• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Seneta mwenye ulemavu wa macho asisimua kwa kuzindua albamu ya HipHop

Seneta mwenye ulemavu wa macho asisimua kwa kuzindua albamu ya HipHop

NA FRIDAH OKACHI

SENETA maalum Crystal Asige amezindua albamu mpya inayofahamika kama Blinding Allure, yenye nyimbo sita. Albamu hiyo ikiwa ni njia ya kufikia vijana wengi ambao hutangamana naye kwenye shughuli zake za useneta pamoja na kuonyesha ulimwengu anaweza lolote licha ya kuwa na ulemavu wa kuona.

Bi asige anayefahamika kuwa mwimbaji tajika na mwandishi wa nyimbo, aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba nyimbo hizo ni mtindo wa RNB na HipHop ili kubadilisha dhana ya wanaomfuatilia.

Seneta huyo alipoteza uwezo wa kuona akiwa na miaka kumi na miwili, hali hiyo ikimfanya kusalia na sauti anayotumia kwenye kipaji chake.

“Kupoteza uwezo wa kuona kumenifanya nielewe umuhimu wa kusimama pekee yangu. Unaona nikitoka hapa nitatembea polepole hadi nifike niendapo,” alisimulia Bi Asige.

Katika utunzi huo, Bi Asige alisema ni njia ya kujitambulisha. Kila mmoja akiwa na umuhimu wa kufanya jambo bila kujificha kwa wengine.

“Maishani kuna vitu mtu angependa kuonyesha kutoka moyoni. Labda, unakuwa muoga kuonyesha kipaji, kutojiamini una talanta fulani,” alisema Bi Asige.

Kwenye albumu hiyo alikuwa na uoga mashabiki wangemchukulia visivyo kujaribu mbinu nyingine ya uimbaji kando na ile anayojulikana nayo.

“Wengi wananifahamu na mtindo wa Chakacha na Rhumba kwa kuwa mimi ni mzaliwa wa Mombassa. Nataka kubadilisha hiyo dhana na kuwafahamisha kuwa naweza mtindo huu mwingine. Pia, mimi ni mpenzi wa hiphop kwa kuwa nilianza kusikiza nikiwa mdogo hadi nilipoenda kusoma huko Marekani,” alieleza seneta huyo.

Anasema kuzindua albamu hiyo ni kutaka kufahamisha ulimwengu huwezi kufanya jambo moja tu. Alisisitiza kuwa mara ya kwanza kutoa ngoma hakuwa anaamini iwapo mashabiki wake wangemkubali jinsi alivyo.

“Ukionyesha watu kitu tofauti, huenda wakose kukubali. Najitolea nione mashabiki watachukulia vipi. Kuna wale wamepokea vizuri. Kuna wimbo mmoja naimba na mwingine nafoka foka,” alisema Bi Asige.

Mwanamuziki huyo alianza kuimba akiwa na miaka mitatu. Talanta hiyo ni kutokana na kutazama, kusikiza miziki mbalimbali.

“Kila wakati mama hunitia moyo na kuniambia niendelee. Hunikumbasha nilianza kuimba nikiwa na miaka mitatu, alisema kiongozi huyo.

Mwimbaji huyo anajulikana kufanya kazi na kundi la Sauti Sol ambalo tayari lishasambaratika.

Mwaka 2022 aliweza kuteuliwa kuwasilisha vijana, wanawake na walemavu kwenye chama cha ODM.

Alisema nafasi yake ya kuhudumia vijana na walemavu hapa nchini kama seneta huwa na changamoto kama msanii.

“Kuna wakati vitu haviendi sawa, hapa kuna siri nyingi hadi nauliza Mungu mimi kama mwanamuziki nitaweza,” alisema.

“Katika mwaka wa kwanza ripoti iliyotolewa imenipa moyo na kunifanya kuwa na uhakikisho wa kuwakilisha Wakenya jinsi inavyohitajika,” aliongezea Bi Asige.

Novemva 16, 2023, kiongozi huyo alitangamana na watu wanaoishi na ulemavu na kufanya maandamano Kaunti ya Nairobi kulalamikia kudhulumiwa na askari wa kaunti.

  • Tags

You can share this post!

NCPB Mwea yaanza kununua mchele kutoka kwa wakulima...

Mabroka kuendelea kuvuna serikali ikitangaza bei ‘duni’...

T L