• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Fahamu tamaduni za jamii ya Wanubi

Fahamu tamaduni za jamii ya Wanubi

NA FARHIYA HUSSEIN

KATIKA eneo la Changamwe, Kaunti ya Mombasa, sauti zinasikika za watu wakipiga vigelegele, makofi na kuimba nyimbo za sifa.

“Tausi huyo, ndege wa angani, tausi ni ndege, mwenye pambo na manyoa,” sauti za wanawake zinasikika kwa umbali.

“Mna bahati kushuhudia mojawapo ya harusi za Wanubi,” Bi Halima Abdulrahman akasema mapema Agosti 2023 alipokuwa akimtayarisha bintiye, ambaye siku ya kuolewa ilikuwa imekaribia.

Anasema katika mila za Wanubi, ‘bei’ ya bibi arusi haikuwa ikipita Sh200 siku za nyuma.

Ingawa hivyo, kulikuwa na utaratibu maalum wa kupata vitu kama kitanda na fanicha za kutumika na waliooana. Pia namna ya kupata vyombo kama sahani, vikombe na mwiko huwa imewekwa wazi.

Lakini haya yamebadilika ikilinganishwa na arusi nyingi za siku hizi.

“Bibi-arusi ndiye anayechagua kitakacholipwa kwa mahari, kama inavyotajwa katika sheria na desturi za dini ya Kiislamu,” Bi Abdulrahman asema.

Bi Abdulrahman anaeleza kuwa ili bwana arusi akubaliwe, familia yake huandika barua kwa upande wa bibi arusi kueleza kwa kina ombi lao la ndoa.

Ikiwa pendekezo la ndoa limekubaliwa, basi baba ya bibi arusi hupokea mahari kutoka kwa familia ya bwana arusi na kuamua jinsi ya kuigawa ndani ya familia yake.

Najua utashangaa jinsi Sh200 zitakavyogawanywa, lakini ukweli ni kwamba akina baba wanajua zaidi.

“Siku zote tunapendelea ndoa za Wanubi kwa Wanubi kutokana na kuelewa zaidi kwa tamaduni,” anaongeza.

Katika mila ya Wanubi, arusi huchukua takriban siku tatu. Katika siku ya kwanza, mahari, inayojulikana kwa jina Sela, hulipwa. Siku ya pili ni mahususi kwa ajili ya majadiliano baina ya familia hizo mbili pasipokuwapo bibi na bwana arusi, na siku ya mwisho ni pale bwana arusi anapopambwa kwa pambo liitwalo Derira lililotengenezwa kwa manyoya ya wanyama kama ngamia na kondoo na kucha za ndege kama mwewe.

Binti ya Bi Abdulrahman alikuwa na bahati kwani bwana arusi mtarajiwa wakati huo alikubaliwa katika familia na maandalizi ya arusi yalikuwa tayari yameanza.

Kulingana na utamaduni wao, gauni, viatu, na vito vya kumpamba bibi arusi hununuliwa na bwana arusi mwenyewe.

“Tayari tumeanza maandalizi ya arusi. Tunasubiri bwana arusi alete gauni la arusi lijulikanalo kwa jina la Gurbaba, khanga na shanga zitakazovaliwa na mkewe,” alieleza Bi Abdulrahman.

Gurbaba ni kitambaa kikubwa cha rangi za kuvutia na hujumuisha pia sketi iliyovaliwa chini ya mavazi.

Gurbaba, zamani likichukuliwa ni vazi la kawaida la kila siku, hutumika tu katika hafla maalum, kama vile arusi na Dholukas (ngoma za Wanubi pale ngoma ndio pekee inachezwa). Wakati wanawake wote wa Nubi wanajitokeza wakiwa wamevaa Gurbaba , wanaume huvalia Kanzu,” Bi Abdulrahman asema.

Upande wa bwana arusi pia hupata afueni kwani vyombo, kitanda, na samani nyingine zitakazotumiwa na waliooana hununuliwa na familia ya bibi arusi.

“Hata ikiwa bwana arusi ni tajiri, haruhusiwi kununua kwa mara ya kwanza kitanda na vyombo vya kutumika katika nyumba yao mpya,” Bi Abdulrahman asema, akiongeza kuwa nyumba zote ambazo bwana arusi alikuwa nazo kabla ya kumuoa bintiye zitarudishwa kwa familia yake na kama ni nyumba ya kukodisha, basi itabidi wagure waende katika nyumba nyingine.

Katika dakika kumi, Bi Abdulrahman alikuwa amemaliza kuchora hina kwenye mguu wa bintiye.

Bi Aisha Hassan alipofanya arusi ya kitamaduni ya Wanubi. Pamoja naye ni familia yake na ya bwana arusi. PICHA | FARHIYA HUSSEIN

Wanubi asili yao ni kutoka kaskazini mwa Sudan na kusini mwa Misri (jangwa la Nubian), ambapo walikaa kando ya kingo za Mto Nile.

Sasa wanaweza kupatikana wametawanyika kote Afrika Mashariki na baadhi ya maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa Afrika.

Wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, walisaidia kupanua himaya ya Mkoloni Mwingereza.

Kama zawadi kwa utumishi wao wa uaminifu, Waingereza waliwaweka maveterani wa Nubi katika msitu karibu na Nairobi, ambao waliuita Kibr. Walikuja Kenya kama wanajeshi, na Waingereza wakawapa makazi huko Kibera (Kibr), ambayo ina maana ya msitu katika lugha ya Nubi. Hapo walijenga nyumba kwa kutumia udongo na miti.

Kulingana na Bi Abdulrahman, ambaye alizaliwa na akalelewa kwa tamaduni za Wanubi, akina babu wao walikuwa madereva baada ya vita kuisha, na akina nyanya wao waliuza zaidi pombe ya kitamaduni, gin ya Wanubi, ambayo sasa inajulikana kama chang’aa.

Wanubi wamegawanywa katika koo kadhaa, ambazo ni pamoja na Dinka, Muru, Kotoria, Bari, Kuku, na Lendu.

Walendu hasa asili yao ni kutoka Kongo, wakati wengine wanapatikana katika maeneo kama Majengo, Mombasa, na Kibera jijini Nairobi.

Wakati wa arusi yao, kamba inafungwa kwenye kiuno cha bibi arusi, na bwana arusi hufungua kamba. Kitendo cha kufungua kamba kinaashiria kwamba mwanamke sasa ni mke.

“Pia bwana arusi anampapasa mke mara saba kichwani. Hili ni fundisho kwake kwamba mgogoro unatakiwa kusuluhishwa kwa amani na mwanamke asipigwe fimbo wala bomba,” akaeleza mama wa mtoto huyo ambaye bintiye ni bibi arusi.

Wana salamu za kipekee zinazoashiria mila zao na kuhakikisha zinapitishwa kutoka kizazi hadi kizazi.

Kila kijana anapowasalimia wazee wao, anakumbatia mikono yao, kisha anaiweka kwenye kidevu kisha paji la uso, kuashiria heshima.

Watu wazima wanaruhusiwa kumwadhibu mtoto yeyote aliyekosa nidhamu. Haijalishi mtoto ni wa nani.

Chakula chao kikuu ni Kisra, mlo unaotengenezwa kwa unga wa mahindi yaliyochachushwa na ngano iliyochanganywa na unga wa simsim, ambao bado unapatikana kwenye menyu yao.

Pia, hufurahia Gurusa, toleo lao la Anjera ya Ethiopia.

Nyingine ni Gurusa din ambayo huangazia hasa katika kifungua kinywa chao. Inajumuisha mchele uliovunjwa kupikwa kama Anjera (inayojulikana na wengi kama mkate wa maji).

Chakula kikuu huliwa pamoja na kitoweo kinachojulikana kama mchuzi wa kuftah, ambacho hujumuisha kima, yaani nyama iliyosagwa.

Miaka iliposonga, walianza kula pilau na nyama ya ng’ombe kama sehemu ya vyakula vyao vikuu.

Bi Abdulrahman anaeleza kuwa ikitokea kwamba Mnubi anaoa wake wengi , basi anachukuliwa kuwa ni tajiri.

Wakati wa jioni, bi arusi lazima apeleke sahani maalum, iliyotiwa Kisra au Gurusa, kwa bwana arusi, chakula ambacho huwa kimepikwa kutoka nyumbani kwao.

  • Tags

You can share this post!

Wanaoishi na HIV kupata dawa za kupunguza makali kwa bei...

Kijiji ambapo wazee huchapwa viboko kwa ‘utovu wa...

T L