• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 3:09 PM
Masoja walalamikia kufungiwa chooni na wahalifu wizi ukitekelezwa  

Masoja walalamikia kufungiwa chooni na wahalifu wizi ukitekelezwa  

NA RICHARD MAOSI

WALINZI wa usiku katika kituo cha Mabasi cha Railways, jijini Nairobi wanalalamikia kupitishiwa mateso na wahalifu wanapofumaniwa wakitekeleza majukumu yao.  

Wanadai wahalifu huwanyatia usiku na kuwafungia ndani ya choo.

Tabia hiyo ya wahuni kusaka mwanya kutekeleza uhalifu, ni njia mojawapo kuwaadhibu na huwaacha kwenye uvundo mkali hadi asubuhi.

Visa hivyo vya uhalifu vinajiri wakati ambapo baadhi ya masoja wanarai serikali kuwaruhusu kumiliki bunduki, ili kuimarisha shughuli za ulinzi.

Hali kadhalika, wanataka nyongeza ya mshahara ikizingatiwa kuwa utendakazi wao unawatia katika hatari hasa uhalifu unapotokea.

Wahalifu huwa wanalenga kuvunja maduka madogo na kuiba chakula.

Mmoja wao ambaye anajitambulisha kwa jina Salim, mlinzi wa duka la soda, anasema wahalifu wengi huwa ni vijana kutoka mitaa ya Kibera, Mutindwa, Satellite na Mukuru kwa Njenga.

Ni hali ambayo imewaletea baadhi yao masaibu chungu nzima wengine wakiishia kufutwa kazi na waajiri wao.

“Waajiri wanaamini kuwa tunashirikiana na wezi kuwaibia mali zao,” akasema.

Anasema kituo cha Railways ni mojawapo ya maeneo ambayo hushuhudia shughuli nyingi nyakati za mchana, ila ifikapo usiku hubakia kuwa mahame.

Kulingana na Salim, Kituo cha mabasi cha Railways ni mojawapo ya mazingira hatari sana kufanyia kazi nyakati za usiku kwa sababu wezi hunyatia usiku na kuwakamata masoja kisha wanawafungia ndani ya choo na kuendelea na shughuli zao

“Kwa kawaida tunatumia muda wetu mwingi kulinda mali ila waajiri wetu wanatuelewa vibaya pale mali yao yanapoibiwa,”

Licha ya kwamba mshahara wa masoja wa usiku ni mdogo sana, bado wanapitia changamoto nyingi sana mojawapo ikiwa kuendesha shughuli zao katika maeneo hatari katikati mwa jiji hasa wakati huu ambao hali ya uchumi ni ngumu.

Alphonce Musau dereva wa magari ya Rembo kuelekea Kitengela, anasema amewahi kusikia visa kama hivyo ila hajawahi kushuhudia.

Anasema hili ni jambo la kawaida ingawa baadhi ya walinzi wamekuwa wakiumia kimyakimya.

Angependa maafisa wa polisi kuimarisha doria kwa sababu wahalifu wengi Railways hujifanya ni maafisa wa polisi.

  • Tags

You can share this post!

Kuku wageuka dhahabu Desemba 2023

Barua ya majonzi ya binti kwa Waziri Kindiki akimsaka...

T L