• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Baba wa watoto 16 Mandera ashangaza wengi kwa kujizolea alama 355 katika KCPE

Baba wa watoto 16 Mandera ashangaza wengi kwa kujizolea alama 355 katika KCPE

NA MANASE OTSIALO

Isack Alio Shamo, 51, baba wa watoto 16 alifanya uamuzi wa kurudi shule baada ya kiangazi kuangamiza mifugo wake na katika miaka mine iliyopita, amekuwa mwanafunzi katika kituo cha Elimu ya Watu Wazima, eneo la Mandera Mashariki.

Wakati matokeo yalipotangazwa Alhamisi Novemba 23, 2023, alisubiri kwa hamu kubwa kwa sababu yalikuwa ni yake na binti yake, ambaye pia alifanya mtihani.

Shamso Isack Alio

“Nilirudi shuleni kwa sababu nilikuwa nimekosa fursa hiyo udogoni mwangu. Nilitumia muda wangu kuchunga mifugo wa babangu,” anasema Bw Shamo.

Anasema aliagizwa na babake kuchunga ngamia na hiyo ilimaanisha kwamba alitumia muda mwingi akiwa mbali na nyumbani.

“Kuchunga ngamia ni mojawapo ya kazi ngumu zaidi kufanya kwa sababu inahitaji uende mbali na nyumbani ukitafuta malisho na maji. Hurejei jioni kama wale wanaochunga mbuzi na kondoo,” akasema.

Wakati mtihani wa KCPE ulipong’oa nanga Oktoba 30, anasema hakuwa na wasiwasi wowote akisema alikuwa amejiandaa vyema.

“Kiingereza ndio somo ambalo nilipenda zaidi na nimepata alama 63. Nilifurahia masomo yote yaliyofunzwa kwenye kituo hicho cha elimu ya watu wazima,” anasema.

Bw Shamo alipata alama 70 kwenye Hesabu, 75 Sayansi, 75 kwenye Sayansi ya Kijamii na 70 katika Kiswahili.

“Elimu ni muhimu sana na ndio kila kitu maishani. Nilitambua kwamba ninafanya kila niwezalo kuelimisha watoto wangu,” mume huyo wa wake watatu anasema.

Binti yake, Shamso Isack Alio alipata alama 384, na kumshinda kabisa babake.

Licha ya kujipatia alama nzuri ambazo zinaweza kumpatia nafasi katika shule nzuri ya sekondari nje ya Mandera, Bw Shamo anasema hayuko tayari kuacha familia yake kubwa.

“Kujiunga na sekondari nje ya Takaba itakuwa vigumu sana kwa familia yangu. Nahitaji niwe karibu ili kuhudumia familia yangu kubwa,” anasema.

Anataka serikali kuajiri walimu zaidi wa elimu ya ukubwani Mandera ili yeye na wengine wanufaike na elimu ya sekondari kwa urahisi.

“Nitakuwa naenda shuleni kuanzia saa moja jioni hadi saa nne usiku kwa sababu lazima nikimu familia yangu. Nilikuwa na biashara ya mkokoteni mjini lakini saa hii nina duka dogo. Nahitaji tu kuwa karibu na familia yangu kwa sababu wananitegemea,” akasema.

Anaomba wahisani wajitokeze kumsaidia binti yake apate karo ya miaka minne katika shule ya upili.

“Binti yangu alifanya vyema sana kwenye mtihani na najua ataitwa kujiunga na shule nzuri lakini sina uwezo wa kumsomesha. Naomba serikali ya kaunti na ile ya kitaifa inisaidie kumlipia karo kwa sababu nang’ang’ana kukithi mahitaji ya watoto wangu wengine,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Majambazi walivamia nyumbani wakanibaka nikapata ujauzito,...

Israeli na Hamas wabadilishana wafungwa na waliokuwa...

T L