• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
BAHARI YA MAPENZI: Je, inafaa kutegemea watoto uzeeni?

BAHARI YA MAPENZI: Je, inafaa kutegemea watoto uzeeni?

SIZARINA HAMISI Na BENSON MATHEKA

WANASEMA ujana ni maji ya moto na fainali ni uzeeni.

Mzunguko wa maisha huwa na awamu na ile ya mwisho huwa ni uzeeni.

Pale umri wako unaposonga, umri wa wazazi pia huelekea machweo. Na ukweli ni kwamba kwa jinsi moja ama nyingine wazazi watahitaji uwepo wako kihali ama kimali, kama vile ambavyo hapo awali tulihitaji vitu hivyo kutoka kwao.

Swali ambalo limekuwa likiulizwa na wengi ni je, ni jukumu la watoto kuwaangalia wazazi katika umri wa uzeeni?

Ukweli ni kwamba uhusiano baina ya wazazi na watoto huwa una changamoto zake, wakati mwingine watoto wanakuwa wamebeba machungu ya matukio ambayo walitendewa ama yalitokea wakati wa utoto ama wakati wanapokua.

Wakati mwingine maisha ya watoto pia yanaweza kuwa na changamoto zake, hasa iwapo yanahusisha malezi ya watoto, kazi, marafiki, ndugu na jamaa na hata afya pia.

Je katika hali hii jukumu kwa wazazi linakuwaje?

Kawaida watoto wanapokua huwa na mahusiano mchanganyiko na wazazi na hisia tofauti kuhusiana na kuwahudumia hapo baadae wanapokuwa wanawahitaji kihali ama pia kimali.

Hata hivyo pamoja na tofauti zilizopo na historia binafsi, watoto wanalo jukumu la kuhakikisha wazazi wako salama na wanawapa huduma na mahitaji muhimu.

Wanapofika uzeeni, wazazi wengi hukabiliwa na upweke, kwani watoto wote wameshakua na huenda wametoka nyumbani na kwenda kuishi maisha yao.

Halikadhalika kuna magonjwa ya uzeeni na wakati mwingine changamoto za kushindwa kutembea vizuri ama kushindwa kabisa kutembea na hivyo kulazimika kuwepo nyumbani kwa muda mrefu.

Ndiposa katika umri huu, wazazi wanahitaji zaidi ukaribu wa watoto wao. Pia wakati huu wanaweza kuwa wanashuhudia marafiki zao wakiaga dunia na wengine wakiwa katika hali ya kutojiweza zaidi. Uhitaji huu unaweza usiwe wa pesa pekee, bali kuwepo kwako katika maisha yao, badala ya kuwatupa na kuwasahau kabisa.

Huduma kwa wazazi wazee linatakiwa liwe ni jambo la kipaumbele kwa watoto.

Hata pale wanapoajiri mhudumu ama pale anapokuwepo mashambani, bado wanahitaji uwepo wa watoto wao na hata wajukuu.

Kuna mambo ya msingi ambayo huna budi kutathmini linapokuja suala la wazazi walio katika umri wa uzeeni, hata iwapo una shughuli nyingi ama pia hauna uwezo kifedha wa kuwahudumia katika mahitaji yao mengine.

Katika hili, wapo pia wazazi ambao wanakuwa ni wakorofi pale wanapofikia uzeeni, wanakuwa ni wenye mahitaji makubwa, walalamikaji na wakati mwingine wasioridhika.

Hata katika hali hii, huna sababu ya kuwatelekeza, bali kuelewa kwamba umri unakuja na mambo mengi zikiwemo changamoto za kuwa na uhitaji wa ziada.

Kumbuka kwamba wazazi wanakuhitaji zaidi katika siku zao za machweo na unalo jukumu la kuwa karibu nao katika kipindi hiki. Iwe katika hali ama katika kutimiza mahitaji yao mengine.

[email protected]

JAMII nyingi za Kiafrika zinaamini kwamba kuna baraka katika kutunza wazazi wanapokuwa wazee.

Imani hii imekitwa katika ukweli kwamba kama sio wazazi mtu hawezi kuwa katika ulimwengu huu.

Kama wazazi wangepuuza mtu akiwa mtoto, hangekua na kuwa mtu mzima.

Kama wazazi hawangewajibika kwa malezi na kulipia mtu karo, hangekuwa na kazi au mali. Hivyo basi, mtu yeyote anayepuuza wazazi wake akiwa na uwezo wa kuwasaidia huwa anaalika laana.

Inasikitisha kuona mtu akipuuza mzazi akiwa mgonjwa ilhali ni mzazi huyo aliyekuwa akimpeleka hospitali alipougua akiwa mtoto.

Ni masikitiko kuona mtu akiacha wazazi wake kuteseka na njaa ilhali walifanya kazi kusudi wahakikishe amepata chakula alipokuwa mtoto mdogo.

Nimeona watu wanaoishi katika nyumba za kifahari huku wazazi wao wakiishi katika mazingira ya kusikitisha ilhali walitumia nguvu zao kuwalea na kuwasomesha hadi wakafaulu maishani.

Katika kisa kimoja cha kuatua moyo, nilishuhudia mtu akikosa kumbeba baba yake mgonjwa kwa gari lake na kuacha abebwe na pikipiki hadi hospitalini. Tabia kama hizi ndizo huwa zinaalika laana kwa watu wanakosa kufurahia mali wanayotafuta.

Mzazi huwa anatumia pesa na nguvu zake kwa watoto wake ili waweze kuwa na maisha bora nao wanafaa kufurahia uwekezaji huu wanapoishiwa na nguvu kwa sababu ya uzee.

Kuna wanaotumia chochote wanachopata kwa watoto wao kisha watoto hao wanawatelekeza wanapopata mali. Hii ni laana ya moja kwa moja.

Ninaamini kuwa ni haki ya mtu kumtunza mzazi wake uzeeni jinsi alivyotunzwa akiwa mtoto. Ajabu ni kwamba baadhi ya watu huwa wanawania mali ya wazazi wanaowapuuza uzeeni.

Visa vimeripotiwa vya watu kupigania mali ya wazazi wao ambao huenda wanafariki kwa kutelekezwa. Ninaamini kwamba ikiwa mtu hawezi kuwekeza katika kutunza mzazi wake akiwa mzee, basi hana haki ya kudai urithi. Hii ndio sababu wazee wengi huwa wanauza mali ambayo wangeachia wanao ili waweze kujitunza.

Ikiwa mzazi alitumia nguvu na mali yake kwa malezi ya wanawe hakuna kinachomzuia kuwategemea katika maisha ya uzeeni. Inasemwa kuwa baraka huwa zinarithishwa na mtu akikosa kuwatunza wazazi wake wakiwa wazee, hafai kutarajia atunzwe na wanawe akiwa mzee. Mtu akipuuza mzazi wake, anatarajia atatunzwa na nani?

Narudia kuwa ni haki ya mzazi kutegemea mwanawe uzeeni na ni haki ya mtu kumtunza mzazi wakati huu bila kuuliza swali lolote.

Ikiwa kuna aliye na sababu ya kutosha kumpuuza akiwa na uwezo wa kumsaidia, basi ningemtaka afute ukweli kwamba ni mzazi huyo aliyemleta katika ulimwengu huu.

Ningemtaka mtu kama huyo atangaze kwamba hakuzaliwa na kwamba hataishiwa na nguvu uzeeni kama wazazi wake na kwamba hatahitaji kutegemea watoto wake.

[email protected]

You can share this post!

UJAUZITO NA UZAZI: Mzio wa chakula kwa mtoto mchanga

Uamuzi unaotarajiwa kutolewa kesho utahusisha masuala tisa

T L