• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Barua ya majonzi ya binti kwa Waziri Kindiki akimsaka mamake aliyetoweka Julai mtaani Kiria-ini

Barua ya majonzi ya binti kwa Waziri Kindiki akimsaka mamake aliyetoweka Julai mtaani Kiria-ini

NA MWANGI MUIRURI

“KWA Waziri wa Usalama wa ndani Prof Kithure Kindiki,

Ningetaka kwanza kukupa hongera kwa niaba ya familia yetu kufuatia kuteuliwa kwako kuwa waziri mwenye nguvu ndani ya Utawala wa Rais William Ruto. Mungu akuzidishie neema zake na akubariki katika majukumu yako.

Maana ya kukuandikia barua hii ni kukufahamisha kwamba mnamo Julai 1, 2023 mamangu mzazi Bi Esther Ruguru, 43, alitoweka kutoka mji wa Kiria-ini ulioko katika Kaunti ndogo ya Mathioya, Murang’a.

Mamangu alikuwa mhudumu katika hoteli yake ndogo na masaa ya jioni, kulingana na habari tumezipata hadi sasa, alikuwa apelekwe hepi na mwanamume mmoja ambaye tunamjua vyema.

Hata hivyo, asubuhi iliyofuatia mwanamume huyo alipatikana katika hospitali ya Kiria-ini akiwa na mejaraha ya kushambuliwa huku naye mamamngu akiwa hapatikani na simu yake ikiwa imezimwa.

Baada ya kumngojea arejee nyumbani pasipo mafanikio kwa siku nne, tuliripoti kutoweka kwake katika kituo cha polisi cha Kiria-ini na ambapo tulipewa nambari ya kisa kuwa 07/04/07/23.

Tangu hiyo siku, tumekuwa tukiahidiwa kwamba mamangu anatafutwa, kwa nyakati zingine baadhi ya watu wa familia yetu wakiagizwa watoe pesa kwa baadhi ya maafisa ndio tupatiwe habari muhimu kuhusu aliko mamangu.

Kwa sasa, mahangaiko yametuzidi kwa kuwa mamangu alikuwa akitulea mimi na dadangu na kakangu akiwa peke yake kwa kuwa baba yetu aliaga dunia.

Harakati zetu za kusaka mamangu zimetufichulia kuwa kuna washukiwa wawili wakuu katika kutoweka kwa mamangu huku mmoja wao hata akiwa na ujasiri wa kuja kwetu nyumbani na kutufichuliwa kwamba huenda aliuawa na mwili wake ukatupwa katika bwawa la Chinga lililoko Kaunti ya Nyeri.

Habari hizi zote tumekuwa tukiziwasilisha kwa maafisa wa polisi wa Kiria-ini lakini tumekuwa tukiambiwa kwamba tunazingatia sana uvumi badala ya kuwapa nafasi ya kufanya kazi yao.

Waziri Kindiki, jifahamishe na masaibu yetu kama familia ambapo kwa sasa mimi, dadangu na kakangu tumelazimika kuwa chini ya malezi ya nyanyangu wa miaka 71 na ambaye hana kazi wala msaidizi.

Umasikini ambao umetukumba kwa sasa unahatarisha masomo yetu ambapo mimi niko katika chuo kikuu cha Maseno, dadangu akingojea matokeo ya Kidato cha Nne huku kakangu akingojea kujiunga na Kidato cha Kwanza.

Mamangu ndiye alikuwa chakula, mavazi, malazi na malezi yetu na katika hali yake ya kutoweka kwa njia ambayo serikali imelemewa kutoa jibu kuihusu kunazidisha mahangaiko yetu.

Profesa Kindiki, tunashindwa kama familia kuelewa itakuwaje mtu atoweke kutoka mji mkubwa kama Kiria-ini, aliokuwa nao mara ya mwisho kuonekana wako na pia washukiwa wengine katika kisanga hiki wanajulikana lakini maafisa wa polisi walemewe kutoa jibu.

Imani yetu kwa serikali inayumba huku sasa mwezi wa saba ukikaribia kuisha tangu mama yetu atoweke na katika muda huo wote hakuna hata fununu ya maafisa wako kutuelekeza aliko aidha akiwa hai au akiwa maiti.

Waziri, uamuzi wa kukuandikia barua hii si wa kukukosea heshima wala kukutetesha lakini ni wa kukuuliza na kukusihi kwa heshima kuu uambie maafisa wa polisi wa Kiria-ini watueleze alikokwenda mama yetu.

Hawa maafisa wanatufanya tukose imani na serikali na wanatutwika msongo wa mawazo tukiwa katika hali ya sintofahamu kuhusu kilichomfanyikia mama yetu.

Profesa Kindiki, pitisha hongera zetu kwa Rais Ruto na wote wanaomsaidia kutawala taifa hili na kwa sasa natia tamati nikiwa na matumaini tele kwamba maafisa hawa watatuita katika kikao cha kutuelekeza aliko mama yetu katika hali yoyote ile.

Hatuamini kamwe kwamba taifa hili lina ubutu wa kiusalama kiasi kwamba mtu anaweza akaonekana mtaani akiwa mzima, akingojea mtu anayefahamika vyema na akiwasiliana kwa njia ya simu na hatimaye tuambiwe kwamba alitoweka pasipo kujulikana njia aliyofuata.

Ni mimi wako,

Carolyne Njoki,

05/12/23”

  • Tags

You can share this post!

Masoja walalamikia kufungiwa chooni na wahalifu wizi...

Mama mboga aliyedunga kisu mgeni aliyemvamia nyumbani...

T L