• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Betty Njeri: Mkome kutembea na pini za kutia pancha penzi letu

Betty Njeri: Mkome kutembea na pini za kutia pancha penzi letu

NA MWANGI MUIRURI

MBUNGE Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Murang’a Bi Betty Njeri Maina amesema Ijumaa, Septemba 1, 2023, kwamba baadhi ya wanaume, wakiwemo wanahabari wa kiume, wanamwinda kimahaba na akiwakataa, wanamsema vibaya na hata kumchafulia jina.

Akiongea katika kaunti ndogo ya Kandara katika hafla ya kusajili wanyonge katika mpango wa kuwapa kiinua mgongo kutoka kwa hazina ya serikali, Bi Maina amedai kwamba wanaume hao pia hudai hongo za Sh100,000 kutoka kwake.

“Niko na pesa nyingi na ninazitumia jinsi nitakavyo na sitazitumia kuwapa wanaume,” amesema.

Alisema kwamba yeye yuko kwa ndoa akifurahia maisha na mbunge wa Mathira Bw Eric wa Mumbi.

Mathira iko Kaunti ya Nyeri.

“Mimi nimeolewa na mume wangu ni mbunge wa Mathira anakotoka Naibu Rais Rigathi Gachagua. Nyinyi watu wa Murang’a mnafaa mmakinike sana kwa kuwa baadhi ya waandishi hawa sio wa huku kwenu na hawataki mpate maendeleo,” akadai.

Amesema kwamba atazidi kujenga na kuimarisha ndoa hiyo yake, akiwataka wasio na washikaji wakome wivu.

Bi Maina ameongeza kwamba yeye hahitaji vyombo vya habari ili kuafikia malengo yake ya kisiasa.

Tangu achaguliwe Agosti 9, 2022 , Bi Maina amekuwa katika vita vya maneno na viongozi wenzake akiwemo Waziri wa Maji Bi Alice Wahome, Spika wa Kaunti ya Murang’a Bw Johnson Mukuha, na Kiranja wa wengi wa bunge la Murang’a Bw Kibe Wasary.

Wengine ambao amevuruga kwa maneno ni wanasiasa wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambacho ni cha Rais William Ruto, akiwasuta kwa kumshambulia Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, mtangulizi wake katika cheo hicho cha Kaunti Bi Sabina Chege na sasa, vyombo vya habari.

Aidha, amekuwa mshambulizi sugu wa uwiano wa kitaifa ambapo husuta kikatili mrengo wa Azimio la Umoja One Kenya Coalition na viongozi wake wakiongozwa na kinara wao, Raila Odinga.

  • Tags

You can share this post!

Pasipoti: Kindiki aendelea kuvunja makateli wa Nyayo House

Ruto kurejea tena kunyonga ‘payslips’ za Wakenya

T L