• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Koffi Olomide kutumbuiza nchini akiendelea kusahau masaibu ya 2016 alipofurushwa kwa kupiga mnenguaji

Koffi Olomide kutumbuiza nchini akiendelea kusahau masaibu ya 2016 alipofurushwa kwa kupiga mnenguaji

NA MERCY KOSKEI

MWANAMUZIKI mahiri wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Koffi Olomide anatarajiwa kutumbuiza mashabiki wake nchini mnamo Desemba.

Kupitia mtandao wake ya kijamii Novemba 8, 2023, nguli huyo alifichua mpango huo akisema kuwa anatazamia kupiga shoo kali nchini Kenya, baada ya miaka kadhaa.

Olomide alitoa wito kwa mashabiki wake kujitokeza kwa wingi kwenye hafla
hiyo akiahidi burudani ya kukata na shoka.

“Mopao anakuja Nairobi mnamo Desemba 8, 2023, na Desemba 9, 2023. Kutakuwa moto,
nitarudi Kenya baada ya miaka mingi. Nimewakosa kwa muda mrefu, nataka
kuwaonyesha undani wa mapenzi yangu,” akaandika.

Akaongeza: “Kila mtu, vijana, wanawake kwa wanaume, njooni mjiunge nami katika onyesho la moja kwa moja katika Starehe hizo jijini Nairobi. Mopao anarejea Kenya, ninawapenda.”

Msanii huyu anapendwa sana nchini ingawa tukio la mwaka 2016 nusura liharibu uhusiano huu.

Wakati huo, alinaswa kwenye kamera akimpiga teke mmoja wa wanenguaji wake wa kike katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) na baadaye akafurushwa.

Olomide alikanusha makosa hayo, na kudai kuwa alikuwa akilinda kundi lake dhidi ya mtu ambaye alikuwa anatishia usalama wao.

Miaka minne baadaye, Olomide aliomba msamaha Wakenya na kukiri kwamba
alikosea, na kuishukuru serikali ya Kenya kwa kumkubali tena. Huo ulikuwa mwaka 2020 aliporuhusiwa kutua nchini.

Olomide ni mwanamuziki bora kutokana na ufundi wake na amebaki kuwa mahiri kwa miongo kadhaa sasa.

  • Tags

You can share this post!

Nafikiria kumwambia baba simpendi mke wake wa pili

Jamii Lamu yaahidi kusaidia serikali kutokomeza Al-Shabaab

T L