• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Kijiji ambapo wazee huchapwa viboko kwa ‘utovu wa nidhamu’

Kijiji ambapo wazee huchapwa viboko kwa ‘utovu wa nidhamu’

NA LUCY MKANYIKA

POLISI katika kaunti ndogo ya Voi, Kaunti ya Taita Taveta, wanachunguza visa vya watu wazima kuchapwa viboko na wanakamati ya usalama wa jamii, kila wanapodaiwa kupotoka kinidhamu.

Kisa cha hivi majuzi ambacho kimeibua malalamishi kutoka kwa baadhi ya wakazi na mashirika ya kutetea haki za binadamu, ni kichapo cha kaka wawili waliokuwa wakipigana sokoni wakiwa walevi.

Wawili hao, Bw Collins Maza, 40, na Bw Joseph Kinywa, walipigana katika soko la Wongonyi kufuatia ugomvi kuhusu kwa nini Kinywa alichelewa kurudisha betri ya simu ya Maza.

Vita vyao vilivutia wanakijiji ambao waliita wanachama wa kamati ya usalama wa jamii. Badala ya wanachama watatu waliowasili kuwapatanisha, waliamua kuwacharaza kila mmoja viboko 30 mgongoni, miguuni na kwenye makalio.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Voi, Bw Banastein Shari, alisema uchunguzi umeanzishwa kwani si haki kuchapa watu, na waliohusika kuwapiga wawili hao watashtakiwa.

“Hata polisi hawakubaliwi kutumia nguvu wanapochukulia raia hatua,” akasema Bw Shari.

Imebainika kuwa, kisa hicho kilichotokea wiki iliyopita kilikuwa cha tatu kushuhudiwa katika siku za hivi majuzi.

Kulingana na wakazi, kamati hiyo imekuwa ikiwachapa wanakijiji wanaodaiwa kuvunja sheria mara kwa mara.

Akieleza waliyoyapitia, Bw Maza alisema kakake mdogo alikuwa amekataa kurudisha betri yake ambayo alikuwa ameomba mapema siku hiyo.

“Sote wawili tulikuwa tumelewa wakati tulipoanza kupigana lakini mjomba wetu aliingilia kati akatutenganisha. Dakika chache baadaye, tuliitwa na wanakundi la usalama wa kijamii katika ukumbi ambapo tulichapwa viboko,” akasema.

Video iliyoenezwa mitandaoni iliwaonyesha wawili hao wakilia kwa uchungu huku wakiendelea kuchapwa.
Kila mmoja aliyewachapa aliwapa viboko kumi. Bw Kinywa alisema walichapwa kwa karibu dakika 15 kisha wakapewa onyo wasiwahi tena kupigana na waheshimiane.

Wawili hao ambao bado wanauguza majeraha nyumbani, walisema huwa ni marafiki na walipigana tu kwa hasira.

“Ninamheshimu ndugu yangu mkubwa na najutia sana kisa hiki. Hata hivyo, nakashifu hatua za wanaume hao watatu na natumai tutapata haki,” akasema Bw Kinywa.

Mwenyekiti wa shirika la Taita Taveta Civil Society Organisations Network, Bw Ezra Mdamu, alisema kazi ya kamati hiyo huwa inafaa kuwa ni kuwaleta pamoja polisi na raia ili kudumisha usalama wala haina mamlaka ya kuwaadhibu raia.

“Hatua hizo zinakiuka sheria na heshima ya wananchi. Kikundi cha usalama wa kijamii kilitumia vibaya mamlaka yake na kukiuka haki za kibinadamu kwa kuwachapa kaka hao wawili,” akasema.

Kamati hizo huwa zimebuniwa chini ya Sheria ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (2011) ili kuweka nafasi ya mazungumzo na ushirikiano kati ya polisi na jamii kuhusu masuala ya kiusalama.

  • Tags

You can share this post!

Fahamu tamaduni za jamii ya Wanubi

Mwanamume afariki baada ya kuanguka kwa shimo la kina cha...

T L