• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:39 AM
Kundi la Les Wanyika lakutana Garden Square Jumamosi kujikumbusha walikoanzia miaka 45 iliyopita

Kundi la Les Wanyika lakutana Garden Square Jumamosi kujikumbusha walikoanzia miaka 45 iliyopita

NA JOHN ASHIHUNDU

Kundi maarufu la muziki wa dansi la Les Wanyika leo Jumamosi linarejea katika ukumbi wa mkahawa wa Garden Square walikoanzia miaka 45 iliyopita.

Kulingana na kiongozi wa bendi hiyo, Sijali Zuwa mualiko wao ni kutokana na hitaji la umma na mashabiki wao wanaotarajiwa kufurika kwenye mkahawa huo ambao sasa unajulikana kama Garden Square Ashaki Grill.

Zuwa na naibu wake Tommy Malanga ni miongoni mwa wanamuziki wakongwe watakaokuwa jukwaani kuburudisha wateja na mashabiki kwa vibao vyao moto moto.

“Les Wanyika inarejea nyumbani ilikozaliwa mnamo 1978 baada ya baadhi yetu kuagana na Simba Wanyika mnamo 1978. Kwa miaka kadhaa tumekuwa tukifanya maonyesho katika sehemu tofauti nchini Kenya, lakini sasa mashabiki wetu wametuagiza turejee katikati mwa jiji la Nairobi kuwapa uhondo wa kutosheleza,” alisema Zuwa ambaye ni mzaliwa wa Morogoro, Tanzania.

Maonyesho ya Les Wanyika katika mkahawa wa Garden Sqaure Ashaki Grill ni sehemu ya tamasha rasmi zilizoandaliwa kuandama na ufunguzi rasmi wa mkahawa huo wa kifahari ambao imefanyiwa ukarabati wa hali ya juu tangu ufungwe miezi kadhaa iliyopita kwa shughuli hiyo.

Kundi la Les Wanyika wakiwa pamoja. Picha|John Ashihundu

“Natoa mwito kwa mashabiki wetu popote walipo wafike kwa wingi kuburudika kwa miziki yetu halisi kama Afro, Sina Makosa, Pamela, Kujituliza Kasuku, Safari ya Samburu, Amigo, Jessica, Safari Sio Kifo, Dunia Kigeugeu, Mama Watoto, Nimaru miongoni mwa nyingine nyingi,” alisema Zuwa ambaye pia ni mpigaji tarumpeta na keyboard matata.

Les Wanyika iliundwa 1978 baada ya Zuwa, Omari Shaban, Malanga, Rashid Juma na Foni Mkwanyule kujitenga kutoka kwa kundi la Simba Wanyika la ndugu watatu William, George na Wilson Kinyonga waliunda bendi hiyo mnamo 1971 kutoka kwa Arusha Jazz.

Baadaye Les Wanyika ilifanikiwa kusajili Johny Ngereza, Issa Juma, Mohamed Tika Abdallah, Victor Boniface, Joseph Justy Shiayo na Sammy Waingo.

Asilimia kubwa ya wanamuziki wa kundi hili walikuwa Watanzania, huku wengine wakiwa Wakenya hasa kutoka eneo la Pwani ambao walianza nalo miaka 45 iliyopita.

Kwa mara mbili tofauti, bendi ya Les Wanyika ilififia na wanamuziki kutawanyika, mara mwisho ikiwa mnamo 2006, miaka michache baada ya kifo cha Ngereza, lakini Zuwa, Juma, Malanga na Justy wakaungana na kuirejesha mnamo 2010 ambapo hadi sasa imekaa imara.

Wanamuziki wa Les Wanyika walio kikosini kwa sasa ni:

Waimbaji: Rama Kocha, Rajab Kadima and Charles ‘Tabu’ Obala. Wacharazaji magita: Tommy Malanga (basi), Damas Lobanga (solo) and Murhula E.M Moses (rhythm). Wapijaji tarumpeta: Sijali Zuwa, Bernard Kilindo na Olabode Idowu. Drummer: Ado Voyant na Konga: Hassan Ngao.

  • Tags

You can share this post!

Wakenya watakiwa wabonyeze nambari kufuatilia pesa...

Polisi wawili kusotea jela kwa kujaribu kuzuia kukamatwa...

T L