yamejiri kutokana na ukubwa wa Kiswahili duniani. Kati ya zaidi ya lugha 6,900 zinazozungumzwa ulimwenguni kwa sasa, Kiswahili ni lugha ya saba kutengewa siku mahsusi ya kuadhimishwa baada ya Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kiarabu, Kichina na Kirusi,” akasema Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kibabii, Prof Isaac Ipara.

Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika UN, Prof Kennedy Gastorn asema Tanzania ilipendekeza siku hii kwa sababu ni Julai 7, 1954 ndipo chama tawala cha Tanzania African Union (TANU) – kama kilivyoitwa hapo awali – kikiongozwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere, kilitambua Kiswahili kuwa silaha muhimu ya kupigania uhuru.

Mwanzilishi wa taifa la Kenya, hayati Mzee Jomo Kenyatta, naye alitumia mwito wa ‘Harambee’ kurai Wakenya kuungana ili wakabili ukoloni.

Aidha, ni Julai 7, 2000 ambapo EAC ilifufuliwa ili kurejesha ushirikiano na utangamano miongoni mwa wananchi wa Kenya, Tanzania na Uganda ambako Kiswahili kinazungumzwa zaidi. Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimejiunga kuwa wanachama wa EAC baadaye.

“Kwa hivyo, Kiswahili ni silaha kuntu ya kupigania uhuru wa mwanadamu popote alipo. Lugha hii imekuwa wenzo wa kuunganisha harakati za ukombozi na utetezi wa haki za Mwafrika tangu enzi za nira ya ukoloni. UNESCO inahimiza umoja ndani ya uanuwai wa tamaduni na lugha za ulimwengu, ukiwemo uhuru wa mtu kujieleza kwa lugha yoyote anayoiteua,” anaeleza Prof Mbuthia.

Kiswahili ni lugha ambayo si tu njia ya mawasiliano, bali kielelezo cha utamaduni kinachoonyesha utambulisho, maadili na dira ya dunia. Ni chombo ambacho kinawasilisha tofauti mbalimbali za tamaduni na mazungumzo ya ustaarabu. Ni daraja linalowezesha uhusiano wa karibu baina ya jamii na ni utajiri thabiti wa kujieleza na kubadilishana mitazamo na desturi mbalimbali.

Zaidi ya kutumiwa katika nchi nyingi za Afrika Mashariki, Kati, Kusini na Mashariki ya Kati, Kiswahili kinafundishwa katika vyuo vikuu vikubwa duniani.

Katika miaka ya 1950, UN ilianzisha Redio ya Umoja wa Mataifa na leo hii Kiswahili ni lugha ya pekee ya Kiafrika katika Idara ya Mawasiliano ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa (DGC).

  • Tags

You can share this post!

Asasi ambazo zinachangia makuzi ya lugha

SIKU YA KISWAHILI DUNIANI: Maadhimisho ya hafla ya...

T L