• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
NCPB Mwea yaanza kununua mchele kutoka kwa wakulima kufuatia agizo la Ruto

NCPB Mwea yaanza kununua mchele kutoka kwa wakulima kufuatia agizo la Ruto

GEORGE MUNENE na SAMMY WAWERU

MAMIA ya wakulima wa mpunga Mwea, Kirinyaga wana kila sababu ya kutabasamu baada ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) kuanza kununua mazao yao ya mchele.

Hatua hiyo inatokana na agizo la Rais William Ruto, NCPB ianze kununua zao la mche kwa bei nafuu.

Bodi hiyo inanunua kilo moja ya mchele ambao haujaongezwa thamani kwa Sh85, kama alivyoamuru Rais Ruto.

Kulingana na Meneja wa tawi la NCPB Mwea, Joseph Okiru, wakulima walianza kusambazia bodi hiyo mchele mnamo Jumanne, Novemba 21, 2023.

“Tumeanza kupokea mchele kutoka kwa wakulima na tunawalipa mara moja,” Bw Okiru akasema.

Aidha, wanalipwa kupitia M-Pesa au chaguo la benki ya mkulima.

Licha ya hatua hiyo inayopaniwa kuletea wakulima wa mpunga afueni, NCPB inakiri kuwa na changamoto za kukausha mchele.

Bw Okiru, hata hivyo, alisema bodi hiyo inahimiza wakulima kusambaza mchele uliokauka.

“Kiwango cha unyevuunyevu wa maji kinapaswa kuwa asilimia 14.0,” afisa huyo akashauri.

Wakulima wa Mwea Irrigation Scheme wameandikisha kiwango cha juu cha zao la mchele 2023, kufuatia mvua inayoendelea kunyesha.

Taifa lilianza kupokea mvua mapema 2023, na walikuwa na hofu huenda mazao yao yakakosa kununuliwa vyema kutokana na kero ya mabroka.

Mawakala walikuwa wamevamia soko la mchele, ule ambao haujaongezwa dhamani wakiununua Sh65 kwa kilo.

Ni kutokana na kilio chao ambapo Rais Ruto aliahidi kuwaboreshea soko.

Akizungumza katika Kaunti ya Kirinyaga juma lililopita, kiongozi wa nchi alisema wakulima wanapaswa kuchungwa kwa njia zozote zile ili wasikandamizwe.

“Ninaelewa bei ya mchele ni duni, ila NCPB inapaswa kununua kila kilo kwa Sh85 wakulima wapate faida,” Dkt Ruto akasema.

Baadhi ya wakulima wameelezea kuridhishwa kwao na hatua ya Rais Ruto kuingilia kati na kuwasaidia.

Simon Njogu, ni mmoja wa wakulima wa mchele na anasema bei ya NCPB ni bora ikilinganishwa na ya mabroka – mawakala.

“Mwaka huu (2023), tumepata mazao ya kuridhisha ya mchele na mabroka walitaka kutukandamiza. Tunashukuru Rais kwa kuingilia kati kutuokoa,” Bw Njogu akaambia Taifa Leo Dijitali.

Serikali ya Kenya Kwanza, inayoongozwa na Rais William Ruto imeapa kukabiliana na mawakala katika sekta ya kilimo, ikiahidi kuimarishia wakulima soko.

  • Tags

You can share this post!

Ajira za kiufundi zakosa wafanyakazi wengi wakishikilia...

Seneta mwenye ulemavu wa macho asisimua kwa kuzindua albamu...

T L