• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
BAHARI YA MAPENZI: Kuboresha uhusiano baada ya ugomvi

BAHARI YA MAPENZI: Kuboresha uhusiano baada ya ugomvi

SIZARINA HAMISI Na BENSON MATHEKA

KUGOMBANA ni jambo ambalo halikwepeki katika uhusiano wa kimapenzi.

Upo ugomvi ambao ni wa kawaida na huisha kirahisi lakini upo ugomvi ambao huwa mkubwa na kama ukitokea na ukashindwa kujua nini cha kufanya kuweka mambo sawa, husababisha ufa kwenye penzi lenu.

Baada ya ugomvi mara nyingi uhusiano huyumba, huwa na dosari na zinahitajika juhudi za ziada kuweza kurudisha maelewano na upendo baina yenu. Mara nyingi baada ya ugomvi, kurudisha tena maelewano, mazungumzo na ukaribu na mwenzako ni jambo ambalo sio rahisi. Kwani hisia huwa zimejeruhiwa na wakati mwingine ule mvuto kwa mwenzako umesambaratishwa.

Hivyo ili kuweza kurudisha tena uhusiano ni vyema kuelewa jinsi na hatua za kurudisha ukaribu baina yenu. Hatua ya kwanza na muhimu ni kutambua hali yako kabla ya kujaribu kuwasiliana tena na mwenzako baada ya ugomvi. Ni vyema uwe umetulia kimawazo na kiakili, bila hasira wala jazba.

Iwapo unaona kwamba hautaweza kuzungumza na mwenzako bila kupandisha hasira, kufoka ama kulaumu, jipatie muda hadi pale utakapoona hasira zimepungua. Kwani unapozungumza ukiwa bado na hasira, unaweza kuharibu zaidi badala ya kutengeneza.

Hatimaye unapoona kwamba unaweza kuzungumza bila kufoka ama kupandisha jazba, uwasilishe azma yako ya mazungumzo kwa mwenzako na ni vyema umpatie nafasi kwanza azungumze, aeleze yaliyo moyoni mwake. Hii itakupa nafasi ya kutathmini yaliyomo katika mawazo yao na pia kukupatia nafasi ya kuangalia mvutano wenu katika mtizamo mwingine.

Ukipata kuelewa mtizamo wa mwenzako, jitathmini pia hisia zako. Unajisikiaje, umechangiaje kwenye ugomvi wenu, aliyozungumza mwenzako yamechangiaje kuongeza uchungu ama hasira na kuathiri hisia zako kwake.

Kabla ya kumweleza mwenzako yale yaliyokukwaza kwake, jitathmini na kuwa tayari kubadilisha yale ambayo yalimkwaza. Hatua hii ni muhimu kwani ni vigumu kubadilisha mtizamo na fikra za mtu mwingine lakini inawezekana kufanya hivyo kwako.

Ukishaweza kusuluhisha hisia zako, ni vyema pia kumweleza mwenzako yale ambayo amekukwaza, maelezo haya yasiwe na lengo la kulaumu bali kupata suluhisho. Mazungumzo haya yalenge kumtaarifu mwenzako vitendo ama maneno ambayo ametenda ama kuzungumza ambavyo vimejeruhi hisia zako.

Hata hivyo, usitarajie kwa kumueleza kwamba atabadilika mara moja. Mabadiliko huwa ni hatua. Kumaliza ugomvi ni safari ambayo inahitaji wahusika wote kuwa tayari kuleta suluhu. Kurudisha uhusiano baada ya ugomvi kunaanza kwa kumwelewa mwenzako na kukubali kwamba mmetofautiana katika mambo mengi na kwamba ugomvi ni sehemu ya uhusiano.

Unapoyaweka haya akilini, unahitaji pia kujua kwamba ili kurudisha uhusiano, huna budi kuwa tayari kwa hilo na inahitajika uvumilivu na uelewa kuweza kuleta maelewano tena baada ya kutofautiana. Mshirikishe mwenzako katika kila hatua ya kurudisha tena uhusiano na hata pale mnapokwama ama kujikuta mnatenda ama kusema yale ambayo yalileta ugomvi baina yenu ama kuchangia kufanya hivyo, muwe tayari kurudi tena kwenye tathmini.

[email protected]

NDOA sio paradiso, japo ni matumaini ya kila mtu kuishi kwa furaha na mwenzi wake baada ya harusi. Kuna nyakati ambazo wanaopendana huwa wanatofautiana na hata kugombana vikali. Hii ni kawaida na haimaanishi kuwa mnapotofautiana na kugombana mnafaa kununiana au kuachana.

Wanaofanya hivi hawawezi kudumu kwa ndoa sawa na wanaoamini kuwa maisha ya ndoa ni tambarare. La hasha! Ndoa ni safari inayopitia milima na mabonde na vichaka vyenye miba inayoweza kukudunga na kufifisha matumaini yako

Ugomvi katika ndoa unaweza kutokana na tofauti zinazosababishwa na mambo mbalimbali. Inafaa kufahamika kuwa wanandoa huwa wametoka familia na desturi tofauti ambazo wakati mwingine huwa zinazua mkinzano wa maoni na hata tabia.

Kwa kufahamu haya basi, wanandoa wanaweza kutatua tofauti zao zinapozuka na kusonga mbele na maisha yao pasipo kupigana na kuachana. Hapa inahitaji mtu anayekosea mwenziwe kuwa mwepesi wa kuomba msamaha na anayekosewa pia kuwa mwepesi wa kusamehe.

Msamaha kati ya wanandoa unafaa kuwa wa dhati. Imethibitishwa kuwa msamaha ni tiba ya sumu inayoangamiza ndoa inayoitwa ugomvi. Waliodumu kwa ndoa kwa miaka mingi wanajua kwamba hawangefika walipo isingalikuwa kukumbatia msamaha kwa dhati.

Ikiwa Maandiko Matakatifu yanasisitiza umuhimu wa msamaha katika maisha ya mwanadamu sembuse katika ndoa ambayo ni taasisi ya kwanza kuundwa na Mungu.

Makosa ambayo wengi hufanya ni kukumbusha wenzao makosa waliyowatendea hata baada ya kuomba msamaha na kuyaepuka. Yazike katika kaburi la sahau!

Hata hivyo, mkosaji hafai kuwa na mazoea au kukosea mwenzake makusudi eti kwa kuwa atasamehewa. Mazoea kama haya ni sawa na kudharau mke au mumeo na anaweza kuchoka.

Kuna watu wanaopenda kutangazia marafiki na jamaa zao wanapotofautiana na wenzao, hatua ambayo inavuruga zaidi ndoa zao kutokana na mchanganyiko wa ushauri wanaopata. Ugomvi wa kawaida kati ya mtu na mkewe sio suala la kuanika kwa marafiki na wanaofanya hivi huwa wamekosa ukomavu.

Huenda nikaeleweka visivyo hapa lakini ninachoamini ni kuwa wanandoa waliokomaa wana uwezo wa kusuluhisha masuala madogo madogo bila kuyaweka kandamnasi. Inawezekana wanandoa kusuluhisha tofauti zao wenyewe ila kile ambacho watu wanafanya ni kukubali kuongozwa na hasira na hii inawafanya kuongeza msumari moto juu ya donda ndugu. Hasira, daima ni hasara.

Watu wanapaswa kukumbushana walipoanzia kwa kuwa sidhani kuna mtu na mke walioona wakiwa wamenuniana. Kukumbushana huku kunafufua hisia zilizowaunganisha na kwa kawaida, hisia hizi huwa na nguvu za kuwafanya kusahau kilichowafanya wagombane.

Ukweli usiopingika na ambao wengi hupuuza ni kwamba upendo huwa unafunika wingi wa makosa. Hapa nataka nirudie kuwa hiki hakifai kuwa kisingizio cha mtu kurudia makosa eti kwa sababu mke au mumewe anampenda sana. Huu ni ufala!

[email protected]

You can share this post!

PENZI LA KIJANJA: Kuepuka uvundo wa upweke!

Wanawake Garissa walalamika kunyanyaswa kisiasa kupitia...

T L