• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 7:05 PM
Wanaoishi na HIV kupata dawa za kupunguza makali kwa bei nafuu

Wanaoishi na HIV kupata dawa za kupunguza makali kwa bei nafuu

NA MARY WANGARI

MAMILIONI ya watu wanaougua Ukimwi huenda wakapata afueni kuu kufuatia mkataba mpya utakaowezesha wagonjwa kupokea matibabu bora ya kisasa kwa bei nafuu zaidi.

Wagonjwa sasa wataweza kupata dawa zenye nguvu zaidi ya kupunguza makali ya virusi vya HIV zinazofahamika kama TLD kwa takriban Sh6,543 pekee kila mwaka, shirika la Global Fund lilitangaza kupitia taarifa Jumatano.

Hatua ya kupunguza bei ya tembe hizo kwa asilimia 25 inayotazamiwa kuokoa maisha ya mamilioni ilifanikishwa kupitia mkataba baina ya Global Fund na kampuni zinazounda dawa.

Global Fund ni shirika la kimataifa linalojishughulisha na ufadhili ambalo lilibuniwa mnamo 2002 kwa lengo la kukabiliana na maradhi ya malaria, kifua kikuu na ukimwi.

“Hatua ya kupunguza bei ya dawa hizo itawezesha serikali katika mataifa maskini kupanua usambazaji wa huduma muhimu za matibabu ya HIV,” ilisema Global Fund kupitia taarifa.

TLD ni tembe inayojumuisha viungo vitatu vya kukabiliana na virusi ambavyo ni pamoja na tenofovir disoproxil, lamivudine na dolutegravir.

Dawa hii iliidhinishwa 2019 na Shirika la Afya Duniani (WHO) kama matibabu ya kisasa bora zaidi kwa wanajamii wote ikiwemo wanawake wajawazito na wale wenye uwezo wa kupata watoto.

Kando na kuwa na athari chache, TLD ni rahisi kutumiwa na wagonjwa huku ikiwa na nguvu zaidi za kupiga vita HIV.

Mkuu wa Global Fund Peter Sands alielezea wasiwasi kuhusu “mamilioni ya watu wanaougua HIV ambao hadi sasa hawana uwezo wa kupata matibabu bora hasa katika nchi maskini zenye kiwango cha juu cha maambukizi ya gonjwa hilo.”

“Hatua ya kupunguza bei ya TLD inamaanisha serikali na wahisani wengine wanaoshirikiana na GF sasa wanaweza kudhibiti maambukizi mapya na kuokoa maisha kwa kuwekeza zaidi katika mikakati ya kuzuia na kupanua mipango ya matibabu,” alifafanua Bw Sands.

Mikataba ya utowaji leseni iliyoafikiwa 2017 iliwezesha watu zaidi ya 19 milioni wanaougua HIV katika nchi zinazoendelea kupata TLD kila mmoja kwa hadi Sh10,912.

Kiwango hicho cha bei ambayo haingetarajiwa enzi hizo, kilifanikishwa kupitia ushirikiano baina ya Global Fund na wahisani mbalimbali ikiwemo Wakfu wa

Bill & Melinda Gates na Miradi Jumuishi ya Umoja wa Mataifa kuhusu HIV/ukimwi (UNAIDS).

Hatua ya WHO kupendekeza TLD miaka minne iliyopita ilijiri baada ya ushahidi mpya kuzima hofu kuhusiana na usalama wa kiungo cha dawa ya HIV dolutegravir (DTG).

Utafiti wa mwanzo uliashiria kuwepo uwezekano wa wanawake wajawazito wanaotumia DTG kujifungua watoto wachanga walio na matatizo ya kiafya kwenye ubongo na uti wa mgongo.

Wanawake wanne miongoni mwa 426 waliotungwa mimba walipokuwa wakitumia tembe za DTG waliripotiwa kuwa na matatizo hayo ya kiafya katika matokeo ya utafiti yaliyochapishwa Mei 2018 nchini Botswana.

Kwa mintarafu hiyo, mataifa yalipendekeza tembe za efavirenz (EFV) kutumika kwa matibabu ya HIV badala ya DTG kwa wanawake wajawazito na wale wenye uwezo wa kupata watoto.

Hata hivyo, majaribio mawili ya kina yaliyofanywa na wataalam wa afya kwa lengo la kulinganisha ufaafu na usalama kati ya tembe za DTG na EFV barani Afrika yalipanua upeo wa ushahidi uliokusanywa.

Kinyume na ripoti ya awali, matokeo kwenye utafiti mpya yaliashiria kiwango cha chini cha matatizo ya ubongo na uti wa mgongo kwa watoto wachanga.

Aidha, utafiti ulionyesha DTG kuwa na nguvu zaidi, kiwango cha chini cha athari za kiafya na rahisi kutumika na wagonjwa kuliko dawa mbadala za HIV.

Isitoshe, huku virusi hivyo hatari vikizidi kuwa sugu na kuzidi makali mengineyo, tembe za kisasa zina uwezo asilia wa kijeni unaoshinda nguvu virusi vya Ukimwi.

  • Tags

You can share this post!

Ogina Koko alenga kuwa Rais akiahidi kuondoa Januari kwenye...

Fahamu tamaduni za jamii ya Wanubi

T L