• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Berita: Upshaws yazidi kumpa umaarufu katika uigizaji

Berita: Upshaws yazidi kumpa umaarufu katika uigizaji

Na JOHN KIMWERE

NI miongoni mwa waigizaji chipukizi hapa nchini wanaopania kuibuka wasanii mahiri miaka ijayo. Sharon Musungu Berita ambaye kisanaa anafahamika kama Mzunye alianza kujituma kwenye masuala ya uigizaji miaka miwili iliyopita anakolenga kutimiza azimio la kuwa staa ndani ya miaka mitano ijayo.

Binti huyu mwenye umbo la kuvutia kando na uigizaji ni mwimbaji na voice over artist. ”Ndio nimeanza kucheza ngoma ninakolenga kukuza kipaji changu ninakoamini kuwa ninatosha mboga yaani ninaweza kufanya makubwa katika uigizaji,” anasema na kuongeza kuwa licha ya matamanio yake anafahamu sio mteremko inahitaji kujiamini na kujibiidisha mithili ya mchwa.

UPSHAWS

Kisura huyu aliyezaliwa mwaka 1993 anasema kuwa alivutiwa na masuala ya uigizaji baada ya kutazama filamu kwa jina ‘Disconnect’ ya muigizaji mahiri nchini Catherine Kamau maarufu Kate Actress. Anajivunia kushiriki kipindi cha Upshaws chini ya Hiventy Africa sehemu ya kiswahili ambayo hupeperushwa kupitia Netflix iliyoelekezwa na kuhariri na Eddie Butita kati ya wasanii wa humu nchini wanaozidi kupiga hatua katika sekta ya uigizaji.

”Kwenye kipindi hicho niliigiza sauti yake Kym Fields aliyekuwa akishiriki kama Regina Upshaw,” anasema. Katika mpango mzima ndani ya miaka miwili pekee ameshiriki filamu kadhaa ikiwamo ‘Njoro wa Uba,’ ‘Kina,’ na ‘Love me,’ kati ya zingine.

Sharon Musungu Berita maarufu Mzunye. …Picha/JOHN KIMWERE

Dada huyu anasema amepania kufuata nyayo zako Gina Rodriguez mzawa wa Marekani ambaye ameshiriki filamu iitwayo ‘Jane the Virgin.’ ”Ninalenga kufahamisha jamii kuwa filamu zina mafundisho mengi hasa kuhusu masuala ya utamaduni na mambo yanayoendelea katika maisha ya kila siku,” akasema.

”Tangia nikiwa mndogo nilitamani sana kuwa mwana habari maana nilipenda sana kuiga kati ya watangazaji mahiri nchini kama Catherine Kasavuli.”

Kwa waigizaji wa kimataifa anasema angependa kujikuta jukwaa moja na msanii wa filamu za Kinigeria ‘Nollywood’ Omotoba Jalade na Joslyn Dumas wa Ghana. Kwa wenzake wa humu nchini anasema anapenda sana kufanya kazi nao Kate Actress aliyeigiza filamu zingine kama ‘Nafsi,’ na ‘The Grand little lie,’ bila kusahau Jackie Matubia anayeshiriki kipindi cha Zora kinachoendelea kupeperushwa kupitia Citizen TV.

CHANGAMOTO

Anasema sekta ya uigizaji ina mapendeleo zaidi bila kuzingatia uwezo wa kufanya kazi. ”Kiukweli ni hali inayotuumiza maana unaenda majaribio lakini unakosa kuchukuliwa kisha waliotutangulia wanapewa nafasi,” anasema na kuongeza kuwa matukio hayo huwa yanawavunja moyo wasanii wanaokuja.

Hata hivyo anasema kuwa uigizaji ni ajira kama nyingine na inasaidie wengi wanawaume kwa wanawake. Dada huyu anashauri wasanii wenzie kuwa wanapojiunga na jukwaa hili kamwe wasitarajie kupata umaarufu wala hela haraka bali wafahamu wapo waliowatangulia. Anawaonya kuwa wasiwe na pupa ya kupata umaarufu maana wasipokuwa makini watatumiwa vibaya kwa jina la kusaidiwa kupanda ngazi haraka.

You can share this post!

Eastleigh FC yabanduliwa kutoka kipute cha Koth Biro

Sofia: Sijapata nafasi lakini sitavunjika moyo

T L