• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
BORESHA AFYA: Kwa nini ule nyama?

BORESHA AFYA: Kwa nini ule nyama?

NA PAULINE ONGAJI

KATIKA enzi hizi ambapo ni kawaida kwa mtu kuiga tabia za mwenzake kwa minajili ya umaarufu, si ajabu kukumbana na wale ambao kwa sababu zisizoeleweka wameamua kutokula nyama.

Japo inaeleweka kususia chakula hiki hasa kutokana na sababu za kiafya, wataalamu wanasisitiza kwamba sio jambo la busara kuchukua hatua hii hasa ikiwa hazikudhuru kiafya. Hii ni kwa sababu mwili unahitaji virutubisho vinavyopatikana katika chakula hiki.

Aidha wanasisitiza kwamba kila kikundi cha chakula kina umuhimu. Madini ya chuma ni kirutubisho muhimu kinachohusika na shughuli za kuzalisha damu. Ikiwa haupati madini haya ya kutosha, basi kiwango chako cha damu (himoglobini) kitapungua.

Kutokana na sababu kuwa himoglobini husafirisha oksijeni katika tishu za mwili, kiwango chake kikipungua, basi mwili unaanza kukumbwa na matatizo ya upungufu wa oksjeni, na hivyo kusababisha maumivu ya kichwa, kisunzi, kuzimia na hata moyo na figo kusitisha shughuli zao.

Ikiwa una upungufu wa madini ya chuma, basi mbali na chakula, unapaswa kutumia vijalizo vya madini yhaya ili mwili uweze kuzalisha himoglobini upesi, na hivyo tishu ziache kukosa oksijeni.

Mwili hufyonza virutubisho vya chuma upesi kutoka kwa nyama zaidi ya vyakula vingine.

Kutokana na sababu kuwa umeamua kutokula nyama, basi itakubidi upate virutubisho hivyo kutoka kwa vyakula vingine kama vile maharagwe, pojo, soya, mboga za kijani, matunda yaliyokaushwa kama vile zabibu kavu na nafaka zilizoimarishwa kama vile unga wa ugali.

Endapo hautapata virutubisho vinavyohitajika hata baada ya kula vyakula hivi huenda ukapungukiwa na damu mwilini na kuanza kushuhudia matatizo kama vile kisunzi.

Ikifika hapa, daktari atalazimika kukushauri kutumia vijalizo vya kuongeza madini ya chuma mwilini.

You can share this post!

JIJUE DADA: Jinsi ya kukabiliana na mafuta kiunoni

SHINA LA UHAI: Maziwa unayotumia huenda yadhuru afya yako

T L