• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Taasisi zinazofundisha Kiswahili ulimwenguni

Taasisi zinazofundisha Kiswahili ulimwenguni

NA BITUGI MATUNDURA

HAFLA ya kwanza ya maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani hivi leo – ilivyopendekezwa na UNESCO inatupa fursa ya kutafakari nafasi ya lugha hii barani Afrika na kwenye ulingo wa kimataifa huku lugha hii ikizungumzwa na takriban watu wasiopungua milioni 200 ulimwenguni.

Pamekuwepo na dharura ya kuanza kuona Kiswahili kama raslimali kubwa. Lugha ni raslimali muhimu kama vile mafuta, maji, misitu, almasi, dhahabu n.k. Inaweza kubidhaaishwa kiuchumi.

Mataifa yenye nguvu yamebidhaaisha lugha zao kwa kuimarisha sera zao za lugha. Asasi maalum za kiserikali kama vile Oxford University Press ya Uingereza kwa mfano, huratibu mikakati na mielekeo ya maendeleo ya lugha hiyo. Goethe Insitute ya Ujerumani inaendeleza maslahi ya Kijerumani ilihali Alliance Francais ikipigia debe lugha ya Kifaransa ulimwenguni.

Ingawa Afrika Mashariki ni kitovu cha Kiswahili, juhudi za kimakusudi aghalabu hazijafanywa kuhakikisha lugha hii inabidhaaishwa, jinsi Waingereza, Wafaransa, Wajerumani, Wachina, Wajapani n.k walivyozifanyia lugha zao.

Kinaya ni kwamba, wageni wametambua umuhimu wa Kiswahili na kukifanya asusa kwa manufaa yao. Wataalamu wa Kiswahili wa Afrika Mashariki wana wasiwasi kwamba Kiswahili ‘si chetu’ tena. Kauli hii ina mashiko, hasa tunapotathmini utafiti na mwamko uliopo katika vyuo vya kigeni katika kukishughulikia Kiswahili.

Kati ya takriban vituo 49 vinavyoshughulika na utafiti na uchambuzi wa masuala ya lugha ikiwemo Kiswahili kote ulimwenguni, ni 5 tu vinavyopatikana barani Afrika. Vituo 26 vinapatikana Amerika, 12 barani Ulaya, na 2 Asia.

Mataifa ya Magharibi pia yanaenda kasi mno katika kujishughulisha na Kiswahili. Tayari vyuo vikuu zaidi ya 100 vya Amerika vinafundisha Kiswahili. Vyuo hivyo ni pamoja na Harvard, Yale, Cornell na Lose Angeles California (UCLA). Vyuo vikuu vingine ni pamoja na Ohio State Columbus, Ohio at Athens Ohio, University of Illinois, Urbana Champaigne, Michigan State University Syracuse na Winscosin. Kule Uingereza, vyuo vya London na York vinafundisha Kiswahili katika viwango vya daraja la nne na kidato cha sita.

Mataifa mengine yanayofundisha Kiswahili ni Ujerumani, Korea Kusini na Japan. Chambacho Rocha Chimerah, vyuo na wasomi hawa wamekuwa wakizuru Afrika Mashariki kila mwaka kwa minajili ya kukifanyia utafiti Kiswahili.

Jambo la kuvunja moyo zaidi ni kwamba, baadhi ya wasomi wa awali waliozuru pwani ya Afrika Mashariki walikusanya baadhi ya miswada adimu ya wasanii mbalimbali wa janibu hizo na kuihifadhi katika maktaba za kwao – hasa School Of Oriental and African Studies (SOAS), Uingereza.

Sherehe ya Siku ya Kiswahili Duniani hivyo basi inapaswa kuibua mwamko na nguvu mpya Afrika Mashariki na kote duniani kuhusu thamani ya Kiswahili.

  • Tags

You can share this post!

Hatimaye Uganda yakweza Kiswahili kuwa lugha rasmi

Asasi ambazo zinachangia makuzi ya lugha

T L