• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Ruto kurejea tena kunyonga ‘payslips’ za Wakenya

Ruto kurejea tena kunyonga ‘payslips’ za Wakenya

CECIL ODONGO na CHARLES WASONGA

SERIKALI ya Rais William Ruto inaonekana kuendelea kuwakaba koo Wakenya kwa kuwaongezea mzigo wa ushuru na kukata mapato yao, ili kufanikisha utekelezaji wa miradi na mipango yake.

Kando na ushuru wa nyumba wa asilimia 1.5 ya mshahara wa jumla wa wafanyakazi wote ulioanza kutekelezwa Julai 1, serikali pia inapanga kukata asilimia nyingine 2.75 kuelekezwa kwa hazina mpya ya bima ya afya ya kijamii.

Hii ina maana kuwa Wakenya wanaopokea mishahara ya Sh50,000 kwenda juu watakatwa asilimia 20 ya mishahara yao (ukijumlisha kodi zote ikiwemo PAYE) kufadhili mipango hiyo miwili ya serikali ya Kenya Kwanza.
Hazina hiyo mpya itaanzishwa baada ya Mswada wa Bima ya Afya ya Kijamii ya 2023 kujadiliwa na kupitishwa katika bunge la Kitaifa na lile la Seneti.

Kulingana na mswada huo ambao umepitishwa katika baraza la mawaziri, itakuwa ni lazima kwa kila Mkenya kuchangia hazina hiyo mpya inayolenga kufanikisha ajenda ya serikali ya Afya Kwa Wote (UHC).

Hii ina maana raia wote watachangia hazina hiyo mpya ya matibabu bila kujali viwango vyao vya mapato.

Kwenye mabadiliko haya mapya, serikali itatokomeza Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) ambayo imedumu tangu 1968.

Kulingana na Mswada huo ambao utawasilishwa bungeni kuanzia Septemba 25, makato ya asilimia 2.75 yanamaanisha kuwa mchango wao kwa hazina hiyo mpya utapanda kutoka Sh500 hadi Sh1,700 kila mwezi.

Kwa kuwa tayari wafanyakazi wanakatwa asilimia 1.5 ya mishahara yao kama ushuru wa nyumba na kodi zingine, hii ina maana kuwa anayepokea mshahara wa Sh50,000 atapoteza Sh10,000 kwa mipango ya serikali.

Na mfanyakazi anayepokea Sh100,000 kwa mwezi atapoteza jumla ya Sh27,389 kwa mipango hiyo vilevile.

Aidha, mfanyakazi kama huyo atakatwa Sh2,000 za kuelekezwa kwa Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF). Serikali ya Rais Ruto iliongeza mchango wa hazina hii kutoka Sh200 miezi michache baada ya yeye kuingia mamlakani mnamo Septemba 13, 2022.

Hii ina maana kuwa makato haya yatasababisha wafanyakazi waende nyumbani na pesa kidogo zaidi kuliko hali ilivyokuwa zamani chini ya tawala za marais watangulizi wa Dkt Ruto.

“Pesa za hazina mpya ya afya ya jamii zitakuwa zikisimamiwa na bodi moja na sekretariati kulingana na makato kutoka kwa familia ambazo zimeajiriwa na wale ambao wanafanya katika sekta mbalimbali za kibinafsi,” akasema Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed.

Msemaji huyo aliongeza kuwa pesa zinazotokana na makato hayo zitatumika kuhakikisha kuwa serikali inatimiza ahadi iliyotoa wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 wa kuwawezesha Wakenya wote kupata huduma za afya kwa gharama nafuu.

Aidha, Mohamed alisema kuwa Mswada wa Huduma za Afya katika Kiwango cha Chini 2023 unapendekeza mabadiliko katika utoaji wa huduma za afya ambapo yataanzia katika ngazi za vijiji kuelekea juu.

“Inatoa mwongozo ambapo wahudumu 100,000 ya afya ya jamii wataajiriwa, alivyoahidi Rais Ruto. Watakuwa wakitembelea familia manyumbani mwaka na kuwapa huduma za afya za kimsingi,”akasema Bw Mohamed.

  • Tags

You can share this post!

Betty Njeri: Mkome kutembea na pini za kutia pancha penzi...

Shakira, aliyeachwa na Pique, atemana na nguli wa magari...

T L