• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
SHINA LA UHAI: Maziwa unayotumia huenda yadhuru afya yako

SHINA LA UHAI: Maziwa unayotumia huenda yadhuru afya yako

LEONARD ONYANGO Na KNA

MAZIWA ambayo wewe hutumia huenda yanahatarisha afya yako kimyakimya.

Ripoti ya utafiti uliofanywa katika Kaunti za Nakuru, Laikipia na Nyandarua – ambazo huzalisha kiwango kikubwa cha maziwa nchini – imefichua kuwa karibu asilimia 47 ya maziwa yanayotumiwa na wakazi yamesheheni viini vinavyodhuru afya.

Kulingana na utafiti huo, kati ya sampuli 493 za maziwa zilizopimwa, 237 zilibainika kuwa na bakteria wanaojulikana kama Pseudomonas spp wanaoweza kuathiri damu, mapafu na sehemu zingine za mwili.

Sampuli 209 za maziwa zilipatikana na bakteria wanaojulikana kama Escherichia coli (E. coli).

Kuna aina za bakteria wa E. coli ambazo husababisha magonjwa yanayoathiri mishipa ya mkojo, magonjwa ya mfumo wa kupumua, kuhara kati ya magonjwa mengineyo.

“Uwepo wa bakteria huonyesha kuwa maziwa huhifadhiwa katika mazingira machafu. Viwango vya ubora wa maziwa na usalama wake hutegemea namna yanavyokamuliwa na kuhifadhiwa. Aidha, maziwa hupata bakteria na sumu nyinginezo ikiwa anayeshika maziwa atakosa kusafisha mikono yake vizuri baada ya kutoka msalani,” inasema ripoti hiyo.

Utafiti huo uliendeshwa na wataalamu kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti kuhusu Mifugo (ILRI)- Kenya, Chuo Kikuu cha Wageningen na Taasisi ya Utafiti, Uholanzi, Chuo Kikuu cha Uppsala-Uswizi, ILRI-Vietnam na Chuo Kikuu cha Sayansi na Kilimo cha Sweden.

Ripoti ya utafiti huo inapendekeza hatua za haraka zichukuliwe na asasi husika katika ngazi za kaunti na kitaifa, wauzaji maziwa, wakulima na waongezaji thamani kwa maziwa ili kuimarisha ubora wake.

Hii ni kwa sababu maziwa yenye viwango vya juu vya bakteria na sumu nyinginezo ni hatari kwa afya ya wateja.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), vyakula vinavyosheheni bakteria, virusi, vimelea au mabaki ya kemikali husababisha maradhi ya kuhara, kansa kati ya maradhi zaidi ya 200.

Mtu mmoja kati ya 10 huugua baada ya kutumia vyakula vilivyoharibika na watu 420,000 hufariki dunia kutokana na magonjwa yanayosababishwa na vyakula visivyo salama kila mwaka.

Asilimia 40 ya wanaokufa kutokana na magonjwa yanayosababishwa na vyakula kama hivyo ni watoto wenye umri usiozidi miaka mitano. Hii ni sawa na jumla ya vifo 125,000 kila mwaka.

Sampuli za maziwa zilizopimwa katika utafiti huo, zilichukuliwa kutoka kwa wakulima na wauzaji wa rejareja katika maeneo ya vijijini na mijini.

Watafiti pia walibaini kuwa kiasi kikubwa cha maziwa yanayouzwa mitaani yametiwa maji. Maji hayo yanaweza kusheheni uchafu na viini vinavyosababisha maradhi.

Ilibainika kuwa vianzo vya pathojeni zilizopatikana ndani ya maziwa mbichi ni sehemu ya ndani na nje ya matiti, sehemu za nje za ng’ombe, mazingira ya kukama ng’ombe, vifaa vya kubebea na kuhifadhi maziwa na wahudumu.

Pathojeni zingine hatari zilizopatikana katika sampuli za maziwa zilizochunguzwa ni bakteria za Staphylococcus spp (asilimia 3.3 za sampuli) huku brucellosis antibodies zikipatikana katika asilimia 2.9 za sampuli hizo.

Watafiti waliwahoji wafugaji 50 wa ng’ombe wa maziwa katika vituo mbalimbali vilivyoteuliwa Nyandarua, Nakuru na Laikipia.

Aidha, walizuru miji 11 ikiwemo Ol Kalou, Oljororok na Engineer katika kaunti ya Nyandarua; Nakuru mjini, Njoro, Molo na Elburgon katika kaunti ya Nakuru; Nyahururu, Kinamba, Rumuruti na Nanyuki katika Kaunti ya Laikipia kufuatilia jinsi maziwa huhifadhiwa, husafirishwa na huuzwa katika vituo mbalimbali.

Watafiti walibaini kuwa maziwa kutoka maeneo ya vijijini yana viwango vya juu vya bakteria aina ya E.coli, Staphylococcus spp na Brucella abortus kuliko maziwa kutoka maeneo ya mijini.

Utafiti huo uligundua kuwa maziwa katika maeneo ya vijijini katika kaunti hizo tatu husafirishwa na kuuzwa katika mazingira machafu, hali inayoongeza uwezekano wa kuingiwa sumu na viini vinavyodhuru afya.

Walibaini kuwa maziwa husafirishwa kwa pikipiki ndani ya mitungi isiyo na barafu na katika mazingira ya joto ambayo huchangia bakteria kukua kwa haraka. Hali hiyo hushusha ubora wa maziwa.

“Katika maeneo ya vijijini ni nadra kwa wahusika kutumia mavazi ya kujikinga wanapouza au kusafirisha maziwa kulingana na kanuni za afya ya umma. Wahusika wengine huendesha shughuli zao bila vyeti vya afya na vile vya kusafirisha maziwa. Aidha ni vigumu kwa wahusika mashambani kupata vifaa vya usafi kama vile vyoo na mitambo ya kunawa mikono,” ripoti ya utafiti huo inasema.

Kulingana na takwimu kutoka kwa Bodi ya Maziwa Nchini (KDB) asilimia 70 ya maziwa yanayouzwa nchini huzalishwa na wakulima wadogo.

Hawa huuza maziwa ambayo hayajatayarishwa viwandani au yale ambayo yamehifadhiwa kitamaduni.

“Ni asilimia 30 pekee ya maziwa inayouzwa nchini Kenya ambayo huwa yametayarishwa kwa njia za kisasa na kampuni mbalimbali za maziwa,” KDB inaeleza katika ripoti yake ya mwaka wa 2021.

  • Tags

You can share this post!

BORESHA AFYA: Kwa nini ule nyama?

TAHARIRI: Mahakama ya Upeo ipewe nafasi kuamua kesi ya urais

T L